in , ,

LIVERPOOL WANAWEZA KUFANYA MAKUBWA MSIMU HUU

Liverpool wamekuwa timu ya pili ya Ligi Kuu ya England kufikisha mabao 100 ya mashindano yote msimu huu baada ya hapo jana kuwaadhibu West Ham United kwa kipigo cha 4-1 ndani ya dimba la Anfield. Wanayo mabao 103 mbaka sasa nyuma ya Manchester City pekee ambao tayari wamefunga jumla ya mabao 111 kwenye mashindano yote mbaka sasa msimu huu.

Mohamed Salah alikuwa mmoja wa wafungaji akiongeza bao lake la 23 kwenye akaunti yake ya mabao ya Ligi Kuu ya England akiwa sawa na Harry Kane ni la 31 kwenye mashindano yote msimu huu. Mabao mengine ya Liverpool yalifungwa na Emre Can, Roberto Firmino na Sadio Mane huku Michail Antonio akiifungia West Ham ya mwalimu David Moyes bao lao pekee la kufutia machozi.

Ushindi wa jana umewapeleka Liverpool kwenye nafasi ya pili nyuma ya Manchester City wakiwa na alama 57 baada ya michezo 28. Wanasubiri matokeo ya mchezo wa Jumapili kati ya Manchester United na Chelsea kuona iwapo United walio nyuma yao kwa alama 1 wanaweza kupata ushindi wakiwa nyumbani Old Trafford na kurejea kwenye nafasi yao ya pili.

Liverpool ni tishio mno kwa sasa. Wana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao na kuzitumia vyema. Wapo kwenye kiwango kizuri kwenye siku za karibuni wakiwa tayari wameshaingiza mguu mmoja kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuwafunga FC Porto kwa mabao 5-0 wiki iliyopita.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wameweka wavuni mabao 28 kwenye michezo 7 mbaka sasa. Wanaogopesha mno. Idadi hiyo ni karibu mara tatu ya idadi ya mabao ya FC Barcelona kwenye michuano hiyo. Hakuna timu yenye mabao mengi ya Ligi ya Mabingwa kuwazidi vijana wa Jurgen Klopp msimu huu.

Macho ya Jurgen Klopp hayapo kwenye taji la Ligi Kuu ya England. Ni vigumu kuwakamata Manchester City huko. Kuna pengo la alama 15 kati ya Liverpool na vinara hao wa Ligi Kuu ya England ambao wana mchezo mmoja mkononi. Hakuna miujiza inayotosha kuwawezesha kuwakamata Kevin De Bruyne na wenzake.

Mbio zao kwenye michuano ya Carabao Cup zilizimwa mapema mno na Leicester City kwa kipigo cha 2-0 Septemba 19 mwaka jana. Walishaondolewa mapema pia kwenye michuano ya FA Cup tangu Januari 27 walipopokea kipigo cha 3-2 kutoka kwa West Bromwich Alibion.. Klopp amebakisha nafasi moja tu ya kushinda heshima ya mashabiki wa Liverpool msimu huu. Ni nafasi ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa.

Ni kibarua kigumu kilicho mbele ya Jurgen Klopp. Si kazi rahisi kushinda taji hili lenye heshima zaidi duniani kwa ngazi ya klabu. Lakini Liverpool wanacho kinachohitajika kwa ajili ya kushinda taji hili msimu huu. Wanacho kinachoweza kuwafanya washinde michezo migumu dhidi ya timu tishio kama Manchester City, Real Madrid, Bayern Munich, Barcelona na PSG na kutwaa taji hilo.

Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino wanaunda moja kati ya safu hatari zaidi za ushambuliaji kwa sasa duniani. Uwezo wao kuchanganyika vyema wakitengeneza nafasi za mabao na kuzitumia ipasavyo unatoa onyo kwa timu yoyote inayoweza kukutana nao. Kikosi chao ndicho pekee kilichowafunga Manchester City mabao matatu au zaidi kwenye mchezo mmoja msimu huu. Wanastahili heshima.

Jurgen Klopp anayo rekodi ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa mara moja akiwa na Borussia Dortmund msimu wa 2012/13. Aliwaongoza Dortmund kuwaondosha Real Madrid kwenye hatua ya nusu fainali msimu huo na kupoteza mchezo wa fainali kwa 2-1 dhidi ya Bayern Munich. Ana mbinu za maana na uzoefu wa kutosha kumuwezesha Liverpool kuvuka zaidi ya hatua kubwa aliyowahi kuwafikisha Dortmund kwenye Ligi ya Mabingwa. Salah na wenzie wanamuongezea faida.

Liverpool wanaweza kufanya makubwa msimu huu. Wanaweza kufanya makubwa kwenye Ligi ya mabingwa Ulaya kwa kuwa wameshapishana na mataji mengine yote waliyoshiriki. Wanaweza kumaliza kiu yao ya mataji ya misimu mitano kwa namna ya kifahari zaidi.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ZANZIBAR WALIPATA FURAHA CECAFA, AIBU WAMEIPATA CAF

Tanzania Sports

MIKONO YA KABWILI INAPINGANA NA HUKUMU YETU KWAKE