in

Mbappe kuwa nyota au kumezwa na kivuli cha Neymar?

Kylian Mbappe

Kylian Mbappe ni nyota wa Ligi Kuu Ufaransa, hilo halina ubishi. Kwa wiki nzima amekuwa wimbo uliotawala midomoni mwa mashabiki. Amateawala ulimwengu wa soka. Ametawala vyombo vya habari.

Kifupi amekuwa gumzo kwa sababu ya kuwatandika Barcelona mabao 3 peke yake maarufu kama Hat Trick kwenye dimba la Camp Nou. Akiwa katika uwanja huo alidhihirisha kuwa ni mchezaji wa daraja la juu kabisa na yuko tayari kuongoza utawala mpya kwenda kandanda licha ya kuwa na umri mdogo wa miaka 22.

Mbappe anaelekea kubeba utawala huo ambao ulikuwa chini ya mastaa wawili Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Nyota hao wawili wamekuwa wakipokezana kutwaa tuzo za uchezaji bora wa Ulaya na FIFA, lakini zama zao zimefika ukingoni hivyo kuhitaji wachezaji wapya ambao wataibuka kuendeleza burudani za soka.

Mbappe akiwa na miaka 22 tu aemeonesha kuwa anaweza kubeba timu miguuni mwake na kuipa matokeo mazuri. Katika mcehzo huo PSG walionekana kuziba kabisa mapengo ya nyota wawili Neymar Junior raia wa Brazil na Angel Di Maria raia wa Argentina. Neymar alikosekana katika mchezo huo sababu ya majeraha sawa na Di Maria.

Tanzania Sports
Kylian Mbappe

Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Mbappe kwenye dimba la Camp Nou, na mchezo wa pili dhidi ya gwiji wa kandanda Lionel Messi. Kwa mara nyingine Mbappe alifanikiwa kumfunika kabisa Messi na kuibuka nyota wa mchezo.

Mabao matatu aliyofunga Mbappe yalikuwa ya kwanza dhidi ya Barcelona katika dimba la Camp Nou tangu Andriy Shevchenko alipopachika mabao kama hayo miaka 23 iliyopita.

Uzito wa majukumu aliyokuwa nayo kwenye mchezo huo hayakuweza kumfanya apoteze mwelekeo licha ya kuwakosa nyota wenzake ambao wamecheza kwa ushirikiano kwa miaka kadhaa sasa. Mbappe aliiongoza PSG kuchukua ushindi mnono katika mchezo wa mtoano dhidi ya miamba ya ulaya kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

Hali ya baadaye Mbappe hadi sasa haifahamiki kwa sababu hajafanya mazungumzo ya mkataba mpya na PSG. Kwa sasa mkataba wake umebakiza miezi 18 tu kukiwa na wasiwasi nyota huyo huenda akawahama miamba hao wa Ufaransa licha ya wao wenyewe kuwa na uhakika kumbakiza Paris.

Kiwango alichokionesha katikati ya wiki kimeleta mjadala mkubwa na Nyemar. Baadhi ya wachambuzi wa soka na wataalamu wa uchumi wanamaini Mbappe ni mchezaji ghali kuliko Neymar. PSG wanajenga tiu yao kumzunguka Mbappe ili awe kila kitu katika klabu hiyo kuliko nyota wawili waliokosekana dimbani Neymar na Angel Di Maria.

Kwa upande mwingine, matokeo ya mchezo huo yanaonesha pia PSG wanaweza kushindana na kuzifunga timu bora barani Ulaya, hivyo kuwa mchezaji muhimu bila kuwepo kwa Neymar.

Wakati Mbappe akiwa kwenye tafakari ya kubaki au kuondoka PSG, anatakiwa kujiuliza iwapo ataendelea kuwa kinara wa PSG ama kuwa mchezaji mshiriki wa timu hiyo.

Mchezaji mshiriki ni yule ambaye anakuwa chini ya nyota mkubwa kama Neymar alivyo pale PSG. Mbappe yuko njia panda ya kuwa nyota wa kutumainiwa zaidi PSG au aendelee kuwa chini ya kivuli cha Neymar?

Kwa mchezo uliopita umeonesha Mbappe amefuzu mtihani wa kuongoza mafanikio ya PSG, kwahiyo anayo njia ya kuchagua kwani tayari ameonesha Camp Nou.

Wakati Neymar Juniptr alipohama Barcelona wengi waliamini kuwa amekimbia kivuli cha Lionel Messi. Kivuli cha Messi ndicho kilichotawala Barcelona hadi sasa, nyota wote wanaokuja hapo wanafunikiwa na kivuli hicho.

Kwa vile Neymar mchezaji wa Kibrazil alijiunga timu hiyo akiwa nyota aliona wazi jinsi anavyofunikwa na Messi. Akawa anacheza kwenye kivuli hicho na mafanikio yao ya safu ya ushambuliaji maarufu kama MSN yaani Messi,Suarez na Neymar imebaki kuwa historia kwa sasa.

Licha ya PSG kumwaga feddha nyingi kumsajili Neymar lakini nyota huyo aliamua kukimbia kivuli cha Messi. Ilikuwa ajabu kuachana na Barcelona ili kujiunga PSG lakini kwa soka la kisasa ambalo waarabu wanaomiliki PSG walikubali kumwaga fedha nyingi basi hakuna lisilowezakana.

Habari za Neymar kukimbia kivuli cha Messi zinajulikana dhahiri, lakini sasa naye kivuli chake kimetawala PSG. Wakati fulani ziliibuka habari baadhi ya wachezaji walilalamika kwa uongozi wa PSG kwamba unampendelea zaidi Neymar kwa kumfanya mfalme wa kila kitu huku wachezaji wengine wakionekana kama wa ziada.

Msimu uliopita ni jambo hilo hilo pia lilizuka kwa Mbappe ambaye aliamua kitamka mbele ya vyombo vya habari akimtaka aliyekuwa kocha wake Thomas Tuchel kumpa majukumu makubwa katika klabu hiyo.

Mbappe alitaka kupewa majukumu zaidi katika safu ya ushambuliaji, inasemekana alitaka kucheza nambari 9 ambayo anaamini anaimudu. Ukweli halisi Mbappe hafai kucheza nambari 9 lakini anafaa kucheza winga wa kulia au kutosho na mshambuliaji wa pili.

Mtindo wake wa kucheza unashahibiana na Karim Benzema alipokuwa akicheza Olympique Lyon ambako alikuwa na kasi wakati akikokota mpira lakini hakuonekana kama nambari 9 kamili.

Miaka yote Benzema amecheza kama mshambuliaji mwenye mtindo wa mchezaji wa nambari 10 ambapo anasaidia majukumu ya viungo washambuliaji. Wakati wa Thomas Tuchel hapakuwa na mafanikio ya kutosha lakini matakwa ya Mbappe yalikuwa wazi kabisa.

Kwenye mchezo dhidi ya Barcelona tumeona kocha wake Maurizio Pochettino akimpanga kama mshambuliaji namba mbili huku namba moja akiwa Mauro Icardi. Hivi ndivyo unavyoweza kumtumia Mbappe.

Lakini je, pamoja na kuonesha uwezo wa kuivusha timu kwenye mechi kubwa ataendelea kubaki chini ya kivuli cha Neymar? Je PSG watakuwa tayari kumuuza nyota huyo?

Je, mwenyewe atakuwa tayari kuhama PSG? Pengine msimu huu ukimalizika tutajua mengi zaidi ni ama aondoke awe staa wa timu ama aendelea kuwa chini ya kivuli cha Neymar.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Benjamin Mkapa Stadium Dar

‘Uenyeji’ wa mashindano ya CAF ni heshima Tanzania

Tanzania Sports

EPL hawataki Ligi ya Mabingwa Ulaya