in

Mnyukano wa European Super League na UEFA

MOTO wa soka umewaka barani Ulaya. Makumi ya timu wamekubaliana  kuanzisha Ligi maalumu iitwayo European Super League ambayo  inajumuisha vilabu vigogo vya soka batrani humo. mjadala wa kuanzishwa European Super League umekuwa mkubwa na kujikita kwenye masuala ya  haki za televisheni na fedha. Makala haya yanakuletea masuala muhimu  kuhusu European Super League.  

Ni timu gani zimekubali kucheza European Super League? 

Klabu 12 za Ligi mbalimbali barani Ulaya zimekubaliana kuanzisha Ligi yao  ya Mabingwa. Klabu hizo ni; Manchester United, Tottenham  Hotspurs, Real Madrid,Atletico Madrid, Juventus, AC  Milan,Barcelona,Chelsea,Liverpool,Inter Milan, Man City na Arsenal. EPL  inaongoza kuwa na timu nyingi ambazo ni Man City, Chelsea, Liverpool,  Arsenal, Man United na Tottenham Hotspurs.  

Je, timu za Ulaya hazitaki muundo mpya wa Ligi ya Mabingwa? 

Tanzania Sports
Baadhi ya Nyota wa EPL

UEFA wanataka kupanua muundo wa mashindano hayo kutoka timu 32  hadi 36 kuania mwaka 2024 na kuendelea. Idadi ya mechi itaongezeka kwa  asilimia 100 kutoka mechi 125 za sasa hadi 225 kwa muundo mpya. Pia  wanataka mechi hizo kuchezwa kila mwezi wakati Ligi za ndani zikiendelea.  Klabu zimekataa mpango mpya wa UEFA kwa sababu wanahofia endapo  utakubaliwa na kutekelezwa maana yake utashusha thamani ya Ligi Kuu za  ndani. 

Chini ya muundo mpya wa UEFA, timu mbili kila msimu zitatoka Europa  League na hatua za awali za nafasi za kufuzu Europa zitapelekwa Ligi ya  Mabingwa Ulaya. Utaratibu huo utatumika kote Ulaya, lakini ukweli ni  kwamba utahusisha timu 400 zile zilizoko kwenye orodha ya ubora  inayotolewa na UEFA.

Hilo litakuwa na maana timu zinazomaliza Ligi Kuu zikwa nafasi ya  tano,sita au saba zitaingizwa daraja la timu za juu chini ya orodha ya timu  bora zenye viwango vya UEFA. Nafasi mbili za Ligi ya Mabingwa  zitaamuliwa namna hiyo kuanzia mwaka 2024 chini ya mapendekezo mapya  ya UEFA. 

Tanzaniasports imefanya uchambuzi wa mapendekezo hayo kulingana na  viwango vya timu mbalimbali vilivyotolewa na UEFA kwa misimu ya 2019- 2020, 2018-2019 na 2017-2018. Kwa msingi huo timu zitakazonufaika na  mapendekezo mapya ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zitakuwa kama ifuatavyo; 

Msimu wa 2019-2020; timu za Tottenham Hotspurs (ilimaliza nafasi ya sita  RPL) na AS Roma (ilimaliza nafasi ya tano Ligi Kuu Italia). Msimu wa  2018-2019; Timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya tano EPL, Sevilla ililazima  nafasi ya sita La Liga. Msimu 2017-2018; timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya  sita EPL na Sevilla ilimaliza nafasi ya saba La Liga. 

Tatizo ni fedha za zawadi za mashindano 

Tangu mwanzo European Super League imelenga kupata mapato makubwa  kuliko ya sasa yanayotolewa na UEFA. Kwa waendeshaji wa European  Super League wamepanga kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza anayetwaa  ubingwa wa ligi yao kiasi cha pauni milioni 82. Msingi wa hoja hiyo ni  kutokana na zawadi za UEFA, kwamba inatoa fedha ndogo kuanzisha  zawadi za mashindano na mshindi wa kwanza, hadi haki za Televisheni na  Streaming. 

Je UEFA wamechukua hatua gani? 

Shirikisho la,soka Ulaya nalo linatarajiwa kuziadhibu timu zote  zilizokubaliana kuanzisha European Super League. Kwamba klabu zote 12  zitaadhibiwa kama ifuatavyo; zitaondolewa kwenye mashindano ya Ligi za  ndani kuanzia msimu ujao, kila mchezaji atakayeshiriki European Super  League atafungiwa kushiriki fainali za Kombe la dunia mwaka 2022, kila 

kiongozi wa soka atakyejihusisha na European Super League atafungiwa  kushiriki shughuli zozote za mashindano ya Shirikisho la Soka barani Ulaya  (UEFA) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). UEFA itafungua mashtaka  kudai fidia ya pauni bilioni 50 kwa kila klabu. 

Je hofu ya UEFA ni nini? 

Upo wasiwasi kuwa kupanuliwa kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa  kutashusha thamani ya Ligi za ndani barani Ulaya kwa sababu mapato  yanayotokana na matangazo yatakuwa makubwa zaidi hivyo kuwavutia  wawekezaji zaidi. pia timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa huenda zikawa  tajiri zaidi kuliko zingine zinazoshiriki Ligi ya ndani bila kufuzu  mashindano hayo hivyo kuchangia mapato yao kuporomoka. 

Majadiliano ya mapendekezo mapya yanahusisha vyama vya soka 55, Ligi  Kuu za Ulaya na chama cha timu za soka. hata hivyo UEFA imepania  kukamilisha mapendekezo hayo mapema kabla ya kufanikiwa mpango wa  kuanzishwa kwa European Super League ambao unasimamiwa na Real  Madrid. 

Je ladha ya klabu zitakuwa zilezile kwenye soka? 

Si jambo rahisi hadi sasa, kwa sababu sheria nyingi za Ligi za ndani  zinawabana vilabu husika. Pia wapo makocha wanaopingana na wazo la  kuanzisha European Super League, kwa mfano kocha wa Liverpool ambaye  amesema, “Nategemea wazo hilo litakwama na halitotokea. Kwa mimi  Super League tunayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kuna umuhimu gani kwa  mfano Liverpool kupambana na Real Madrid kwa miaka 10 mfululizo?  Hakuna mtu atakayetamani kuona hilo, linakinaisha,” 

Kimsingi hoja ya Klopp ni sawa na kusema European League itakinaisha  kuona Juventus na Madrid zinacheza mara kwa mara tena mfululizo kwa  miaka 10 hivi. Hoja hiyo ni sawa na alivyowahi kusema Rais wa FIFA Giani 

Infatino kuwa AFCON inakinaisha kwa sababu inachezwa kila baada ya  miaka miwili badala ya kuwekwa miaka minne minne. 

Je ni rahisi kuzifuta klabu zitakazojiunga European Super League? 

Tanzania Sports
Vilabu vya Ligi ‘MPYA’

Kimsingi miongoni mwa watu walioanzisha mpango huo ni rais wa Real  Madrid, Florentino Perez, hivyo inaelekea wamejipanga vizuri. Fedha ndio  kila kitu kwenye mashindano ya mpira wa miguu, kwa vyovyote vile  walikuwa wanafahamu kuna vita kubwa itakuja na jinsi ya kukabiliana nayo.  Haiwezekani vyama vya soka kuzifuta klabu hizo kwneye Ligi zao. Vilabu  hivi vina mtaji mkubwa wa fedha na mashabiki hivyo kuwapa changamoto  vyama vya soka. 

Je tishio la UEFA na FIFA linatafsiriwa vipi? 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tmu zilizothibitisha kushiriki European  Super League, Florentino Perez ameviambia vyombo vya habari kuwa  hawaogopi vitisho vya mashiriko ya FIFA na UEFA, na tayari wamejipanga kuanzisha mashindano yao ya EURO kwa bara la Ulaya na Fainali za  Kombe la Dunia. 

Kwanini FIFA inakataa Ulaya na kutaka African Super League? 

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, Giani Infatino anakumbukwa kwa  kutoa wazo la kuanzisha mashindano ya African Super League, lakini  ameungana na UEFA kukataa European Super League. Hii ina maana gani?  Je FIFA walitaka kutumia African Super League kupima mambo katika  uwanda wa soka? 

Mchambuzi maarufu wa soka Afrika mashariki, Israel Saria anasema,  “Mashindano ya soka huanzishwa yapate baraka za FIFA. Kwa bara la  Afrika bado haliwezi kusimama peke yake bila kusaidiwa, hivyo kwa klabu  za Ulaya zinataka kupandisha dau la mashindano ya Ligi ya  Mabingwa, Michuano ya Euro na Kombe la Dunia,”

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Liverpool

Ni wakati wa Liverpool kufanya mabadiliko

Tanzania Sports

Kwanini PSG na Bayern Munich hazipo European Super League?