in

MAUZO YA KLABU EPL:

Zamu ya Burnley

Simulizi za majadiliano ya biashara ya kuuza klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zinaendelea, na baada ya jamaa wa Mashariki ya Kati kukwama kuwanunua Newcastle ya Mike Ashley, leo wanazungumzwa Burnley.

Kulikuwapo vizingiti katika kuwauzia wawekezaji wa Saudia Arabia klabu hiyo ya Newcastle, kutoka kwa washabiki lakini na wadau wazalendo wa soka, kwa madai kwamba, pamoja na mambo mengine, falme hiyo imekuwa ikilinda maharamia wanaovuna mamilioni ya pauni kutoka EPL bila England kufaidi.

Burnley ni klabu ya wagumu kiasi, lakini kwa sasa hawapo vyema kivile, leo hii wakiwa miongoni mwa timu tatu za mkiani kwenye jedwali la msimamo wa EPL. Hawajafunga bao hata moja wakiwa nyumbani na kitu pekee wanachoweza kuonesha ni bao moja tu baada ya mechi tano za msimu huu.

Pamoja na hali yao hiyo ambayo bila shaka wao na wadau wanaamini si ya kudumu, kuna muunganiko wa kampuni kadhaa wanaoshindana kuwanunua na kuwamiliki. Kutoka nchini Marekani kuna kundi la kampuni ya masuala ya fedha ya ALK Capital LLC imeibuka wiki kadhaa zilizopita kuitaka Burnley.

Hii itamaanisha kwamba wanataka kuchuana na wengne wanaoendelea na mazungumzo wakiongozwa na mwanasheria wa masuala ya michezo mwenye makazi yake Cheshire, Chris Farnell fedha ikitiwa na mfanyabiashara mkubwa wa chakula wa Misri, Mohamed El Kashashy. Dili linalodaiwa kuwa mezani ni la kwenye pauni milioni 200.

Farnell amekuwa akifanya kazi na wanamichezo wa kaskazini-magharibi kama Cristiano Ronaldo na Roberto Martínez na kwa muda mrefu amekuwa na tamaa ya kusonga mbele na kumiliki klabu.

Alijaribu kuwanunua Charlton Athletic lakini akawa, kwa muda walau, katika marufuku kutoka kwa EFL kwa sababu za mparaganyiko wa kiufundi, japokuwa alifanikiwa baadaye kuondoa marufuku hiyo dhidi yake baada ya kukata rufaa na Bodi ya Ligi imethibitisha kwamba yupo huru kufanya mazungumzo na klabu nyingine.

Kiutamaduni, Burnley wanachukuliwa kama klabu wanaoendeshwa vyema, wenyewe uwezo wa kuishi ndani ya kiule wanachokipata EPL, kwa maana nyingine hushona vazi lao kuendana na ukubwa wa kitambaa walicho nacho.

Katika kipindi cha miaka minane cha mafanikio chini ya kocha Sean Dyche, wamefanikiwa kuboresha miundombinu yao kwa kiasi cha kuridhisha, japokuwa palikuwapo dalili za mvutano hata kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya Corona vilivyofisha uchumi wa klabu kubwa na ndogo.

Kocha huyo alikuwa akilalamikia kuwekwa katika bajeti iliyominywa sana kiasi cha kushindwa kupata wachezaji aliokuwa anataka kuwasajili. Lakini pia ilihusu suala la mishahara ya wachezaji.

Wakati Mwenyekiti Mike Garlick kwa ujumla ameiendesha klabu kwa busara na utulivu, Dyche naye amekuwa mzuri kuwezesha wachezaji wake kufanya vizuri uwanjani, kana kwamba ni kupiga juu ya uzito wao kwa bajeti ndogo.

Kwa vile hawana mfumo wa kibiashara wa nje ya uwanja wa kuweza kuwasaidia kukwepa athari hasi za majanga kama Covid-19, wamekuwa wakitafuta wawekezaji kutoka nje kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Lengo ni kumudu hali ya kutokuwa na watazamaji hivyo kukosa mapato.

Garlick anadhaniwa kwamba anataka kubaki bado katika nafasi fulani ya utawala chini ya wamiliki wapya na angependa klabu ichukuliwe mapema ili Dyche apate fedha kwa ajili ya kufanya usajili kwenye dirisha dogo Januari mwakani. Huenda akawa vyema na kikosi chake kama ilivyokuwa misimu iliyopita japokuwa msimu huu wameanza vibaya.

Kima cha pauni milioni 200 kinahusiana na thamani ya Burnley kama klabu ya EPL, na ni hadhi hiyo iliyokaribisha vita ya watu kuweka madau kuichukua. 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Bernard Morrison

Simba Itaweza Kariakoo ‘Derby’?

Tanzania Sports

Wabongo Hawana Shukrani Kwa Kiduku