in , , ,

Mourinho: Tumeumia kumpoteza Lampard

 

*Hatima ya Drogba mikononi mwa Abramovich

 

Chelsea wanapoelekea kulitwaa taji la Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya ukame wa miaka mitano, Kocha Jose Mourinho ana masikitiko moyoni mwake.

 

Hayo ni kutokana na kumpoteza mmoja wa mashujaa wa Stamford Bridge, Frank Lampard ambaye mkataba wake ulimalizika na hakuna aliyefanya jitihada kumpa mwingine.

 

Lampard (36) aliondoka baada ya kuwachezea Blues mechi 648 na kufunga mabao 211, ambapo hadi sasa anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi.

 

Mourinho anashindwa kuamini kilichotokea, ambapo Lampard alielezwa kusajiliwa na New York City FC wa Marekani, ghafla akatolewa kwa mkopo kwa Manchester City kabla ya ofa hiyo kugeuzwa kuwa usajili wa kudumu.

 

Kocha huyu anasema kwamba wamepoteza mchezaji aliyekuwa anatisha, mbaya zaidi ni kwamba alirudi England na kujiunga na wapinzani wao wakubwa kwenye EPL.

 

Hata hivyo, uwapo wake City haujawasaidia kutetea ubingwa , na pengine ndiyo faraja pekee kwa Mourinho juu ya mchezaji huyu wa zamani wa Timu ya Taifa ya England na klabu ya West Ham, alikoanzia soka ya kulipwa.

 

Kiungo huyu veteran alicheza mechi 40 kwenye msimu wake wa mwisho Chelsea, na alitumia kila aina ya fursa kupata mabao yanayomweka kwenye rekodi ya klabu hiyo.

 

Baada ya kuhamia City, Lampard amepata kucheza dhidi ya Chelsea na Mourinho anasema aliumia lakini anafurahi kwamba maisha yanaendelea.

 

“Kwa kweli tulipoteza mtu ninayemchukulia kuwa mmoja wa wachezaji watano muhimu zaidi katika historia ya Chelsea: Frank Lampard. Lakini aisha yanaendelea, ni muhimu kufikiria yajayo na kujijenga zaidi.

 

“Nasema hivyo kwa sababu Chelsea tulipoteza aina ya mchezaji anayebadili mchezo, anayewapa ushindi; ukiangalia mabao aliyofunga, mchezaji asiyeumia, mwenye nidhamu, mchezaji nyota.

 

Naam tulimpoteza, lakini maisha yanatakiwa kuendelea,” anasema Mourinho.

 

Bado anaendelea kuzifumania nyavu, kwani hadi wikiendi iliyopita alikuwa ameshafunga mabao saba licha ya kucheza mechi chache

 

WATAMWACHA DROGBA NAYE AONDOKE?

 

Wakati Mourinho akimlilia Lampard, ni zamu ya Chelsea kufanya uamuzi juu ya mkongwe mwingine, Didier Drogba aliyerejea Chelsea msimu uliopita.

 

Baada ya kuwatumikia Blues tangu 2004 hadi 2012 mkataba wake ulipomalizika na kwenda Shanghai Shenhua ya China kisha

Galatasaray wa Uturuki, alirejea Stamford Bridge mwaka 2014.

 

Mkataba wa mwaka mmoja wa Drogba (37) unamalizika kiangazi hiki na kocha Mourinho hana uamuzi juu ya mchezaji huyu wa kimataifa wa Ivory Coast.

 

Mourinho anasema hilo ni suala la klabu, na kwa maana hiyo mmiliki Roman Abramovich ndiye atatoa uamuzi juu ya mkongwe huyu aliyeanzia soka ya kulipwa Ufaransa akiwa na umri wa miaka 18 katika klabu ya Le Mans.

 

Msimu huu Drogba amecheza mechi 27 na bila shaka atafurahi kwamba kurejea kwake kumewaletea Chelsea kombe, japokuwa hayupo kwenye kiwango kama cha awali.

 

Mourinho alipoulizwa wiki kadhaa zilizopita iwapo Drogba angekuwapo klabuni msimu ujao, Mreno huyu alijibu kiaina, akisema anachojua ni kwamba angekuwapo kwa ajili ya mechi iliyokuwa inafuata, maana Diego Costa alikuwa majeruhi.

 

Zipo taarifa, hata hivyo, kwamba Mourinho ana nia ya kusajili mshambuliaji chipukizi, na wanaopewa nafasi zaidi ni Charlie Austin wa QPR na yule wa Inter Milan, Paulo Dybala wanaoweza kuchukua nafasi ya veterani huyu.

 

Hata hivyo, kocha anasema suala litaamuliwa na tajiri mwenyewe lakini pia anasema mchezaji huyu amekua sehemu kubwa ya historia ya Chelsea.

 

Huyu ndiye aliyefunga bao lililowapa Chelsea ubingwa wa Ulaya, lakini bado akaachwa usajili uliofuata.

 

“Nadhani hili ni suala la klabu. Hili ni suala la bwana Abramovich…anamtaka kufanya kile anachotaka katika klabu hii.

“Lakini bwana Abramovich ndiye atamwambia. Itabidi aamue lakini ni wazi yeye ni sehemu kubwa ya historia ya klabu hii,” anasema Mourinho akielekea kukwepa kuweka wazi mambo.

 

Zimekuwapo tetesi kwamba Drogba anaweza ama aendelee kucheza kidogo au apewe kazi ya kocha msaidizi au nyingineyo klabuni.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Klabu za EPL na faida ya £198m

MAJERUHI LIGI KUU ENGLAND