in , , ,

MISINGI TUMEIACHA, TUNASINGIZIA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI

Utimilifu wa maisha hutimia kipindi ambacho mwanadamu anapokuwa anapitia pande zote mbili za maisha (huzuni na furaha).

Maisha hayawezi kuitwa maisha kipindi ambacho mwanadamu anapitia hatua za furaha pekee, hatua za huzuni huitajika ili kukamilisha neno “maisha”.

Huzuni ambayo huja na matatizo, matatizo ambayo ni msingi wa kuimarika kwa mwanadamu yoyote.

Kuna vitu vingi hubadilika kipindi ambacho mwanadamu anapokumbwa na matatizo. Kuna watu huanguka na kushindwa kuinuka kabisa wanapokumbwa na matatizo na kuna wengine huanguka kisha wakainuka wakiwa imara na kuanza safari yenye mafanikio makubwa.

Kwa kifupi tunatofautiana jinsi ya kukabiliana na matatizo, mapokeo yetu ni tofauti ndiyo maana hata matokeo yetu ni tofauti.

Kuna wakati tatizo huja na kushindwa kufikiria njia ya kwanza ya kutatua tatizo husika, mara nyingi watu wengi huzunguka tatizo husika kwa kujitia upofu wa kutoliona kuwa ni tatizo.

Hapo ndipo mizizi ya tatizo hilo hukomaa na hii ni kwa sababu waliamini kukaa kwenye giza kipindi cha matatizo.

Njia bora na ya kwanza ya kutatua tatizo ni kujua tatizo kabla hujaanza kutafuta tiba sahihi ya tatizo husika.

Kuzunguka tatizo siyo njia sahihi ya kutatua tatizo, ndiyo maana huwa siamini kupitia mtu imara kwa kupuuza ujenzi wa taasisi imara. Wengi wetu hatuoni kumtegemea mtu ni tatizo na kwa sababu hatupendi kujitegemea.

Tuko radhi kuamini Yanga inaweza kuishi maisha bora kwa kumtegemea mtu na siyo kumtegemea. Akili zetu zimepata ukilema wa kufikiria.

Ukilema ambao hata makocha wetu wa ndani wanao, hawafikirii katika kujiimarisha wao katika soko hili la ushindani.

Watatumia muda mrefu sana kulalamika kuwa hawatendewi haki kwa kutoajiriwa na vilabu vyetu bila kufikiria kwanini hawaajiriwi na timu zetu.

Kuna kipindi Mziray aliwahi kuzifundisha Simba na Yanga kwa mafanikio, na hii ni kwa sababu aliamini kupitia kujitengeneza yeye imara ili aongoze timu imara.

Hakuona dhambi kujifunza kitu kipya kinachohusu mpira. Leo hii tupo katika mapinduzi ya mpira, mpira uliojaa mbinu nyingi kuliko kutegemea vipaji binafsi vya wachezaji.

Lakini mbinu za makocha wetu wazawa haziendani na mapinduzi haya mapya ya sayansi ya mpira duniani.

Hakuna anayewekeza muda wake mwingi kufikiria kwenye mifumo mipya ya kisasa, kuwaanda wachezaji kiufundi na kuwalisha wachezaji mbinu nyingi mpya za kisasa zinazoendana na sayansi ya mpira wa sasa.

Ndipo hapo nafsi zetu zinaposhindwa kujizuia kumsifia Masoud Djuma. Kocha kijana anayeendana na sayansi ya mpira wa kisasa.

Kocha anayeendana na wakati wa maendeleo ya mpira wa miguu, sisi tuko nyuma sana na tumeachwa na vitu vingi sana.

Inawezekana kutokuwa na makocha wengi tena imara katika ufundishaji umesababisha kupata wachezaji ambao siyo imara.

Tuna idadi kubwa ya wachezaji ambao siyo washindani. Wachezaji ambao hawajaandaliwa katika misingi imara. Misingi ambayo itawafanya wawe wachezaji imara ambao wataweza kushindana na wachezaji wa kila kona ya dunia.

Ndiyo maana tunapata hofu kubwa tunaposikia shirikisho la mpira wa miguu (TFF) kuwa limetangaza ongezeko la idadi ya wachezaji wa kigeni ndani ya timu kutoka wachezaji saba mpaka wachezaji kumi.

Tunaumia kusikia hivo na kikubwa tunapata hofu kubwa kwa sababu tunarundo la wachezaji ambao hawajaandaliwà katika misingi ya ushindani tangu wakiwa watoto.

Ndiyo maana tunahisi wao kutopata nafasi ndani ya timu zetu. Na kuna wakati tunatumia maendeleo ya timu yetu ya taiga kudumaa kutasababishwa na ongezeko la wachezaji wa kigeni katika ligi yetu.

Huku ni kuzunguka mbuyu wa tatizo ilihali tunajua mzizi wa tatizo uko wapi. Hakuna anayefikiria kabisa namna ya kukata mizizi ya matatizo yetu.

Tumekuwa tukiimba wimbo wa kuanzisha vituo vya kuibua, kulea na kukuza vipaji lakini wimbo huu umekuwa mtamu sana na maarufu kipindi cha kampeni tu.

Hakuna kitu kikubwa kilichofanyika hapa. Hata ligi ya vijana inaendeshwa tu kwa sababu ionekane ipo. Hata sheria ya kila timu kuwa na timu ya vijana waliochini ya umri wa miaka 20 ipo tu kwenye maandishi mazuri yaliyonakshiwa na wino mzito.

Yataendelea kubaki pale pale kwenye makaratasi hakuna anayefikria kuyahamisha kutoka kwenye makaratasi mpaka kwenye vitendo.

Utapataje wachezaji imara wa kushindana na wachezaji wa kigeni bila kuwa na timu za vijana au vituo vya kuibua vipaji vya vijana?

Tutaacha lini kuogopa wachezaji wa kigeni wakati sisi hatuandai makocha ambao watatusaidia kuibua vipaji vya watoto ambao wataandaliwa kuwa wachezaji imara?

Kuna mazingira yapi mazuri na rafiki kwa wachezaji wastaafu ambayo yatawapa nafasi ya kusomea ukocha kwa msaada wa shirikisho la mpira wa miguu? Kuna ugumu gani wa kuingia makubaliano na nchi zilizoendelea kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ukocha kwa hawa wachezaji wa wazamani?

Nadhani hatujafikria kuviweka katika vitendo vitu vyote tunavyovitamani, ndiyo maana tunalalamika vitu vidogo na kusahau kurudi kwenye misingi imara ya maendeleo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

YANGA  INATUMIA KICHWA KUTEMBEA NA MIGUU KUFIKIRIA

Tanzania Sports

Hivi bado hatujaona pesa kupitia neno “Ali Kiba”?