in , , ,

MANCHESTER UNITED ILITUONESHA UDHAIFU WA ARSENAL

Jana kulikuwa na mechi nzuri na kubwa sana katika ligi kuu ya England, mechi ambayo iliwakutanisha Arsenal na Manchester United.

Arsenal waliingia kwenye mechi hii wakiwa wana mechi zaidi ya kumi bila kupoteza katika uwanja wao wa nyumbani.

*Kipi kilisababisha wao kupoteza nyumbani?*

Manchester United walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye mbinu yao ambayo waliingia nayo ya kuanzia kukabia juu.

Uwepo wa Lingard, Martial na Lukaku ulikuwa na msaada mkubwa sana kwa sababu walikuwa wanaanza kukabia juu ( mbele).

Hali ambayo mabeki wa Arsenal iliwagharimu mpaka wakawa wanapoteza umiliki wa mpira kutoka na wao kulazimishwa kufanya makosa baada ya kuanza kukabiwa juu.

Mfano goli la kwanza na la pili , lilitokana na wachezaji wa mbele wa Manchester United kuwalazimisha mabeki wa kati kufanya makosa kutokana na kuwakaba kwa kasi.

Hali ambayo ilisababisha wao kupoteza mipira, walipopoteza mipira, ilikuwa faida kwa Manchester United kuanzisha mashambulizi haraka na kuyatumia vizuri.

Beki ya Arsenal haikuwa imara kwa kiasi kikubwa jana, haikuwa inajipanga vizuri.

Pia hata kwenye mashambulizi ya kushtukiza kwao ilikuwa ngumu kutokukaba kwa umakini, hali ambayo ilisababisha hata goli la tatu kutokana na shambulizi la kushitukiza ambalo mabeki wa Arsenal walishindwa kuwa makini kuzuia.

Ubovu wa beki ya Arsenal ulikuwa uimara wa kikosi cha Manchester United.

Na Manchester United walitumia vizuri madhaifu ya mabeki wa Arsenal kwa kutumia kwa kiasi kikubwa nafasi ambazo walizitengeneza.

Asilimia 80 ya mpira wa jana ulichezewa katika nusu ya timu ya Manchester United.

Hii ilionesha Arsenal kwa kiasi kikubwa walikuwa wanamiliki mpira mbele ya lango la Manchester United.

Ndiyo maana ilifanikiwa kupita mipira 33 iliyolenga goli.

Kitu ambacho kilisababisha wao kutokufanikiwa kupata magoli ni David De Gea.

Huyu ndiye aliyeiweka Manchester United kwenye mchezo muda mrefu na ndiye ambaye alitia ugumu kwenye kikosi cha Arsenal.

Aliokoa michomo 14 ikiwa michomo mingi kuokolea na golikipa katika mchezo mmoja.

De Gea aliwazuia Arsenal kwa kiasi kikubwa, na ndiye ambaye aliifanya mechi iwe ngumu kwa upande wa Arsenal.

Ingizo la Iwobi lilimsaidia Ozil kwa kiasi kikubwa kuwa huru kuichezesha timu.

Iwobi alikuwa anatokea katikati ya uwanja, kitu ambacho kilikuwa na faida kwa sababu moja aliongeza idadi ya watu katika eneo la kati ( Xhaka, Ramsey na Iwobi).

Pili Iwobi ndiye alifanya Kazi ya kuchukua mipira na kuisogeza mbele, ikiwa imemrahisishia Kazi Ozil. Ambaye badala ya kuhusika kukaba zaidi yeye akawa anasubiri mipira kwa ajili ya kuichezesha timu.

Ndiyo maana kwa kiasi kikubwa jana Ozil aling’aa tofauti na anavyokuwa anacheza kwenye mechi kubwa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

DE BRUYNE NDIYE BORA ZAIDI MPAKA SASA

Tanzania Sports

SIKU MBAYA ZAIDI ZINAKUJA ZINEDINE ZIDANE!