in , , ,

Manchester United: Kelele za nini?


*Moyes angemnasa Fabregas kimya kimya
*Mbinu za Fergie zinapotea Old Trafford

Manchester United wanahaha kuonyesha kwamba David Moyes ni mahiri anayeweza kunasa wachezaji nyota kwenye usajili huu.
Lakini mtindo walioanza nao unaelekea kuwapeleka pabaya, kama si kuwapoteza kabisa, japokuwa ikiwa bahati, hatimaye wataweza kusajili.
Desemba 2008 aliyekuwa kocha hapo Old Trafford, Sir Alex Ferguson alitoa kauli maarufu kwamba hangekaa awauzie Real Madrid kirusi.
Ni bahati mbaya kwamba hadi sasa historia haijatuambia iwapo aliwauzia kirusi au la – isipokuwa miezi sita baadaye aliwauzia mchezaji wake bora zaidi, Cristiano Ronaldo, kwa pauni milioni 80!
Lilikuwa ni dili ambalo Ronaldo mwenyewe alisita na kulisubiri kwa muda mrefu, na ambalo Man U walijaribu kwa kila hali kulizuia au kulichelewesha.
Ukweli usiofutika ni kwamba, kocha Fergie na Mtendaji Mkuu David Gill walikuwa wakisuka mipango yao kimya kimya nyuma ya pazia na kuhakikisha wanakamua hadi senti ya mwisho waliyoweza katika dili husika.
Hayo yalikuwa enzi hizo, ambapo kabla dili halijatimia, Fergie hangesema chochote, na si ajabu akawapumbaza wanahabari, ambapo akisea hawangesajili tena, ilikuja kumaanisha kwamba wangesajili na vinginevyo.
Sivyo mambo yanavyofanywa sasa, au kuelekea kuchongwa na kocha mpya, David Moyes na Naibu Mtendaji Mkuu, Ed Woodward, na matokeo ya awali hayawatii moyo hata wadau wa United.
Wanachofanya wawili hao ni kujaribu kunasa saini ya nyota wa kimataifa, wakiongeza dau kila uchao, na vyombo vya habari vinajulishwa kila hatua iliyofikiwa.
Matokeo yake, washabiki wamewekwa roho juu kwa muda mrefu kusubiri mipango itimie, badala yake wanadhihakiwa na klabu zenye nyota hao, kama hili la Cesc Fabregas wa Barcelona, ikianziwa kwenye tweet ya mwandishi, na kuthibitishwa hadharani na Moyes kwamba wanamchukua.
Hata suala la Wayne Rooney kwenda Chelsea, ambako ilidaiwa angebadilishwa kwa ama Juan Mata au David Luiz, linadaiwa kuvuja kutoka Australia, United walikokuwa wakicheza.
Lazima kuna washabiki wachache wanaoruka ruka kutokana na kutokezea kwa taarifa hizi, lakini lazima kutakuwa na simanzi mahali fulani.
Leo Moyes anasema waziwazi kwamba Rooney haendi popote, baada ya muda anasisitiza atabaki na hatapata namba kabla ya Robin Van Persie na kwamba kamwe hauzwi. Rooney anataka kuondoka.
Hivi kweli United wanaweza kusonga mbele vizuri kiusajili namna hii? Ukitaka kumvuruga mchezaji, si lazima ufanye hivyo hadharani. Unaweza kufanya hivyo ukishakuwa na uhakika wa dili lako, vinginevyo songa mbele kimya kimya ukitundika rada zako kwa uhakika.
Tatizo liko hapa; United wanatupa fedha nyingi mno kwa ajili ya kumnasa Fabregas, ambaye nyumbani kwake ni hapo hapo Camp Nou, na amerejea hapo miaka miwili iliyopita tu, na anasema hataki kuondoka kurejea England.
Inajulikana kwamba viungo wakongwe wa kati wanakaribia kuondoka Camp Nou, wana kocha mpya anayetakiwa kutiwa moyo, sasa ataondokaje?
Hali hii inaacha uwezekano wa jawabu moja tu; msafara wa kocha, mtendaji mkuu, washabiki na umma wanaomfukuzia mchezaji mmoja maarufu anayeitwa Fabregas kufikia ukingoni kwa aibu kubwa!
Je, itakuwaje United watakapojaribu tena kununua wachezaji wa kaliba ya Fabregas? Ni wazi wachezaji watakaotakiwa watarejea kwenye sakata hili na kujiuliza iwapo Man U ni klabu sahihi kwao na Moyes kocha anayewafaa, na jibu linaweza kuwa ‘hapana’.
Kama Manchester United wamedhamiria lazima wasajili mchezaji wa aina yake, basi kuna kiungo mzuri asiye na tatizo, tena atapatikana kwa bei ndogo zaidi.
Yawezekana Fabregas wala hafurahii Hispania kama England na angeweza kuhama Barca wakimruhusu, lakini Moyes aelewe umma utakachofurahia ni kuwasili kwake Old Trafford wala si hizi blah blah za safari ndefu na mchakato unaofanywa jichoni mwa umma.
Hata hivyo, United wanakosa utu na maadili, kumng’ang’ania mchezaji na kuisumbua klabu iliyopoteza kocha aliyelazimika kuachia ngazi kwenda kupambana na maradhi ya saratani!
Bado Barca walikuwa wakijiweka sawa kupata kocha mwingine kuchukua nafasi ya mgonjwa, wamempata sawa, lakini muda wote huo United wameendelea kusukuma dau moja baada ya jingine, pasipo kujali majonzi yaliyopo pale Camp Nou. Ni sawa na kupeleka posa na kutaka harusi wakati baba mkwe yu taabani hospitalini.
Labda Moyes anachanganywa na ukubwa wa kitita cha pauni milioni 100 wanachojgamba United kuwa nacho kwa ajili ya usajili, maana Moyes alizoea kiasi kidogo sana kule Everton.
Hata hivyo, haijulikani kama kweli amepewa kiasi hicho, maana mtangulizi wake, Fergie, tangu kuondoka Ronaldo ametumia pauni milioni 150 tu kwa miaka minne na Ronaldo aliwaingizia karibu nusu ya hiyo!
Wanachohitaji Manchester ni wachezaji wawili au watatu tu nyota ili kukifikisha kikosi katika hatua ya juu zaidi, lakini mbinu anazotumia Moyes na mwenzake zinatia shaka ya kuwanasa.
Mskochi huyu, kama Fergie, alianza vizuri alipoingia Old Trafford kwa kuwachukua Phil Neville na Ryan Giggs kwenye benchi lake la ufundi, akawa mkali juu ya Rooney, lakini tangu hapo hasomeki vyema.
Angeweza pia kurudi Everton, awachukue Marouane Fellaini na Leighton Baines, ambapo angekuwa amejihakikishia kikosi imara kinachoweza kutetea taji. Badala yake anataka nyota, na hayo yamemfikisha hapa.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Bado tuna ushamba kwenye soka!

‘£9bn zilitumiwa vyema Olimpiki’