in , ,

MAKALA YA WIKI LA LIGA

 

PENGO LA BUENO LITAIGHARIMU RAYO VALLECANO

 

Imepita mizunguko mitatu kwenye Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) msimu huu ambapo Rayo Vallecano ipo kwenye nafasi ya pili kutoka chini kwenye msimamo wa La Liga. Rayo imefungwa michezo miwili kati ya mitatu iliyocheza mbaka sasa na kutoa sare moja.

Timu hii iliyo chini ya kocha Paco Jemez imesharuhusu jumla ya mabao sita na kufunga bao moja tu. Kiwango wanachokionyesha kwenye upande wa kulinda si kizuri na hata kwenye swala la kushambulia pia kiwango chao hakiridhishi.

Pengine haishangazi kuwaona wakiwa dhaifu kwenye ulinzi kwa sababu wamekuwa hivi kwa misimu yote minne tangu walipopanda daraja mwaka 2011. Msimu uliopita wa La Liga Rayo waliruhusu jumla ya mabao 68 sawa na Cordoba walioburuza mkia kwenye ligi hiyo.

Hata hivyo pamoja na kuruhusu idadi hiyo kubwa ya mabao bado waliweza kumaliza kwenye nafasi ya 11. Hiyo si nafasi mbaya kwa timu kama Rayo ambayo kimsingi ni timu ya malengo ya kati kwa kuwa msimu huu ni wa tano tu  kwa timu hii tangu iliporejea kwenye La Liga baada ya kukosekana kwa miaka nane.

Kumaliza kwenye nafasi ya 11 msimu uliopita kuna maana kuwa ulinzi wao mbovu ulioruhusu mabao 68 haukuwagharimu chochote. Kuna kitu kiliwaokoa. Ni mabao ya aliyekuwa mshambuliaji wao Alberto Bueno ambaye msimu huu ametimkia FC Porto ya Ureno.

Mabao ya mshambuliaji huyo yaliwawezesha kukusanya alama muhimu hata kwenye baadhi ya michezo ambayo Rayo waliruhusu zaidi ya bao moja. Alberto Bueno msimu uliopita aliifungia Rayo Vallecano mabao 17 kwenye michezo 35. Hakuna aliyefikia idadi hiyo ya mabao kati ya Karim Benzema, Luis Suarez na Gareth Bale.

Ingawa kati ya hayo 17 kulikuwa na mabao ya penati lakini bado si idadi ndogo ya mabao unapoifungia timu kama Rayo. Mabao hayo ni takribani asilimia 40 ya mabao yote ambayo Rayo walifunga msimu uliopita.

Kati ya washambuliaji wa Rayo ambao timu hiyo inawategemea kwenye kupachika mabao msimu huu bado hakuna aliyeonyesha kiwango cha kushawishi kuwa atamaliza na angalau mabao 10 msimu huu. Si Bebe, Manucho wala Javi Guerra anayewapa matumaini ya mabao Rayo Vallecano.

Kuendelea kuwa na ulinzi mbovu na kukosekana kwa mshambuliaji anayeweza kufunga mabao ya kutosha kuna maana kuwa Rayo watapoteza alama nyingi msimu huu. Nina mashaka watajikuta kwenye nafasi mbaya mwishoni mwa msimu.

Sina mashaka na mwalimu Paco Jemez kwani kwenye msimu wake wa kwanza akiwa na timu hii, 2012/13 aliiwezesha kumaliza kwenye nafasi ya 8 kwenye La Liga na kuweka rekodi kwa kuwa ilikuwa ni nafasi ya juu zaidi kwenye historia ya klabu hii.

Ulinzi wa kiwango cha chini wa Rayo pia haunipi mashaka kwani ndiyo hali ilivyo kwenye timu hii tangu iliporejea kwenye La Liga. Hata kwenye msimu huo iliyomaliza kwenye nafasi ya 8 iliruhusu mabao 66 na kuwa timu ya tatu kwa idadi kubwa ya mabao ya kufungwa.

Tatizo ni nani atakayeweza kuziba pengo la Alberto Bueno?! Nani atakayeifungia Rayo mabao ya kutosha msimu huu ili isionje madhara ya idadi ya mabao itakayoruhusu kutokana na kuwa na ulinzi mbovu?! Nina mashaka pengo la Alberto Bueno litaigharimu Rayo Vallecano msimu huu.

 

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU BARA

Tanzania Sports

EPL KESHO: MOURINHO v. WENGER