in , , ,

LUKAKU HATOSHI, NI LAZIMA POGBA AREJESHE MAKALI YAKE

Romelu Lukaku amekamilisha vipimo vya afya na anakaribia kujiunga na Manchester United kwa ada ya paundi milioni 75. Paundi milioni 15 zaidi zinaweza kuongezeka kwenye ada hiyo kutegemeana na mafanikio atakayopata Old Trafford. Mshambuliaji huyo alikuwa kwenye nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita akiifungia Everton jumla ya mabao 25. Nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Harry Kane wa Tottenham aliyefunga mabao 29 na hivyo kushinda kiatu cha dhahabu.

Ni hatua nzuri na kubwa kwa Manchester United kumpata mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji kwa kuwa atawaongezea makali katika safu ya ushambuliaji hasa inapozingatiwa kuwa aliyekuwa mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita, Zlatan Ibrahimovic hatakuwepo msimu ujao. Ataongeza kitu kikubwa kwenye kikosi cha United ambacho kilikuwa butu mno kwenye kwenye idara ya kufunga mabao. Hata Bournemouth waliomaliza kwenye nafasi ya 9 walifunga mabao mengi zaidi ya vijana hao wa Jose Mourinho waliokamata nafasi ya 6.

Hata hivyo United wanahitaji zaidi ya makali ya Lukaku ili kuleta upinzani kwenye Ligi Kuu ya England na mashindano mengine msimu ujao. Wanahitaji Paul Pogba arejee kwenye ubora wake. Kiungo huyo Mshambuliaji hakuwa na makali yake yaliyotarajiwa msimu uliopita. Alifunga mabao matano pekee na kupiga pasi 4 za mabao kwenye michezo yote 30 aliyocheza. Kwa ujumla alihusika kwenye mabao 9 pekee. Hizi ni takwimu duni na finyu mno kwa mchezaji ghali zaidi kwenye historia ya mpira wa miguu.

Kwa utendaji finyu kiasi hicho kutoka kwa mchezaji muhimu zaidi kwenye kikosi haikuleta mshangao United kumaliza kwenye nafasi ya sita huku wakifunga mabao 54 pekee kwenye msimu mzima wakati Bournemouth walifunga bao 1 zaidi ya idadi hiyo. United walimlenga mno Paul Pogba katika kupika mashambulizi. Alihusika zaidi kwenye pasi za Manchester United kwa kuwa Mourinho anamtegemea zaidi. Aliongoza orodha ya wachezaji waliopiga pasi nyingi ndani ya kikosi cha Manchester United msimu uliopita akipiga pasi 2,178.

Paul Pogba

Kiungo huyo anapolinganishwa na viungo tegemeo wa timu nyingine kadhaa ambazo zilifanya vizuri zaidi msimu uliopita anaonekana duni mno. Kevin De Bruyne wa Manchester City alikuwa kinara wa pasi za mabao akipiga pasi 18 za mabao, idadi ambayo ni zaidi ya mara tatu ya pasi za mabao zilizotolewa na Pogba. Makali hayo ya De Bruyne ambaye alifunga pia na magoli 6 yalichangia kwa kiasi kikubwa Manchester City kufunga jumla ya mabao 80 na kumaliza kwenye nafasi ya 3 wakiwaacha mbali Manchester United.

Tottenham ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England. Walifunga mabao 86 wakimaliza kwenye nafasi ya pili. Kiungo Mashambuliaji tegemeo wa kikosi hicho Christian Eriksen alipika moja kwa moja mabao 15 huku akifunga mengine 8 na hivyo kuhusika kwenye mabao 23. Wakati Pogba ambaye ni mchezaji muhimu zaidi wa kikosi cha United akihusika kwenye mabao 9 pekee haiwi jambo la ajabu Spurs kuwaacha mbali Pogba na wenzie kwenye jedwali la Ligi Kuu ya England.

Kuna viungo wengi wengine muhimu wa timu nyingine waliofanya vizuri zaidi ya Paul Pogba msimu uliopita. Dele Alli, Philippe Coutinho, Cesc Fabregas, Mesut Ozil na Ross Barkley ni baadhi ya viungo hao. Kwa mujibu wa takwimu waliupiku utendaji wa Paul Pogba. Haishangazi timu zao kufunga mabao mengi zaidi ya Manchester United. Washambuliaji wa timu hizo waliweza kuzifungia timu zao mabao ya kutosha kwa kuwa viungo tegemeo walionesha makali ya kutosha.

Itakumbukwa kwenye msimu wake wa mwisho Paul Pogba akiwa Italia aliongoza kwenye kipengele cha pasi za mabao akiwa amepiga pasi 12 za mabao kwenye Ligi Kuu ya Italia. Alifunga na mabao 8 mengine na hivyo kuhusika kwenye mabao 20 yaliyochangia Juventus kutwaa taji. Anakumbukwa pia kwa makali aliyokuwa nayo msimu wa 2014/15 yaliyowapaleka Juventus fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ubora wake msimu huo ulimpelekea kuwemo kwenye vikosi bora vya mwaka vya UEFA na FIFA.

Pogba anapobakia kuwa mchezaji anayetegemewa zaidi uwanjani ni lazima arudi kwenye makali yake ndipo United wataweza kuwa washindani wa kweli kwenye EPL na kwingine. Lukaku ni nyongeza ya maana kwenye kikosi. Hata hivyo pasipo makali ya Paul Pogba hataweza kuwafanya United watwae taji la EPL walilolikosa kwa misimu minne mfululizo sasa. Ibrahimovic alikuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita ambapo alifunga mabao 17. Pogba angekuwa kwenye makali yake yanayofahamika Zlatan angeweza kufunga zaidi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TERRY HAJAACHA PENGO CHELSEA, LAKINI AMEACHA ALAMA ISIYOFUTIKA

Tanzania Sports

KUNA HAJA YA KUJIVUNIA NA COSAFA ?