in , , ,

Mabingwa waanza na ushindi

*Zamu ya Mourinho leo

Mabingwa watetezi wa England, Manchester City wameanza kwa ushindi katika mechi yao ngumu dhidi ya Newcastle waliyocheza ugenini St James’s Park.

Iliwachukua City dakika ya 38 kufumania nyavu, pale David Silva alipofanikiwa kufunga baada ya kudokolewa mpira kwa nyuma na Edin Dzeko aliyeanza mechi kisha kumpisha Sergio Aguero dakika saba kabla ya mpira kumalizika.

Alikuwa ni Aguero aliyeshindilia bao la pili katika dakika ya 90, ambapo alitumia makosa ya kipa Tim Krul aliyetema mpira wa awali wa raia huyo wa Argentina, akakwamisha wavuni na kuwaweka City kileleni. Aguero bado hayupo fiti kamili kwa sababu ya maumivu ya hapa na pale.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa vijana wa Manuel Pellegrini kuwafunga hao wa Alan Pardew katika mechi ya kwanza ya msimu. Newcastle walimchezesha Remy Cabella aliyesajiliwa kiangazi hiki kwa pauni milioni 12, na alicheza vizuri.
 
CHELSEA WANAANZA NGWE YAO JUMATATU HII

Jumatatu hii, kocha mwenye tambo nyingi, Jose Mourinho anaingiza kikosi chake kuchuana na Burnley ugenini, ambapo wachezaji wapya wa Chelsea, Cesc Fabregas, Diego Costa na kipa Thibaut Courtois aliyerejea kutoka mkoponi Atletico Madrid wanaweza kuanza.

Burnley wana mchezaji mpya katika Lukas Jutkiewicz anayetarajiwa kushirikiana vyema na Danny Ings mbele kama ilivyokuwa kwa mechi za kabla ya msimu. Kipa wao, Tom Heaton naye yupo vyema baada ya kuwa majeruhi muda uliopita.

Chelsea walikuwa bado wanaangalia iwapo mkongwe waliyemrejesha, Didier Drogba ataweza kucheza baada ya kuwa ameumia goti kwenye mechi ya kirafiki.

Mwaka 2009 Uwanja wa Burnley wa Turf Moor palikuwa pagumu kwa wenyeji kuondoka na ushindi, na inakumbukwa jioni ya Agosti mwaka huo Robbie Blake alifyatua kombora lililowatikisa Manchester United na kuwapatia Burnley ushindi na sifa nyingi.

Baada ya hapo Burnley walipata ushindi dhidi ya Everton pia na waliwabana Arsenal walipokutana nao Desemba walipokwenda sare ya 1-1, lakini walipokwenda Highbury Arsenal waliwakandika Burnley 3-1.

Mourinho ameanza msimu kwa tambo na bezo dhidi ya Arsene Wenger wa Arsenal na Pellegrini, akidai kwamba Arsenal wapo kwenye mtelemko baada ya kutwaa makombe mawili baada ya ukame wa miaka karibu 10, hivyo yeye Mourinho amewekwa kwenye shinikizo japo amemaliza misimu miwili tu bila kombe.

Kadhalika alisema kwamba yeye hajui sana kuchagua timu ya kufundisha, ambapo hupewa timu ngumu na kujenga mwenyewe kila kitu mpaka kupata mafanikio makubwa, tofauti na mtu kama Pellegrini, aliyemfananisha na mtu anayekwenda kuchuma matunda kwenye mti bila kujali aliyehangaika kulima, yaani Roberto Mancini aliyeijenga Man City.

Wenger na Pellegrini wamempuuza tu, ambapo katika siku ya kwanza ya msimu, ni Arsenal pekee waliofanikiwa kushinda wakiwa nyumbani, kwani Jumamosi wenyeji wengine ama walifungwa au kwenda sare, ikiwa ni pamoja na Manchester United waliopigwa 2-1 nyumbani na Swansea

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Liverpool washinda kwa mbinde

Wenger: UCL ni kufa na kupona