in , ,

Naiona Taswira ya Township Rollers kwenye kivuli cha Wolayta Dicha

Kupangwa na timu kutoka ushelisheli ilikuwa furaha kubwa kwa Yanga kwa
sababu furaha yao waliitengeneza kutokana na historia yao ya nyuma.

Historia ya Yanga ilikuwa imeshiba dhidi ya hivi vilabu vya visiwani
kama Comoro, Ushelisheli

Haikuwa jambo la kushangaza kusikia Yanga wameitoa timu kutoka katika
visiwa hivi kwa jumla ya magoli mengi.

Kwao wao walikuwa wanajipigia wapendavyo, hakuna ambaye angeweza
kuwazuia au hata kuwashauri kupunguza uzito wa vipigo kwa hizi timu.

Jambo hili liliwafanya wapate viburi kwa kiasi kikubwa kila walipoona
wanakutana na timu kutoka hizi sehemu.

Hata walipokutana na St. Louis walijua kabisa jana inaweza ikawa na
taswira ya leo, kitu ambacho kilikuwa tofauti sana.

Ushindani waliokutana nao haukuwa ushindani ambao umezoeleka kwa
kipindi cha nyuma, hakukuwepo na urahisi tena kwa Yanga kwenye mechi
hii.

Hadithi ya Yanga kuzitoa timu za ukanda huo kwa jumla ya magoli 2-1
ilikuwa hadithi ambayo ilikuwa haijazoeleka katika masikio na macho ya
mashabiki wa Yanga.

Siku za nyuma hadithi yao ilipambwa na majigambo ya kuzitoa timu za
ukanda huu kwa jumla ya magoli 7-1, 5-1 !, n.k

Hata walipovuka kwenda hatua ya awali, kazi ilionekana rahisi sana kwa
Yanga kwa sababu walikuwa wanaenda kukutana na timu ya Township
Rollers kutoka Botswana.

Kwa macho ya kawaida ilikuwa mechi rahisi sana kwao kwa sababu
Township Rollers ilikuwa inatoka kwenye nchi ambayo kiwango chake cha
mpira siyo kikubwa sana.

Hivo wengi walitegemea Yanga ingeweza kufanya vizuri na kuwatoa hawa
watu, ƙlakini hadithi ikasomeka kinyume na Yanga ikatolewa katika
mashindano haya na kushushwa kwenye kombe la shirikisho barani Afrika.

Sehemu ambayo anaenda kukutana na timu ambayo inaonekana pia kama timu
isiyotisha sana kwa sababu imetokea katika nchi ambayo kiwango chake
cha soka barani Afrika siyo kikubwa sana.

Hadithi ya Yanga msimu huu inakuwa ile ile tangu mwanzo mpaka sasa
hivi inapofika hatua hii.

Tangu mwanzo Yanga inaonekana imekutana na timu ambazo siyo tishio kwa
kiasi kikubwa kila zikitamkika midomoni mwa watu kwa sababu hata
historia zao huko nyuma hazikuwa na historia ya kutisha.

Yanga waliona ukawaida usio wa kawaida kila walipokuwa wanakutana na
hizi timu. Ndiyo maana walicheza kawaida kwa sababu walijua wanaenda
kukutana na timu za kawaida.

Hakukuwepo na njaa kwenye miguu ya wachezaji wa Yanga kitu
kilichopelekea hata kushindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani katika
michezo yote miwili iliyochezwa hapa nyumbani.

Nafasi nyingi za wazi walikosa, nidhamu ya matumizi ya nafasi ilikuwa
haipo ndani ya wachezaji wa Yanga.

Mchezo wa kwanza dhidi ya St.Louis walipoteza mpaka penalti,
wakashinda ushindi mwembamba, ushindi ambao haukuwapa asilimia kubwa
ya kupita. Hata walipoenda kwenye uwanja wa ugenini mechi ikaonekana
ngumu kwao pia.

Ugumu huu waliutengeneza pia kwenye mechi dhidi ya Township Rollers
waliyocheza hapa nyumbani. Hadithi ilikuwa ile ile, Yanga walipoteza
nafasi nyingi hapa nyumbani , hawakuwa na nidhamu ya matumizi ya
nafasi katika uwanja wao wa nyumbani, kitu kilichopelekea mechi iishe
hapa nyumbani.

Tatizo la kwanza la Yanga katika mashindano ya kimataifa msimu huu ni
kutomheshimu mpinzani wao kwa kila hatua ambayo walikuwa wanaipiga.

Hali ambayo ilisababisha wao kujiamini sana , kujiamini kwao
kuliwaondolea umakini. Hii ilikuwa rahisi kwao kukosa nidhamu ya
matumizi ya nafasi walizokuwa wanazipata.

Hivo nidhamu ya matumizi ya nafasi kiwe kitu cha msingi katika mchezo
huu dhidi ya Deycha ya Ethiopia. Wasiruhusu ile hali ya kujiamini sana
ambayo itawaondelea hata umakini ndani yao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SALAH ANAWEZA KUMSHINDA MESSI, LAKINI NI ZIADA YA MAHITAJI NDANI YA BARCELONA

Tanzania Sports

KUKOSEKANA KWA NEYMAR KWENYE MICHEZO YA KIRAFIKI NI FAIDA KWA BRAZIL