in , , ,

Liverpool ndio wanajua ubaya wa Suarez?


*Kweli soka ni mchezo wa kukumbatia makosa
*Hakuonekana mbaya hadi anapotaka kuondoka

“Klabu hii imekosewa adabu kabisa…nitatoa uamuzi na kuchukua hatua kali, lazima…kazi yangu ni kuipigania na kuilinda klabu…nitahakikisha inaombwa radhi kabla ya kitu kingine chochote kuendelea.”
Hayo ni maneno makali kutoka kwa Kocha Mkuu wa Liverpool, Brendan Rodgers dhidi ya mchezaji wake, Luis Suarez anayepigana kufa na kupona kuondoka kwenye klabu hiyo na kusema klabu inamsaliti.
Je, Liverpool ndio leo wanajua kwamba Suarez hufanya mambo mabaya? Maneno hayo ya Rodgers hayangetakiwa kutolewa Oktoba 2011 Suarez alipoigiza na kumsababisha Jack Rodwell kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mechi ya watani wa jadi wa Merseyside (kadi ambayo iligutwa baadaye)?
Au Desemba 2011, tume huru ya uratibu ya FA ilipomtia Suarez hatiani kwa kumdhalilisha kibaguzi Patrice Evra wa Manchester United na kumfungia kucheza mechi nane.
Kisha Februari iliyofuata Suarez tena alikataa kumpa mkono Evra kabla ya mechi baina ya Liverpool na Man United.
Lakini tunakumbuka pia jinsi alivyofunga bao la mkono dhidi ya timu ndogo Mansfield Town iliyokuwa imeing’ang’ania Liverpool kwenye mechi, na kwa bao hilo Liverpool wakawatoa nje ya michuano ya Kombe la FA Januari mwaka huu.
Mwisho kabisa, labda kocha huyu wa Anfield angetakiwa kutoa maneno makali kama haya wakati Suarez alipomng’ata mkono beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic Aprili mwaka huu.
Sisemi kwamba vitendo nilivyotaja hapo juu vilikuwa vibaya sana (kwanza kufunga kwa mkono dhidi ya Mansfield ilikuwa bahati mbaya, kukataa kumshika mkono Evra si dhambi lakini hakutakiwa kuukataa mkono ule) – lakini yote yameichafua picha ya Liverpool machoni pa dunia.
Makocha wake, kwanza Kenny Dalglish na sasa Rodgers, walikuwa na fursa nyingi za kumwadabisha Suarez kwa kuwafanya Liverpool wadharauliwe, lakini waliamua, kwa kiasi kikubwa, kumuunga mkono mtu wao.
Wameendelea hivyo, na sasa Suarez anapotaka kuondoka kwa nguvu ndio wanajidai kutambua kuwa hufanya mambo mabaya.
Kwa hiyo, kwa mtazamo wangu hii si sawa na wala haina mantiki ya kuangalia mema na mabaya. Rodgers anazungumzia ukubwa wa Liverpool na jinsi ilivyojengwa kwenye msingi wa maadili mema, lakini wamemwacha akafanya vitendo vya utovu wa nidhamu pasipo kumchukulia hatua yoyote.
Kwa hakika, wakati pekee Rodgers kutoa kauli dhidi ya Suarez ni raia huyo wa Uruguay alipokiri kujirusha, ndipo kocha akasema haikubaliki na ni si sahihi.
Rodgers hakusema chochote Suarez alipojirusha kwa kuigiza katika mechi dhidi ya Stoke, akaja kubwatuka pale mchezaji alipothibitisha kwamba aliigiza ili wapate penati.
Nyuma ya pazia, ni vigumu kufikiria na kujiridhisha kwamba Rodgers kweli anachukizwa na yaliyotokea wiki hii, ambapo Suarez amesisitiza kuondoka, akisema klabu ilimwahidi hivyo kama hawangefuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ninavyoona ni kwamba Rodgers sasa hivi anapiga hesabu za jinsi ya kutumia fedha za mauzo yake. Kama alivyosema Hyman Roth katika ‘Godfather II’ pale mwenzake Moe Greene alipopigwa risasi jichoni: “Hii ndiyo kazi tuliyoamua kufanya.”
Soka nayo ni hivyo hivyo, kuna siasa chafu hata kama soka si sawa na mafia, lakini kuna ushindani mkubwa kama ambavyo katika ulaji njama za vitendo vya jinai hakuna anayesikitika kupita kiasi mwenzake anapokufa, kwa sababu ni kazi waliyoichagua.
Katika soka, ni mchuano kati ya timu na timu, lakini pia wachezaji wanatafuta kula, na msimu wa usajili maadili hukiukwa, hivyo hakuna haja ya kushangaa mchezaji anapomgeuka mwajiri wake. Nani hafanyi hayo?
Anachofanya Rodgers ni kucheza na hisia za washabiki wa Liverpool, akiwaonesha kwamba amempa kila kitu, anatakiwa kubaki lakini anakuwa mkaidi, na washabiki wameanza kumchukia Suarez.
Hata hivyo, kumuuza mshambuliaji huyo kwa Arsenal, klabu inayopigania kumaliza ligi katika nne bora badala ya kwenye klabu nyingine kubwa ya Ulaya kunaonesha jinsi Liverpool ilivyoshuka na kushindwa hata kuwania hizo nafasi nne muhimu.
Wapo hatarini kugeuka klabu ya kuzalishia nyingine wachezaji, klabu ambayo kiu yake ya kuwa kigogo inafishwa daima na klabu nyingine kwa kunyakua wachezaji wake nyota.
Inakuwa kidogo sawa na Ajax, tena ni huko huko walimchukua Suarez Januari 2011.
Kwa hiyo sasa, badala ya kumwona Suarez kama mtu anayetaka kukuza kipaji na maisha yake ya soka, anaoneshwa kama mamluki, ambaye akiondoka Liverpool watabaki wamoja zaidi kuliko akibaki.
Labda hofu itakuwa juu ya nani atafunga mabao mengi kama alivyokuwa akifanya Suarez, wakati huo huo washabiki wa Arsenal wanachekelea na kujipa moyo kwamba Suarez si mbaya kihivyo, anawafaa.
Jambo la kushangaza, hata hivyo, ni iwapo mtu wa aina ya Suarez, ambaye hukosa karibu asilimia 25 ya mechi kutokana na nidhamu mbaya na kufungiwa, anaweza kuuzwa kwa £40,000,001.
Ikiwa ndivyo, basi soka ni eneo ambalo linavutia wachezaji wenye uwezo wa kucheza vyema na kufunga na atang’ang’aniwa hata kama ana makosa mengi kiasi gani, naam, makosa yote, lakini la kutaka kuondoka linaonekana kuwa kubwa kuliko yote na lisilovumilika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Liverpool wamtenga Suarez

Arsenal, Fenerbahce kujichuja