in , ,

MECHI ZA KIMATAIFA WIKI HII ZIMETUACHA NA DARASA KUBWA SANA

Ukipingana na kauli ya maisha ni kupanda na kushuka basi utakuwa
hujaamua kuishi, maana kwako changamoto utakuwa hujaamua kuzipokea.
Ndiyo maana ushishangae Brazil na Uholanzi wanavyopishana kwenye njia
moja. Mmoja anaelekea kaburini mwingine anatoka kaburini alipofufuka.

Nguvu ya maombi ya mchungaji Titte imefanikisha kwa kiasi kikubwa
kumfufua Brazil, muda huu amekuja na roho nyingine, roho ya mzimu tena
mzimu usiokuwa na huruma na kiumbe chochote kinachokuja mbele yake.

Inawezekana umeshawahi kuwa shabiki mkubwa wa mpira wa Kiholanzi,
mpira ambayo tayari uko njiani kuelekea alipokuwa amelalia Brazil.
Hakuna tumaini jipya ndani ya soka là Uholanzi. Mashine zote za Oxygen
zimeshindwa kumuokoa mgonjwa mahututi, na dunia ndiyo imebaki
ikimwangalia anavyoenda kaburini huku akisubiri mchungaji mwingine
atakayekuwa na nguvu ya maombi ya ufufuo.

Njia zote zimeisha, Academeny ya Ajax muda huu haizalishi bidhaa bora
ambazo kwa kipindi cha nyuma zilikuwa ni ustawi wa soka la Uholanzi.

Kizazi cha kina Robben, Van Persie ukomo wake unaonekana. Ligi yao
haipo tena kwenye ligi za ushindani mkubwa, hata wachezaji wazawa
wanaocheza kwenye ligi yao hawapo katika kiwango cha Ushindani. Upya
ni neno zuri unapolisikia ila uzuri wake hukamilika unapoamua
kulifanya kwa vitendo.

Argentina wanacho cha kujifunza kupitia kwa Uholanzi. Kizazi chao pia
kinaelekea mwisho. Kesho ya Argentina haipo tena kwenye miguu ya Kina
Aguero, Higuain, Messi. Umri wao unaonesha wazi kesho ya Argentina ni
ngumu kama hawa watu wataendelea kutumika kwa kiwango kikubwa.

Messi ni bora, kuna wakati timu inatakiwa kujifunza bila ya mchezaji
bora wao. Kutengeneza timu kumzunguka mchezaji mmoja ni jambo là Kheri
lakini siyo jambo bora. Madhara yake huonekana kipindi ambacho
mchezaji huyo anapokosekana kwenye timu, timu hushindwa kucheza
kitimu.

Sitaki kuzungumzia kiwango cha England dhidi ya Lithuani, unakumbuka
mechi ya England na Germany ? Naam dunia nzima ilitoa mkono wa kheri
kwa Lukas Podolski tena akiwa na miaka 31 pekee, miaka ambayo inampa
fursa kubwa kwake kuendelea kuchezea timu ya taifa. Naamini ana mifupa
migumu, kama mifupa ya Defoe.

Unaweza ukashangaa sana utakaposikia ndiye mchezaji pekee aliyecheza
mechi nyingi za ligi kuu ya England msimu huu, umri wake hamzuii
kufukuzana na kina Sanchez, anapumzi sawa inayotosha kumpa changamoto
Lukaku. Kwake yeye kufunga ndiyo starehe kubwa, mpira ndiyo chakula
chake bora ndiyo maana hatokusikiliza utakapomwambia astafu timu ya
Taifa.

Sudani ya kusini inakuja, hili ni jambo muhimu kuwakumbusha wote walio
katika mbio za pamoja na huyu katili.
Hatua zao zinaweza zikaonekana za kawaida, ila kwangu mimi naziogopa hatua zao.

Wao wameshaanza tayari wamempiga mtu goli 6-0 ,sisi tumekuwa watu wa
kuanza upya kila siku. Hatujui ni ligi tutafika maana kila uchwao
mipango ya kuanza huwa ni mingi kuliko ya kufika.

Mayanga amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupanga kikosi chake bila
kuangalia au kuweka uwiano sawa kati ya wachezaji wa Simba na Yanga.
Hakuwaza kelele ngapi atazisikia kama atapanga wachezaji wengi wa timu
fulani ukilinganisha na wachezaji fulani.

Hiki ndicho tulichokuwa tunakililia muda mrefu lakini kumbe tulikuwa
tunalia kilio bila kujua kipi tulichokuwa tunakililia. Magazeti
yameandika maandiko ya kuigawa timu kwa kutumia siasa zile zile
tulizokuwa tunazikataa siku zote. Mashabiki wametumia mitandao ya
kijamii kuigawa timu kwa siasa hizi hizi mbovu, sielewi ipi haswa
ndoto yetu, wakati mwingine ni vibaya kuota ukiwa umefumbua macho.

Mimi kichwani mwangu kuna swali linaniumiza kichwa sana, hivi ni kipi
wanachojifunza kina Msuva, Mao, Ajib, Kichuya pindi wanapokuwa na
Samatta kwenye kambi ya timu ya Taifa ?

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa
kulipwa kwenye timu ya taifa, na hii ni daraja bora la kuipeleka Taifa
stars mbali baada ya lile la kuwa na ligi bora kutushinda.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ANAYEMNG’ATA SIKIO AJIB ASHIKE NA KIBOKO, BAADA YA MACHWEO NI GIZA.

Tanzania Sports

MAENEO MUHIMU YATAKAYO AMUA MECHI YA EVERTON NA LIVERPOOL