in , , ,

MAN UNITED v. MAN CITY

 

Vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester City kesho Jumapili watawatembelea Manchester United kwenye mchezo wa mzunguko wa 10 wa EPL utakaopigwa ndani ya dimba la Old Trafford. Timu hizi zinatenganishwa kwa tofauti ya alama moja pekee kwenye msimamo wa EPL hivyo mchezo baina yao hapo kesho utakuwa wa kusisimua kupita kiasi.

Itakumbukwa mara ya mwisho timu hizi zilipokutana Aprili 12 mwaka huu ndani ya Old Trafford United waliweza kutoka kifua mbele baada ya kuwatandika mahasimu wao mabao manne kwa mawili. Kabla ya mchezo huo United walikutana na vipigo vinne mfululizo kila walipocheza na wapinzani wao hao kutoka jijini Manchester.

United bado hawajapoteza mchezo wowote wa EPL kwenye dimba lao la nyumbani Old Trafford msimu huu ambapo wameshinda michezo mitatu dhidi ya Tottenham, Liverpool na Sunderland na kutoa sare mmoja dhidi ya Newcastle United. Pengine hili linampa matumaini ya matokeo mazuri mwalimu Louis van Gaal kuelekea mchezo wa kesho.

Advertisement
Advertisement

Manchester City ambao wamekusanya jumla ya alama 21 mbaka sasa wameshinda michezo mitatu ya EPL dhidi West Bromwich Albion, Everton na Crystal Palace kati ya michezo minne ya ugenini. Mchezo pekee wa ugenini waliopoteza ni dhidi ya Tottenham Hotspurs ambao waliwashushia kipigo kikali cha mabao manne kwa moja. Pengine kipigo hicho walichokipata kwenye dimba la White Hart Lane mwezi mmoja uliopita kinawapa tahadhari kuelekea kwenye dimba la Old Trafford hapo kesho.

Hata hivyo kitakwimu Manchester City ni timu tishio mno kwenye EPL msimu huu. Vinara hao wa EPL ndiyo timu inayoongoza kwa kupachika mabao mengi mbaka sasa ikiwa na jumla ya mabao 24. United wapo nyuma kwenye idadi ya mabao ya kufunga wakiwa wamefunga mabao 15 pekee ambayo ni machache ukilinganisha hata na idadi ya mabao ya Arsenal, West Ham na Leicester City.

Hii inaonyesha kuwa safu ya ushambuliaji ya Manchester United haiyakaribii hata kidogo makali ya safu ya ushambuliaji ya Manchester City. Walinzi wa United watatakiwa kuwa macho dakika zote za mchezo wakipambana kuwadhibiti washambuliaji wa City wasisababishe madhara.

Vilevile takwimu za wastani wa mashuti kwa mchezo mmoja wa EPL zinaonyesha umahiri wa City kwenye swala la ushambuliaji. Wababe hao wa Etihad wanaongoza kwa wastani wa mashuti kwa mchezo mmoja wakiwa na wastani wa mashuti 20 kwa mchezo. Hii ina maana kuwa kesho watapiga takribani mashuti 20 ikiwa watakuwa kwenye ubora wao wa siku zote.

United wao wana wastani wa mashuti 11 pekee kwa mchezo mmoja. Hiki ni kielelezo kingine cha udhaifu wao kwenye upande wa ushambuliaji wanapolinganishwa na mahasimu wao Manchester City.

Kwa upande wa vikosi Manchester United wanao majeruhi watatu ambao ni Ashley Young, Luke Shaw na Patrick McNair ambao hawataweza kupatika kwenye mchezo wa kesho. Hata hivyo City ndio wanaokabiliwa na mapengo ya wachezaji muhimu zaidi wakiwemo Sergio Aguero na David Silva wanaosumbuliwa na majeraha pia. Majeruhi wao wengine ni Fabian Delph na Gael Clichy.

Nyota wa kutazamwa kwa upande wa United hapo kesho ni Anthony Martial ambaye kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo juzi dhidi ya CSKA Moscow alifunga bao lake la tano tangu alipojiunga na Manchester United. Kwa upande wa Manchester City Kevin De Bruyne ndiye nyota anayeng’ara zaidi kwa sasa akiwa amefunga mabao manne na kutengeneza mengine matatu tangu alipojiunga na timu hiyo.

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

LIGI YA EUROPA:

Tanzania Sports

Arsenal kileleni