in

Mambo  ya kuchungwa na Simba jijini Lusaka

SIMBA SC

Timu ya Red Arrows licha ya kufungwa mabao 3-0 na Simba bado si timu ya kubezwa. Lakini ushindi wa mabao 3-0 wa Simba unawapa unafuu na kujiamini zaidi kuwa watasnga mbele katika hatua inayofuata. 

Ushindi huo ni mzuri na umeiweka timu katika mazingira ya kufuzu, hata hivyo uzoefu uliopatikana kwenye michezo ya UD Songo ya Msumbiji na Jwaneng Galaxy ni somo tosha kuwa Simba badala ya kupindua meza kama walivyozoeleka wanaweza kujikuta wakipinduliwa wao. Mitihani hii miwili ya UD Songo na Jwaneng inapaswa kuwa somo la kutosha kwa wachezaji wa Simba ambao asilimia 90 ni wale walikuwepo. 

TANZANIASPORTS katika uchambuzi huu inafanya tathmini juu ya mambo muhimu ambayo Simba wanapaswa kuyachunga katika mechi ya marudiano dhidi ya Red Arrows huko nchini Zambia. 

Mchezo ambao una dalili zote za ugumu ambazo kwa lugha ya kimichezo tunaweza kusema ni mchezo wa kufa mtu, na tayari kocha wao Edward Mutupa alionesha dalili hizo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika mchezo wa kwanza kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Yafuatayo ni mambo ya kuchungwa zaidi.

NIDHAMU YA BERNARD MORRISON

Winga huyu alikuwa mchezaji wa aina yake kwenye mchezo wa kwanza. Aliwafanya wachezaji wa Red Arrows waonekane hawana mbinu za kumdhibiti. Aliwageuza, akawasambaratisha na kuichana chana safu yao ya ulinzi na kupachika mabao mawili. 

Pengine angetumbukiza mkwaju wa penati angeibuka na mabao matatu au maarufu kwa kimombo ‘hat trick’. Hata hivyo Red Arrows sio wajinga kiasi hicho, nina uhakika wamesoma mbinu za nyota huyo na hulka zake awapo uwanjani na namna ya kumdhibiti. 

Hatua ya kwanza ambao nina uhakika ifanywa na Red Arrows ni kumchokoza Morrison ili apandwe na hasira. Tukio la kunyimwa penati katika mchezo wa kwanza lilionesha tabia ya Morrison kuwa anaweza kuadhibiwa na waamuzi kirahisi mno japo anawafanya waamuzi wawaadhibu wapinzani wake. Ustahimilivu wake ni mdogo pale anapoona ametendewa ndivyo sivyo. 

Tanzania Sports
Red Arrow

Vilevile Morrison anaweza kukufurahisha kwa dakika tano kisha dakika tano zingine akafanya tukio la ajabu na kuvurunda kabisa mchezo. Benchi la ufundi likiongozwa na Pablo Franco Martin, pamoja na Hitimana Thiery na Seleman Matola wana kazi ya kufanya ili kuhakikisha Morrison anaelekezwa hatari yay eye kugeuzwa ajenda ya Red Arrows na namna ya kukabiliana nayo. 

Simba wakifanikiwa kudhibiti nidhamu ya Bernard Morrison na kuambiwa umuhimu wake katika timu bila shaka ataibuka kuwa mchezaji nyota tena, na kuweza kuwasahaulisha wapenzi na mashabiki wa Simba kuondokewa na Cletous Chama na Luis Miquissone. 

Kila nikimtazama Morrison namwona ndiye nyota wa msimu na ambaye anaweza kubeba majukumu makubwa ya kurahisisha ushindi wa Simba, lakini hayo yatafanyika ikiwa nmchezaji huyo ataweza kutambua na kujidhibiti dhidi ya uchokozi wowote atakaofanyiwa.

NAHODHA MWENYE UCHU

Katika kikosi cha Red Arrows, nahodha wao anaonekana kuwa mchezaji hatari licha ya kucheza beki wa kulia. Ni mtulivu, anausoma mchezo, anawasoma wapinzani, anaelekeza na ushawishi kwa wenzake. 

Kupitia upande wake wa kulia tuliona mara kadhaa akipandisha mashambulizi ya timu yake. ni eneo ambalo Morrison anacheza hivyo ikiwa Simba wanataka kuwashinda Arrows hatua mojawapo ni kumdhibiti beki huyo asimfikie mshambulia wao hatari Chamanga. 

Nahodha huyu anazo sifa kadhaa kama zile za Shomari Kapombe, anakaba, anashambulia, anasumbua na kutawala eneo la upande wa kulia hali ambayo inaweza kumrudisha nyuma mara kwa mara Mohamed Hussein.

LARRY BWALYA ANAWEKWA MBALI

Simba wanaonekana kucheza kwa kumzunguka kiungo mshambuliaji Larry Bwalya. Nyota huyu ana muono mzuri, na mara kadhaa nimemtazama kwenye mechi za kimataifa na ligi ya ndani anacheza kama mfalme ambaye timu nzima ya Simba inatakiwa kupeleka mipira kwake. 

Lakini dosari moja ambayo anayo ni ile hali ya kuchelewesha mipira au kupiga pasi ambazo hazifiki kwa walengwa. Kwenye mchezo wao dhidi ya Red Arrows Jonas Mkude ndiye alionekana kupiga pasi za uhakika katika eneo la kiungo. 

Tunaweza kusingizia mvua iliyonyesha ilisababisha mechi iharibike, lakini hata bila kisingizo hicho Larry Bwalya lazima aambiwe afanye mambo ‘chapuchapu’ kwa sababu maarifa yake ni mazuri na yanatakiwa kuongezewa kasi. 

Mara nyingi anapokuwa na mpira wachezaji wenzake wanakuwa mbali, japo wamefungua nafasi bado hawampi nafasi nzuri ya kuwapatia pasi. Hilo nalo lnamfanya Larry awe anazunguka zunguka na mipira eneo la katikati na hivyo kupoozesha mashambulizi.

MIPIRA YA JUU NA KROSI LANGONI

Eneo hili msimu huu limefanyiwa kazi na makocha wa Simba. Misimu miwili iliyopita Simba walifungwa mabao mengi kwa mpira ya juu na krosi. Sababu kubwa ni moja tu Simba hawakuwa wajanja kwenye kuzuia mashambulizi ya krosi na mipira ya juu. 

Msimu uliopita walifungwa mabao ya namna hiyo pale Afrika kusini na Kaizer Chiefs. Ni mabao yaliyokera na kuudhi kwa sababu mengi yalichangiwa na makosa madogo madogo, lakini yaliwanyima nafasi Simba kwenda nusu fainali. 

Msimu huu tumeona Jwaneng Galaxy wakiimbusha Simba umuhimu wa kuzuia mabao ya krosi wanayofungwa. Ingawa benchi la ufundi linaye beki mrefu kidogo Henock Inonga lakini Pascal Wawa na Joash Onyango wanaonekana kujitahidi bila mafanikio kuzuia mabao ya krosi na mipira ya juu. 

Laiti Simba wangecheza kwa staili ya mtu kam Abadallah Shaibu Ninja wa Yanga wangesafisha mipira ya juu na kukaba tu kwa mtu. Yaani kabla mpokea pasi hajafanya maamuzi beki anakuwa ameshakuja mguuni. 

Uchezaji wa Shaibu una madhara tu kwa kufanya faulo nyingi lakini ni aina ya uzuiaji unaokata mawasiliano mapema au kama asemavyo kocha mkongwe Meja Mingange ni muhimu mabeki kutambua na kuondoa vyanzo vya hatari langoni mwao. 

Bahati mbaya Shaibu pale Yanga anashindana na Bakari Mwamnyeto ambaye anapigana vema mipira ya juu na kuzuia hatari kabla hazijatokea angalau kwa kiwango fulani. 

Simba wanaye Hennock Inonga ninaadhani anaweza kucheza mipira ya juu, lakini watajikuta wakitakiwa kucheza na mabeki wa kati watatu na kuiua nambari 7 ili apewe kiungo mkabaji kati ya Muzamiru Yassing, Tadeo Lwanga na Jonas Mkude. 

MASHAMBULIZI YA KUSHTUKIZA

Benchi la ufundi litakuwa limetazama mechi ya Simba na Jwaneng Galaxy kisha watakubaliana jambo ambalo ni rahisi kuisulubu Simba; mashambulizi ya kushtukiza na kasi ya mchezo. Pablo Franco Martin anajaribu kuichzesha Simba kwa mchezo wa kasi, ikiwa ni njia ya kuwarudisha nyuma wapinzani wao. 

Lakini kwa vyovyote vile makocha wa Red Arrows wataingia uwanjani na akili moja tu kutafuta mabao mapema kwa kushambulia kwa kasi (mfululizo) kadiri wanavyopata nafasi wakijua kuwa si Onyango wala Wawa ambao wataweza mikimbio ya mawinga na viungo wao. Hicho ndicho walichofanya Jwaneng Galaxy kubadili mtindo wa uchezaji sio kuwaiga Simba kwa kutandaza mpira chini.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SSC

Simba katikati ya wababe wa soka Afrika

Tanzania Sports

Refa ameiba matokeo ya Simba na Geita Gold FC