in

Man U wanakosa nini?

Man U wanakosa nini

*Suluhu na timu kubwa zinaacha maswali*

Manchester United wanaonekana kuwa baridi, japokuwa wameketi nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Wamekosa mabao na ushindi kwenye mechi baina yao na timu kubwa msimu huu, wakionekana kushindwa kutia shinikizo kubwa ili wapate ushindi na kuondoka na alama zote, badala yake wamekuwa wakichezea mpira na kuridhika na suluhu.

Jumamosi hii walikuwa Emirates, wakikabiliana na kikosi cha Arsenal ambacho unaweza kusema hakikuwa na wachezaji wake imara sana kwenye ushambuliaji, kiungo mtengenezaji na mlinzi, lakini hadithi kwa United ikawa ile ile – suluhu na vigogo.

Ukosefu huo wa mabao pengine pia unaonesha ukosefu wa ‘motomoto’ kutokana na kutokuwapo washabiki uwanjani ambao wakati mwingine huleta amsha amsha ya aina yake kuwahanikiza wachezaji wafanye mambo kwa kutikisa nyavu.

Sare tasa dhidi ya Arsenal inafuatia matokeo kama hayo hayo dhidi ya Chelsea, Liverpool na City. Je, kocha Ole Gunnar Solskjaer amekosa mbinu za ushindi? Hajapata kuwafunga Arsenal tangu achukue ukocha zaidi ya mwaka sasa.

Tanzania Sports
Lacazette akiongoza safu ya ushambuliaji dhidi ya Man Utd

Ilikuwa wiki nyingine ya lockdown ya soka kutokana na virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu. Kwa timu kubwa kama hizi zinapokutana, pengine inahitajika kelele kiasi fulani kuwasukuma wachezaji.

Ni Arsenal ambao wanaweza kuwa wamefurahia matokeo ya Jumamosi hii na si Mashetani Wekundu waliokuwa na ‘silaha’ zao zote vitani. Mikel Arteta, kocha wa Arsenal pia atakuwa amefurahia aina ya uchezaji wa wachezaji wake, huku mchezaji bora wa mechi akiwa Emile Smith Rowe aliyecheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, Alexandre Lacazette.

Timu zote zilicheza kwa uangalifu mkubwa na milango ikabaki migumu kwa dakika zote 90. Kwa United, bado swali litabaki wazi, kulikoni? Shida ni nini? Kwa nini kutotia jitihada kubwa zaidi na kushinda mechi dhidi ya Arsenal ambao wamefungwa hovyo hovyo msimu huu na wapo katika eneo la mwisho la nusu ya kwanza ya jedwali la msimamo?

Wachezaji walikimbia huku na kule na kutoka jasho jijini London hapa, lakini sasa ni miezi mitatu iliyoshuhudia Man U wakienda suluhu na vigogo. Naam, ni saa sita za ukosefu wa mabao ukuta kwa ukuta, sawa wanaweza kusema wamekwepa vipigo vya vigogo katika saa hizo lakini wengine watasema wamedondosha alama muhimu ambazo zingewafanya wawe mbali kule juu, hasa baada ya Liverpool na Man City, kwa nyakati tofauti kuteleza, sawa na Chelsea na Tottenham Hotspur.

Tanzania Sports
Bruno Fernandes akijaribu kufanya shambulio mbele ya David Luiz wa Arsenal

Lakini kwa kutazama msimamo wa ligi, unaweza kusema walau United wamekaa nafasi inayoendana na rasilimali kubwa walizo nazo kama klabu. Nafasi ya pili nyuma ya Man City wenye mechi moja mkononi, wakitofautiana kwa alama tatu.

Ni timu inayokumbatia uhafidhina, wanapambana kweli lakini wanakosa ile tamaa ya kupata ‘utukufu’ kwa kuzifunga timu kubwa. Ikiwa United wanataka waanze kushinda mechi hizi muhimu itabidi Solskjaer aone jinsi atakavyowatumia wachezaji wake wenye vipaji kama Fred, McTominay na Pogba pamoja na mtu aliyewabadilisha na kuwa wazuri tangu asajiliwe, Bruno Fernandes.

Kadhalika bado mshambuliaji wao mpya, Edinson Cavani hajakuwa na makali aliyokuwa nayo huko alikotoka, akikosa mabao. Lakini swali pia ni kwamba kulikoni Marcus Rashford aliyewika sana sasa amekuwa butu, akiwa na bao moja tu katika mechi tisa? Anthony Martia bao moja katika mechi 11 na Mason Greenwood ambaye angetegemewa kimataifa naye akiwa nalo moja tu katika mechi 13.

Hawa ni washambuliaji wenye vipaji lakini walicholundika ni ukame wa mabao. Iwe iwavyo, Solskjaer anatakiwa kupongezwa kwa kuunda kikosi imara hasa kwenye ulinzi na kiasi katika kiungo. Amewapandisha kutoka chini walikokuwa wamezamishwa na makocha waliopita – Jose Mourinho, Louis Van Gaal na David Moyes baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Kichuya

Uzembe wa Kichuya ndiyo nyota ya Chikwende

SSC

Simba hawajapata hasara kwenye Simba Super Cup