in , , ,

Mourinho katika mtihani mgumu zaidi

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, Jumapili hii anaingia kwenye mtihani wake mkubwa zaidi wa msimu, swali likiwa ni jinsi ya kumzuia Pep Guardiola na Manchester City wake.

Mechi ya watani wa jadi wa Jiji la Manchester inapigwa Old Trafford – ambako kwa muda sasa Mashetani Wekundu hawajafungwa, lakini safari hii Guardiola anakuja na kikosi kikali ambacho hakielewi chochote zaidi ya ushindi.

Utakuwa ni mtanange wa kuvutia, lakini ambao kabla ya kuanza una maswali mengi, hasa kwa United ambao wamekuwa wakati mwingine ‘wakitegea’ kucheza na badala yake kutafuta mbinu ambazo hata wakongwe wa hapo wamezichukia.

Ikiwa United watapoteza mechi, basi pengo kule juu litakuwa kubwa – pointi 11 wakati ikiwa watashinda zitapungua hadi tano lakini Mourinho atakuwa na tambo kubwa sana, ikizingatiwa jinsi amekuwa akichagizwa kwa mifumo na uchaguzi wake wa namna ya kucheza.

Mourinho amekuwa na kawaida ya kutwaa ubingwa anapokuwa katika mwaka wa pili kwenye klabu, lakini asipoweza kuwapiga City, uwezekano huo kwa wakati huu unaweza kuchukuliwa kwamba upo hatarini japokuwa kihesabu bado unawezekana.

Matukio huwa na tabia ya kupita hata katika hali isiyotarajiwa na haijulikani iwapo City wataweka rekodi kwa kushinda mechi ya 14 mfululizo katika msimu au ndio Mourinho ataonesha ufundi wake na njia za kupita kuwafunga City, avunje rekodi yake Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.

City wamepoteza alama mbili tu – nazo ni kwa kwenda sare hivyo wanaingia uwanjani wakiwa hawajui kufungwa huwa vipi msimu huu. Mourinho bado haijulikani hasa mfumo wake ni upi lakini Guardiola anajulikana, na ana kikosi chenye vipaji na wachezaji walio juu kwa ari.

Mourinho pia inabidi aongeze umakini pia, kwa sababu ujio wake huu unaweza kumalizika bila kikombe, kwani ni kawaida yake kuwa na matatizo na klabu msimu wa tatu, hivyo anatakiwa kukazia buti msimu huu apate matunda.

Mourinho ana kazi ngumu ya kuzizuia silaha za Guardiola, kuanzia kwa Raheem Sterling mwenye kasi ya ajabu, uchu wa mabao na ufungaji mzuri na mwenzake Leroy Sané.

Lakini pia kuna akina David Silva na Kevin De Bruyne ambao wamekuwa wazuri sana kwenye pasi na kupanga mashambulizi. Mourinho anaweza kuamua yale yale ya ‘kuegesha basi’ kwa wachezaji wake kubaki kule nyuma katika wingi wao na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

City wamekuwa na usahihi wa utoaji pasi kwa asilimia 88.8 msimu huu na hawaonekani kuwa timu yenye hofu hata kidogo wachezaji wake wanapokuwa na mpira. Mourinho kuna wakati huweka ile beki tatu yake lakini dhidi ya timu zinazoweka hivyo – CSKA Moscow, Arsenal, Watford, Chelsea na Tottenham Hotspur.

Hata hivyo, kwa sababu za watu wa kutumia, anaonekana kwamba Jumapili hii anaweza kutumia mbinu hiyo. Ikiwa Marouane Fellaini yu timamu, kuna uwezekano wa kumchezesha sambamba na Nemanja Matic pale nyuma na Ander Herrera akisogezwa mbele katika mfumo mchanganyiko wa 4-3-3/4-2-3-1.

Ni ngumu kuona iwapo United watakuwa na ujasiri wa kutumia 4-2-3-1 wakiwa na wachezaji wanne wabunifu. Kuwa na mtu mmoja wa ziada nyuma kunawapa urahisi wa kujiegesha nje kidogo ya eneo la penati ambako City hawawezi kuruhusiwa kuvinjari.

Man United wakimudu kuwanyima pumzi City, basi utakuwapo ushahidi mwingi kwamba wanaweza kuwafunga mabao kwa sababu kwa asili ya falsafa ya Guardiola ni kwamba wakati wote watakuwa katika hatari ya kushambuliwa kwani hawajiegeshi nyuma bali wanasonga mbele na kusakata soka ya kuvutia.

Lakini City wanajidai kwa kuwa na moja ya ngome imara zaidi lakini bao la

Angelo Ogbonna la West Ham dimbani Etihad Jumapili iliyopita lilikuwa la kwanza la kichwa City kukubali msimu huu. City hawana walinzi warefu kivile hivyo United wanaweza kuwatumia Romelu Lukaku na Fellaini wakati wa mashambulizi ya kona, na watakuwa tishio hapo.

Walipocheza dhidi ya Watford na Arsenal, kiungo kilikuwa kati ya Paul Pogba na Jesse Lingard na mambo yaliwaendea vyema, hivyo Pogba aliye nje kwa mechi tatu kwa sababu ya kadi nyekundu ataacha pengo kubwa. Amekuwa kiungo lakini Jumapili hii United labda itabidi waende moja kwa moja tu, wakitumia urefu wa Lukaku na kuwagawia akina Anthony Martial na Lingard mipira.

Ni kwa kufanya hivyo kuliwapa ushindi dhidi ya Spurs, United walipotulia nyuma kuwachanganya Spurs lakini City si watu wa kuwachanganya hivyo, watawapeleka mchakamchaka na nionavyo itabidi kila timu ioneshe soka kwenye maeneo yote ya uwanja na si kujiegesha pale nyuma kuzuia mabao.

Lakini, suala hapa si City kuwzuia United kufunga. Mchezo utaamuliwa na jinsi United watakavyoweza kuwakatalia City na kasi yao ya mawimbi kwenye ushambuliaji.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ZANZIBAR ANZENI HAPA NDIPO NITAWASIFIA NA MIMI

Tanzania Sports

MBIO ZA UBINGWA ZIMEFIKIA UKINGONI ?