in , , ,

Liverpool yaimarika, lakini bado makali, yalazimisha sare….

*Reading, QPR zachachiana zenyewe

* Kadi nyekundu zatawala msimu huu

Mapinduzi yanayoendeshwa Liverpool na kocha Brendan Rodgers yanaanza kueleweka, japokuwa bado ushindi umekuwa mgumu.
Liverpool imefikisha mechi tano bila kupoteza, ambao Jumapili hii wametoka sare na Newcastle katika mchezo waliotawala nyumbani Anfield.
Zilikuwa pasi za hapa na pale na mashambulizi ya kushitukiza yaliyowasumbua Newcastle.
Hata hivyo, wageni ndio walitangulia kupata bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kufuatia hekaheka langoni mwa Liverpool na Yohan Cabaye kuonesha maarifa ya umaliziaji.
Mshambuliaji pekee mwandamizi wa Liverpool, Luis Suarez alisawazisha bao kwa ufungaji wa kifundi zaidi, baada ya kupokea mpira na kuwahadaa beki Fabricio Coloccini na golikipa Tim Krul, akatia mpira kwenye kamba na kuuokota mwenyewe kuupeleka katikati ya dimba.
Liverpool walijipanga vyema, lakini walikosa mabao kadhaa, hasa dakika za mwanzo na za mwisho, wakionesha dhahiri kukamia ushindi muhimu.
Newcastle walicheza dakika kama 10 za mwisho wakiwa wachezaji 10, baada ya Coloccini kuoneshwa kadi nyekundu kwa rafu mbaya dhidi ya Suarez ambaye hakuwa na mpira.
Hata hivyo, kocha wa Newcastle, Alan Pardew ameeleza kushangazwa na kadi hiyo nyekundu iliyotolewa moja kwa moja bila onyo la ya njano, na mpira ulipokwisha aliwafuata waamuzi na kuonekana kana kwamba anawauliza kulikoni.
Pamekuwapo malalamiko kwamba Suarez hubaguliwa na waamuzi kwa ama kutopewa penati anapoangushwa kwenye eneo la hatari kwa madai amejirusha au kwa wanaomchezea rafu kutoadhibiwa. Rodgers atakuwa amefurahi kwa mchezaji wake kulindwa jinsi hii.
Rodgers anaendesha kile kinachoitwa mapinduzi mekundu Liverpool, baada ya kuchukua kazi hiyo kutoka kwa mkongwe wa Anfield, Kenny Dalglish. Ameanza kupandikiza umiliki mzuri wa mpira aliofundisha hadi kuwapandisha daraja Swansea City.
Ni Swansea hao hao, hata hivyo, waliomwadhiri wiki iliyopita kwa kuwafunga Liverpool na kuwapokonya kombe la ligi. Rodgers anasema wazi kwamba baada ya Liverpool, timu anayoiombea mema ni Swansea.
Katika mechi nyingine, Queen Park Rangers (QPR) na Reading walio nafasi za 18 na 19 katika msimamo wa ligi, walishindwa kupata ushindi wa kwanza wa msimu.
Walitoka sare ya bao 1-1, wageni wakitangulia kufunga kwa mruko wa kiakrobatiki wa Kaspars Gorkss katika kipindi cha kwanza.
Wakati kocha Brian McDermott wa Reading akiwazia huo ungekuwa ushindi wake wa kwanza, mambo yalibadilika kipindi cha pili, kwa QPR kuongeza mashambulizi.
Vijana hao wa Mark Hughes walifanikiwa kupata bao kupitia kwa Djibril Cisse aliyehaha muda mwingi kutafuta bao. Hiyo ilikuwa baada ya mchezaji wa kimataifa, Esteban Granero kuparaza mwamba wa goli kwa mpira wa adhabu ndogo.
West Bromwich Albion wanacheza na vibonde wa ligi hii, Southampton Jumatatu hii, wakitarajia kujiimarisha kwenye msimamo.
Southampton wanatarajiwa kuwa na mchezaji wao muhimu, Gaston Ramirez, aliyekuwa nje kwa wiki tano kutokana na maumivu ya paja.
West Brom wakishinda wanaweza kupanda hadi nafasi ya nne, kutegemeana na wingi wa mabao watakayopata. Southampton wakishinda hawataweza kuvuka timu nyingine zaidi ya QPR na Reading zilizo jirani mkiani, kwani watafikisha pointi saba.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Abedi Pele awaasa chipukizi wetu

Yanga yashika usukani wa Ligi…