in ,

Manchester City wawamwagia sifa mashabiki

WACHEZAJI na Kocha wa Manchester City wamepokea kwa furaha ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) kuwamwagia sifa mashabiki wao kwa jinsi walivyowaunga mkono. Maandamano ya kihistoria yalifanyika mitaani kwa kikosi kizima kupita kikiwa na kombe hilo baada ya kulipigania bila mafanikio kwa miaka 44. Sherehe hizo zilipambwa kwa rangi za bluu na kuhitimishwa kwa salamu kwenye viwanja vilivyopo katikati ya jiji, kikosi cha Man City kikiwa kwenye basi la wazi. Kocha Mkuu wa vijana hao wa Etihad, Roberto Mancini aliuambia umati wa watu: “Tunajivunia wachezaji hawa kwa sababu wamefanya kila kitu kwa ajili yenu.” Nahodha wa City, Vincent Kompany aliongeza: “Ni fahari kubwa kumwona kila mtu hapa, kuwa na kombe hili na sherehe, ni maajabu.”

Maelfu kwa maelfu ya mashabiki walijipanga mitaani wakati kikosi kikipita kwenye gari hilo kuelekea katikati ya jiji kuonyesha kombe lao. Kabla ya msafara huo kuanza, Kocha Mancini na wachezaji wa kikosi cha kwanza walitoa hotuba jukwaani nje ya Ukumbi wa Jiji la Manchester. Mambo yalikuwa tofauti Jumatatu hii, kwa sababu mara nyingi Jiji la Manchester lilizoeleka kupambwa kwa rangi nyekundu – zinazotumiwa na Manchester United, ambao ni majirani na mahasimu wa Manchester City na wamekuwa wakiitana majirani wapiga domo. Mwaka huu Jiji lilibadilika na kuwa bluu ya bahari – kutokana na maelfu ya mitandio waliyokuwa wamejifunga shingoni wadau pamoja na mabango waliyoshangiliwa na kupokewa nayo City. Bosi huyu wa Kitaliano – Mancini – alichukua hatamu za ukocha Etihad mwaka 2009 na kuwezesha timu yake kutwaa Kombe la FA mwaka 2011, lililokuwa kama utangulizi kwa mwali wa Kombe la Ligi Kuu walilotwaa Jumapili jioni. Kama kawaida, akiwa amevaa mtandio wake wa rangi ya bluu na nyeupe, Mancini aliwatania mashabiki wa City akisema: “Kuna baridi! Ni mwezi Mei, lakini kuna baridi!” Kocha huyo alikuwa akirejea masahibu yaliyoikumba timu yake kwenye mchezo wa Jumapili, ambapo hadi kufikia dakika 90 za kawaida za mchezo, Manchester City ilikuwa imeshafungwa na Queen Park Rangers (QPR), huku Manchester United wakiwa wameishinda Sunderland. Hata baada ya Edin Dzeko kusawazisha bao na kuwa 2-2, kazi ilionekana bado kuwa ngumu. Mancini aliyekuwa akionekana kama kuchanganyikiwa, aliwaasa wachezaji wake kuharakisha kwa jinsi muda ulivyokuwa ukiwatupa mkono. “Zilikuwa dakika tano nzuri zaidi na mbaya zaidi katika maisha yetu, ulikuwa wakati wa maajabu tulipofunga lile bao la tatu, lakini kabla ya hapo mambo yalikuwa magumu,” akasema. Nahodha Mbelgiji Kompany, aliyefunga bao pekee na la ushindi kwenye mechi muhimu ya kubadili mwelekeo kati ya City na United Aprili mwaka huu alikuwa na haya ya kusema kuhusu dakika hizo: “Kwa kweli tulijituma sana jana…ni hilo tu! Tulivikwa medali hizi shingoni na kupata kombe.” Golikipa Joe Hart, ambaye amekuwa mchangiaji mkubwa wakati wote wa kampeni ya Manchester City kuutafuta ubingwa, alisherehekea kwa kuzunguka uwanja mzima baada ya kipenga cha mwisho. Dakika za mwisho kwake zilikuwa kujituma zaidi uwanjani, akifikia kusonga mbele kusukuma mashambulizi, ikiwa ni pamoja na kurusha mpira kuhakikisha shinikizo linabaki langoni mwa adui zao. Katika gwaride la ushindi Jumatatu, Hart ambaye pia ni golikipa wa Timu ya Taifa ya England, alirejea alivyokuwa akisema: “Nilikuwa kama mashabiki jana. Sikuwa na cha kufanya kwenye mchezo ule (kwa jinsi mchezo ulivyokuwa wa upande mmoja kwa QPR muda mwingi) nilikuwa na kiti cha upendeleo dimbani. “Hali ilikuwa ngumu na ya kuchanganya (dakika za mwisho) na sikudhani kwamba tungefanikisha, kwa kweli najivunia vijana na kila mmoja hapa. Ni ngumu kuzuia hisia, tazama watu hapa leo. Eneo lile (Etihad) lilikuwa likitetereka Jumapili nami nilitetemeka, unapoteza udhibiti katika hali kama ile. Ilikuwa moja ya siku za aina yake katika maisha yangu, na pengine moja ya siku nzuri zaidi pia. Mshambuliaji wa City, raia wa Argentina, Sergio Aguero ndiye aliyekata mzizi wa fitina kwa kupachika bao la tatu, la ushindi na kuleta ubingwa Etihad. Alifunga baada ya kusogezewa mpira na Mwitaliano mtata Mario Balotelli aliyekuwa ameanguka chini, kisha kuambaa nao kabla ya kumwangalia golikipa na kuutumbukiza kimiani. Huyu anakijua Kiingereza kwa mbali sana, kwa hiyo katka sherehe za Jumatatu alichoweza kufanya ni kutabasamu mbele ya mashabiki na kusema: “Asanteni sana! Nililia kidogo (nilipofunga bao lile)” Mchezaji mwenzake wa City na timu ya taifa ya Argentina, Pablo Zabaleta alionekana kueleza kilicho ndani ya moyo wake akisema: “Nilikuwa na imani kwa asilimia 100 kwa Sergio (Aguero) wakati ule, nilijua angefunga. Najivunia timu hii, nawashukuru sana mashabiki, kwa sababu wana uwezo na wanatisha. Asanteni.” Naye Dzeko aliyesawazisha bao dhidi ya QPR baada ya kuingia kipindi cha pili, anasema kwamba matukio ya Jumapili ni ishara wazi ya mafanikio yake katika soka hadi sasa. “Hiyo ndiyo ilikuwa mechi kali zaidi niliyopata kucheza, na hii ni kwa hakika. Tulishafungwa mabao 2-1 na nilikuwa na dakika 25 kwa hiyo nikajaribu kila nilichoweza kuubadili mchezo. Mwishowe nikafanikiwa, nadhani tunastahili kabisa kuwa mabingwa,” akasema raia huyo wa Bosnia. Ama kwa upande wa mlinzi wa Timu ya Taifa ya England, Joleon Lescott ambaye upigaji wake mpira wa kichwa kwa udhaifu kuelekea langoni mwake uliiwezesha QPR kupata bao la kwanza, Jumatatu alikuwa amekaukiwa sauti. Alichoweza kuuambia umati wa mashabiki ni: “Haijalishi nini kilitokea kwa kichwa kile, tulishinda.” Mchezaji mwingine wa Timu ya Taifa ya England, James Milner, anasema ilikuwa kama shubiri kuutazama mpira ule wakati mambo yakiwaendea mrama. “Kupitia yote hadi kufika mwisho ni maajabu. Hali ilivyokuwa pale kwenye benchi…nilikaribia kuanguka kwenye ngazi kuwaendea vijana dimbani. Zilikuwa dakika 10 za maajabu ya kuhitimisha msimu huu wa aina yake,” akasema mchezaji huyo wa akiba ambaye hakutumika Jumapili. Milner aliahidi kujaribu kuhakikisha kwamba msimu huu wa 2011/12 unakuwa mwanzo tu wa mafanikio endelevu kwa Manchester City. “Tunatumaini kwamba huu ni mwanzo wa mengi. Tulikuja hapa kutwaa kombe hilo na tumefanya hivyo. Tutafurahia siku hizi chache zijazo, lakini kikubwa ni kuhakikisha taji linabaki kwa sisi kushinda tena na tena. Tunacho kikosi na klabu na mashabiki wa kufanya hivyo,” akasema Milner. Ama kwa upande wa mshambuliaji wa pembeni, Adam Johnson, aliwasifu mashabiki wa City kwa jinsi walivyowaunga mkono miezi yote hii. “Kila tulichofanya kimekuwa kwa ajili ya mashabiki. Tulitwaa vikombe vichache katika miaka kadhaa iliyopita. Ni jambo zuri kulipa fadhila kwa mashabiki kwa vikombe, wamesubiri miaka mingi,” akasema Johnson. City ilitwaa taji katika mazingira magumu, ambapo ilikuwa inafungana na United kwa pointi, japokuwa yenyewe ilikuwa na uwiano mzuri wa mabao. Hata hivyo ilikuwa ikikabiliana na QPR iliyokuwa ikipigana isishuke daraja, lakini ni timu ambayo imepata kuadhiri vigogo wa EPL. United kwa upande wake ilikuwa ikicheza na Sunderland ambayo haikuwa na kikubwa cha kupoteza wala kupata zaidi ya heshima tu.

Report

Tottenham Hotspur

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

Loading…

0

Manchester City wawamwagia sifa mashabiki Gwaride lafunika Jiji….

Athletics duo win Olympic qualifier