in ,

*MBEYA CITY RUDINI MLIKOTOKA, SINGIDA UNITED WANAWASUBIRI*

Msimu wa kwanza baada ya kupanda ligi kuu ya Tanzania bara, timu ya
soka ya Mbeya City ilikuja na ushindani mkubwa sana.

Ushindani ambao ulileta mapinduzi ndani na nje ya uwanja.

Mapinduzi ambayo yalipelekea kila mkoa kuanza kujivunia na timu za kwao.

Hii ni kwa sababu Mbeya City walifanikiwa kutoa hamasa kubwa hali
iliyofanya watu wa Mbeya kujivunia timu yao.

Ilifanikiwa kuwa timu ambayo ilitoa ushindani mkubwa ndani ya uwanja.

Ilifanikiwa kusimama katikati ya wazee wawili wa mpira Tanzania (
Simba na Yanga).

Iliongoza ligi muda mrefu, watu wengi walitamani ichukue kikombe
lakini ukosefu wa uzoefu uliwanyima nafasi wao kubeba kikombe.

Hii haikuwanyima watu wengi kuipongeza Mbeya City.

Ikafikia hatua timu ikawa na wadhamini , kitu ambacho kilikuwa ni
kigumu kwa timu ambayo siyo kubwa ikipata udhamini.

Mipango na ubunifu wa viongozi wa Mbeya City ulifanikisha timu iwe na
ushawishi ndani na nje ya uwanja.

Hata ambaye alikuwa siyo mzaliwa wa mkoa Mbeya alitamani kuwa shabiki
wa timu ya Mbeya City.

Hii ni kwa sababu watu wengi walitamani kuona ushindani mpya tofauti
na tuliouzoea wa Simba na Yanga.

Kila hatua za kuvutia na zenye mlengo chanya wa maendeleo tulianza
kuziona Mbeya City.

Klabu ilianza kutengeneza bidhaa zenye nembo ya timu, hii ni baada ya
wao kuona imeanza kupata kundi la watu wa kuwaunga mkono.

Kundi ambalo lilikuwa tayari kujivunia kunywa chai kwenye kikombe
chenye nembo ya klabu ya Mbeya City.

Kundi ambalo liliona fahari kutundika kwenye kuta zao za sebule
kalenda ambayo ilikuwa na nembo ya klabu ya Mbeya City.

Wengi walipatwa na mihemko mikubwa ya kuwa wafuasi wa Mbeya City, kwao
ikawa kawaida kukatiza mitaani wakiwa wamevaa jezi ya Mbeya City.

Wadhamini wakaja kwa ajili ya kudhamini jezi za kwenye mechi, na
wengine wakaja kudhamini jezi ya mazoezi.

Hii yote ni kuonesha kuwa wanaunga jitihada za mapinduzi za Mbeya
City, ndiyo maana kukawepo na kikundi maalumu cha kushangilia kila
timu ilipokuwa inaenda kucheza .

Kikundi ambacho kilipata mdhamini wa kuwadhamini.

Mbeya City ikawa timu ya mfano , wengi wakatakiwa kujifunza kupitia wao.

Miaka imepita, vitu vingi vimebadirika sana tofauti na awali.

Mbeya City imekuwa siyo timu ambayo inatoa ushindani wa halo ya juu
tena ndani ya uwanja.

Imekuwa timu ya kupigania kubaki ligi kuu na siyo kupigania kuchukua
kikombe kama awali.

Ni timu ambayo imeanza kusahaulika kwenye masikio ya watu wengi .

Hakuna anayeiwaza tena Mbeya City kama timu ambayo inaweza kutoa
ushindani mkubwa katika kuchukua kombe la ligi kuu.

Imeshakuwa timu ya kawaida na siyo timu tishio kama ilivyokuwa awali.

Kibaya zaidi imewaangusha wengi waliokuwa wanatamani kuona ligi yenye
ushindani , yenye timu nyingi za ushindani.

Imepotea kipindi ambacho Singida United inaibuka, timu ambayo
inaonekana ina mipango mizuri kama ilivyokuwa kwa Mbeya City.

Singida United imefanikiwa kupata wadhamini wengi ambao wanasaidia
kuiendesha timu ipasavyo.

Singida United imefanikiwa kuonesha kuwa ina uwezo mkubwa wa
kushindana ndani ya uwanja.

Hiki ndicho kitu ambacho kila mtu anakitamani kwa sababu wengi
wanatamani kuona ongezeko la timu nyingi za ushindani.

Timu ambazo zitaweza kutikisa utawala wa Simba na Yanga kwenye mpira.

Ongezeko la timu nyingi imara kwenye ligi, timu ambazo hazina njaa,
linatoa mwanya wa kupata bingwa imara ambaye ana uwezo wa kuiwakilisha
vyema nchi yetu.

Ongezeko la timu imara na bora inafanya ligi yetu iwe bora na imara.

Kitu ambacho kinaweza kikawa na msaada mkubwa wa kupata timu ya taifa
iliyo bora.

Lakini tatizo linakuja kwa hizi timu zinazoibuka kwa kishindo na
kushindwa kuwa na mwendelezo mzuri wa ushindani.

Natamani kipindi hiki Mbeya City iwe bora kama ya ile Mbeya City ya
Juma Mwambusi.

Lakini cha kusikitisha ni kuwa timu hii ni ya kawaida kwa sasa,
natamani sana ilirudi ilipokuwepo awali.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

REFA ALIIVUNJA NGUVU ARSENAL, MOURINHO ALIJIMALIZA MWENYEWE.

Tanzania Sports

MOHAMMED IBRAHIM, KIVULI CHA HARUNA KINAKUZIBA, TOKEA MLANGO WALIOTUMIA KINA TAMBWE NA AJIB