in , , , , ,

Mkenya ashinda Tour de France


*Man U wampandia dau Fabregas, lakataliwa
*Luis Suarez aripoti kambini Liverpool lakini…

Nderemo na vigelegele vimetawala nchini Kenya, wambapo raia wa nchi hiyo wanasherehekea ushindi wa Chris Froome kwenye mbio za baiskeli katika michuano ya Tour de France.
Wakenya wanamchukulia kuwa ni raia wao, japokuwa rasmi anatambulika kuwa wa Uingereza; aliyezaliwa nchini Kenya na anazungumza lugha nyingi, ikiwamo Kiswahili.
Mwenyewe hakujua kama pangekuwa na sherehe kubwa baada ya kuibuka mshindi kwenye mbio za baiskeli, lakini alikutana na rafiki zake waliofika kutoka Afrika kwa ajili ya kumuunga mkono na kufurahi pamoja naye.
Tofauti na alivyotarajia, usiku wa Jumapili hii hautasahaulika kwake, kwa jinsi rafiki zake wa tangu enzi za shule walivyokusanyika naye, wakimvisha mataji na kufurahia ufanisi wake kwenye mchezo huo mkubwa.
Mapenzi ya Froome kwenye ulimwengu wa mbio za baiskeli yalianza pale mama yake alipomwomba nguli wa kuendesha baiskeli milimani, David Kinjah kumfundisha mwanawe mchezo huo, wakati huo akiwa na umri wa miaka 11 tu.
Alichanua vizuri zaidi kwa mara ya kwanza mwaka 2011, pale alipomaliza nafasi ya pili, nyuma ya Bradley Wiggins, katika mashindano ya Tour of Spain.
Matokeo hayo yalimweka sawa na ushindi wa pili aliopata Robert Millar mwaka 1987 katika Giro d’Italia, akiwa Mwingereza aliyekuwa nafasi ya juu zaidi katika mashindano ya aina hiyo yenye umaarufu mkubwa.
Mwaka jana, Froome alimaliza katika nafasi ya pili tena kwenye Tour de France, ambapo msaada wake katika mbio za baiskeli milimani ulikuwa muhimu sana kwa ushindi wa Wiggins. Mwaka huu kumekucha kwake, baada ya kufanikiwa kuiongoza Team Sky kwenye mashindano hayo kwa mafanikio makubwa.
Kocha Kinjah anamkumbuka Froome, akisema kwamba alipofika kwa mara ya kwanza, alishangaa kwa jinsi alivyokuwa amejawa aibu, lakini akamwambia mama yake kwamba angeweza kumsaidia, maana mwenyewe alionesha kudhamiria kupambana.
Hata katika ushindi wake wa mwaka huu, Froome hajaisahau Kenya na watu wake, kwani alivaa vitu mbalimbali vyenye nembo ya bendera ya taifa la Kenya.
Froome ambaye rasmi ni Mwingereza, anasema kwamba bado hana uhakika nchi gani anaipenda zaidi kati ya Uingereza na Kenya, akisema mapenzi yake yamegawanyika baina ya mataifa hayo mawili na watu wake.
“Kweli nimegawanyika kati ya maeneo hayo mawili…nikienda Kenya wakati jamaa wa forodha wanaponijia na kunipa tabasamu, najiona narudi nyumbani kwangu,” anasema Froome.
Amekuwa na uwezo mkubwa katika mafunzo na hatimaye mbio za baiskeli za kilometa 100
Akiwa Afrika Kusini, Froome aliwahi kujaribu michezo ya rugby na kriketi, lakini baadaye aligundua kwamba kipaji chake kilikuwa kwenye kuendesha baiskeli katika mashindano mbalimbali kwenye barabara za nchi hiyo, hasa maeneo ya Bloemfontein.
Kiongozi wa Sky, Dave Brailsford, anasema si ajabu huu ni mwanzo tu wa zama za mafanikio makubwa kwa Froome.
“Timu yetu haitajengwa kwenye msingi wa mtu mmoja, lakini ni wazi kwamba hizi ni zama za Froome, ni mmoja wao, kama si bora zaidi katika mbio za baiskeli duniani kwa sasa, na hakuna sababu ya kutoamini kwamba kasi hiyo itaendelea,” alisema Brailsford Jumamosi kabla ya mafanikio yenyewe.
DAU LA MAN U KWA FABREGAS LAKATALIWA

Klabu ya Manchester United imeendelea kumsaka kiungo mahiri wa Barcelona aliyekwenda huko akitoka Arsenal, Cesc Fabregas.
Hata hivyo, dau lao lililoongezwa kutoka pauni ilioni 25 hadi 30 limekataliwa tena na Barca, ambao awali walisema Mhispania huyo hana nia ya kurejea Arsenal.
United wanaoongozwa na kocha mpya, David Moyes, wamekuwa wakiendesha kampeni ya kumnasa Fabregas kupitia kwa Mwenyekiti Mtendaji wake, Ed Woodward.
Hii ilikuwa moja ya rekodi kubwa zaidi katika utoaji madau ya usajili, kwani Mashetani Wekundu hao walimsajili Dimitar Berbatov kutoka Tottenham Hotspur kwa pauni milioni30.75; kisha Rio Ferdinand kutoka Leeds United kwa pauni milioni 30.
Wengine waliosajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha hapo Old Trafford ni Juan Sebastian Veron aliyetoka Lazio kwa pauni milioni 28.1;
Wayne Rooney aliyeuzwa kutoka Everton ya Moyes kwa pauni milioni 27 na Robin van Persie aliyetoka Arsenal mwaka jana kwa pauni milioni 24.
“Ukishapenda kumchukua mchezaji fulani, basi unajaribu kutumia kila fursa ili kumpata, name ningefanya hivyo, nadhani mambo yatakwenda vizuri,” akasema Moyes, akizungumzia tamaa yao ya kumsajili Fabregas.
Fabregas alianzia soka yake kwenye chuo cha mafunzo ya vijana cha Barcelona, maarufu kwa jina la La Masia, kabla ya kusaini Arsenal mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 16.
Ametokea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Arsenal, kabla ya kuwa nahodha Novemba 2008, na alikuwa mchezaji mdogo zaidi Arsenal, akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177 walipopepetana na Rotherham United kwenye Kombe la Ligi Oktoba 2003.
Alikuwa katika kikosi cha Arsenal kilichowacharaza Manchester United kwa penati kwenye fainali ya Kombe la FA mwaka 2005 walipotwaa kombe lao la mwisho na amekaa na The Gunners kwa miaka minane, akasaini Barca kwa mkataba wa miaka mitano mwaka 2011, mkataba wenye thamani ya pauni milioni 25.4.
Hata hivyo, kukataliwa kwa dau hilo kubwa, kunaonesha dhamira ya ama Barca inayosaka kocha mpya kubaki na Fabregas au mchezaji mwenyewe kutaka abaki Camp Nou.

SUAREZ ARIPOTI KAMBINI LIVERPOOL

Luis Suarez ameripoti katika kambi ya Liverpool walio ziarani nchini Australia, na atafanya mazungumzo na bosi Brendan Rodgers juu ya hatima yake.
Mchezaji huyo aliyekuwa likizo baada ya kumaliza michuano ya Kombe la Mabara iliyofanyika Brazil. Aliwasili Melbourne Jumapili hii.
Anatamani kuondoka Liverpool ili achezee timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Arsenal wameshapeleka dau la pauni milioni 30 lililokataliwa na Wekundu hao.
Suarez (26) amekuwa akisema anataka kuondoka Uingereza kwa kuwa hapendwi na vyombo vya habari, lakini pia akilaumu Chama cha Soka England kinachompa adhabu kali, ikiwamo ya kukosa mechi 10 baada ya kutiwa hatiani kwa kumng’ata Branislav Ivanovic wa Chelsea kwenye mechi yao ya mwisho ya ligi kuu msimu uliopita.
Suarez alijiunga Liverpool akitoka Ajax ya Uholanzi Januari 2011 kwa thamani ya pauni milioni 22.7, na amefunga mabao 51 katika mechi 96, kabla ya hapo aliwafungia Ajax mabao 49 katika mechi 48. Kwa Uruguay, amewafungia mabao 31 katika mechi 62.
Rodgers anatarajiwa kumweleza Suarez kwamba ana deni kwa klabu hiyo, kwa vile imesimama naye na kumuunga mkono katika nyakati zote alipokuwa matatani. Anasubiri kujua kama Arsenal watapandisha dau hadi pauni milioni 40 wanazomkadiria Suarez kama thamani yake.
Hata hivyo, Real Madrid walishaonesha nia ya kumtaka Suarez, japokuwa wamesita kidogo, hasa baada ya mpango wa mshambuliaji wao, Gonzalo Higuain kwenda Arsenal kusuasua.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

*LIGI KUU YA VODACOM 2013/2014 KUANZA AGOSTI 24*

TUMEJIANDAA KUIKABILI UGANDA- KIM