Maandilizi ya timu za taifa yanahitaji ubunifu

Michezo ya tisa ya Mataifa ya Afrika inaendelea nchini Algeria huku timu ya Tanzania ikiwa ina matumaini finyu kutokana na matokeo mabovu ya washiriki wake tangu mashindano hayo yaanze.

Kimsingi baadhi ya washabiki wa michezo barani Afrika na nje wamekuwa wakiyabatiza mashindano haya kama `Olimpiki ya Afrika` kutokana na msisimko wake mkubwa.

Nchi nyingi zinazoshiriki kwenye mashindao haya zimekuwa zikijitahidi kuwekeza vya kutosha katika maandalizi ya washiriki wake kwa madhumuni ya kuhakikisha zinafanya vyema katika mashindano hayo.

Mfano wa karibu ni nchi jirani ya Kenya ambayo pamoja na kujiandaa vya kutosha, imeweza kupeleka msafara mzito wa wanamichezo na maafisa wasiopungua 200 huko Algeria!

Huku ikionekana kuwa katika hali kama ya kuchechemea, Tanzania nayo imepeleka washiriki katika michezo ya masumbwi, riadha, judo, mpira wa meza na michezo kwa watu wenye ulemavu.

Kulingana na taarifa ambazo zimepatikana kutoka Algeria, tayari mabondia wa Tanzania wameshindwa katika mapambano yao na hivyo kufungishwa virago mapema, huku tegemeo kubwa pekee sasa likibaki katika riadha na mpira wa meza.

Dalili mbaya za timu hiyo ya Tanzania zilianza kuonekana mapema hata kabla wawakilishi wetu hao hawajaondoka kwenda Algeria kushiriki mashindano hayo yanayoshirikisha nchi zote za Afrika na pia hutumika kuwawezesha wachezaji kupata tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki.
Michezo ya Olimpiki itafanyika mwakani huko Beijing, China.

Kabla ya timu hiyo kuondoka nchini zipo taarifa kwamba kulitokea malumbano makali kati ya vyama vyenye wachezaji waliofikia viwango vya kushiriki michezo hiyo na serikali, ambayo awali iliahidi kupeleka idadi ndogo ya wachezaji katika michezo hiyo ikidai kuwa ina uhaba mkubwa wa fedha!

Ilikuja kubainika kwamba baada ya vyama hivyo kutishia kugomea kupeleka kabisa wachezaji wake katika mashindano hayo, ndipo hatimaye serikali ilikubali kuongeza idadi ya wachezaji watakaokwenda kushiriki katika mashindano hayo.

Hata hivyo, baada ya timu hiyo kwenda Algeria na baadhi yao kufanya vibaya ikiwemo ndondi, viongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) wameibuka na kudai kuwa serikali ilishindwa kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mabondia hao.

Kimsingi tunafahamu kwamba BFT ndio waliostahili kubeba jukumu la kuiandaa timu hiyo kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambayo huzichukua timu hizo mwezi mmoja kabla ya kufanyika kwa mashindano hayo.

Kuna kila sababu ya kuishukuru TOC katika maandalizi mazima ya timu zetu hasa ile ya ndondi ambayo ilisaidiwa kuwekwa kambini hata kabla ya kambi halisi ya TOC ambayo ni mwezi mmoja haijaanza.

Kwa kawaida, chama au shirikisho la mchezo hulazimika kuwa na programu zake endelevu kwa ajili ya maandalizi ya timu zao kabla hazijachukuliwa na TOC na baadaye serikali ili kuhakikisha kwamba timu husika zinasafiri kwenda kushiriki mashindano na siyo kubahatisha au `bora kushiriki`.

Katika misingi hii pamoja na maandalizi ya kiufundi, mambo mengine muhimu kama vile hati za usafiri na maslahi bora ya ujumla kwa msafara mzima yanaandaliwa ipasavyo.

Sasa ni wakati muafaka kwa vyama mbalimbali vya michezo vikaweka pembeni porojo na kuandaa programu zinazotekelezeka kwenye maandalizi ya timu mbalimbali badala ya kukimbilia katika kuwa mabingwa wa kutoa lawama.

Siyo siri kwamba Tanzania hivi sasa ina bahati kubwa ya kuwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ameonyesha dhamira yake ya dhati katika kupania kuipandisha nchi hii kwenye ramani ya michezo duniani.

Ushahidi kamili ni huu ambao amewezesha upatikanaji wa makocha wa timu za soka za taifa ikiwa ni pamoja na ya vijana ambapo hadi sasa zimeweza kufanya yale ambayo kwa miaka mingi Tanzania haikuwa ikitarajia kuyafanya.

Vyama vya michezo vinatakiwa kufanya ubunifu mbalimbali wa kuweza kuwashawishi wafadhili kuchangia michezo hii kama inavyofanyika katika timu za soka.

Kwa asilimia nyingi tunaamini kwamba kuna kila uwezekano wa Tanzania kuepuka aibu na majonzi kama yanayotukuta sasa huko Algeria iwapo viongozi wa michezo mbalimbali watakuwa wabunifu katika maandalizi ya timu zetu.

Comments