in , ,

Manchester yatota kwa Sevilla


*Ni mechi ya kwanza ya Moyes Old Trafford

Manchester United imeambulia kipigo cha mbwa mwizi katika mechi ya kwanza nyumbani kwa kocha mpya, David Moyes.
Washabiki hawakuamini kushuhudia gharika Old Trafford, lililomiminwa na vijana wa Sevilla waliojipanga vilivyo dimbani.
Sevilla wanaotoka Hispania, waliwaangushia Mashetani Wekundu kichapo cha mabao 3-1, katika mechi iliyokuwa pia kwa heshima ya utumishi wa muda mrefu wa Rio Ferdinand Man U.
Kipondo hicho kinakuja licha ya kwamba Sevilla kucheza mfululizo siku mbili, wakitoka kupata ushindi mnono kwenye hatua za kuzu Ligi ya Europa, kwa jumla ya mabao 9-1 dhidi ya klabu ya Mladost Podgorica.
Muda wote wa mchezo dhidi ya United, Wahispania hao walionekana wakali katika ushambuliaji, ambapo hadi mapumziko walishapiga bao mbili, kupitia kwa Vitolo na Marko Marin, aliye kwa mkopo kutoka Chelsea.
Moyes alionekana kuwazindua vijana wake baada ya nusu ya kwanza, wakachomoa bao kupitia kwa Antonio Valencia, lakini Sevilla waligoma kuruhusu jingine, bali wakawatia aibu Mashetani hao kwa Bryan Rabello kupachika bao la tatu.
Ferdinand alitwishwa jukumu la ulinzi, ambapo alijaribu kumdhibiti Marin aliyeonekana kuwa hatari mno tangu mwanzo.
Sevilla waliwaacha tumbo joto Manchester United, hasa kwa jinsi Marin na Diego Perotti walivyotamba eneo la kiungo kadiri dakika zilivyozidi kwenda.
Sevilla walilalamika kunyimwa penati pale Carlos Bacca alipochezewa rafu na Shinji Kagawa, lakini wakajibiwa muda mfupi baadaye, pale Vitolo alipofungua kitabu cha mabao kwa kutelezesha mpira chini ya David de Gea, baada ya kutengewa na Perotti.
Hazikupita dakika nne, kwani zilipofika tatu mchezaji Bacca alimpa pande Vitolo ambaye hakuwa mchoyo, akammiminia majalo Marin aliyeupiga kipembeni na kujaa kwenye wavu ambao ni kana kwamba haukuwa na mlinzi.
United walianza kukimbia hovyo uwanjani na kushindwa kuumiliki mpira, ambapo nusura Marin tena aandike bao la tatu kabla ya mapunziko, lakini shuti lake lilikwenda nje.
Kagawa alishindwa kufunga akiwa na kipa Beto, ambapo alimlenga, naye akaokoa na baada ya hapo De Gea aliokoa shuti la Marin lililogonga mtambaa wa panya na kwenda nje. Bacca naye aliwakosesha Sevilla bao la wazi kwa kupiga juu, ikawa ahueni kwa United pale nusu ya kwanza ilipomalizika.
Moyes ‘alitangaza’ hali ya hatari kwa kuwaingiza
Ryan Giggs, Michael Carrick, Wilfried Zaha na Jesse Lingard ili wamnusuru na fedheha, lakini alikuwa mchezaji wa Man U, Januzaj aliyehangaika na kumpasia mfungaji wa bao la kufutia machozi, Valencia.
Zaha alijaribu kufurukuta lakini hakuweza kufunga bao, na licha ya mihangaiko uwanjani, alikuwa Rabello wa Sevilla aliyekomelea msumari kwenye jeneza la United kwa bao safi la tatu kutokana na pasi safi ya Kevin Gameiro.
Man U wanatakiwa kujipanga sawa kuondokana na mfadhaiko huu, ambapo Moyes atakuwa anahisi shinikizo dhidi yake watakapokutana na Wigan kwenye mechi ya Ngao ya Jamii Jumapili.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal, Fenerbahce kujichuja

Arsenal wawanyuka Manchester City