in , , ,

Liverpool bado inaishi kwenye matamanio

Miaka 29 sasa, miaka ambayo ni umri wa mtu mzima. Miaka ambayo Liverpool wamekaa bila kubeba kombe la ligi kuu ya England.

Ni miaka mingi sana. Wameishi jangwani kwa muda mrefu bila ya msaada wa kupata maji ya kutoa kiu chao.

Wana kiu sana , lakini tatizo wapo Jangwani sehemu ambayo ni ngumu kupata maji ambayo yanaweza kukata kiu chao.

Hawajakata tamaa , kila mwaka wanapigana wakiwa na imani ipo siku watapata maji katikati ya jangwa, ndiyo maana huwezi kuwasikia wakisema wamekata tamaa.

Neno sahihi kwao kwa kipindi chote cha ndani ya miaka 29 ni kesho lazima iwe yetu. Hili ndilo neno ambalo wamekuwa wakitembea nalo kila uchwao.

Wanaamini hivo, wanahubiri hivo kuwa kesho lazima iwe yao. Ndiyo maana huwezi kuwakuta wamekonda kisa wamekata tamaa.

Wana imani kubwa sana , tena sana. Wanatembea nayo hiyo imani. Wao kila mtu anayekuja katika ardhi ya Anfield huwa wanampa ushirikiano mzuri tu.

Ulimuona Brendan Rodgers ?, kipindi alipokuwa anatokea Southampton kuja Liverpool alionekana kama kocha wa kawaida sana.

Kocha ambaye hana hadhi ya kuifundisha Liverpool, Klabu ambayo inahistoria kubwa ya mafanikio katika ardhi ya England.

Lakini alikabidhiwa timu, na mashabiki wa Liverpool hawakuwa na shaka naye kabisa. Wakampa ushirikiano mkubwa sana bila kujali udogo wake.

Hakuwahi kushinda kombe la ligi kuu ya England lakini wao waliamini kabisa yeye anaweza kuwapa kombe la ligi kuu ya England.

Hii ilikuwa imani kubwa sana tena ya ajabu sana ambayo huwezi kuikuta sehemu nyingine zaidi ya kuikuta Liverpool.

Sehemu ambayo watu walianza kuipenda timu, wakaupenda mpira. Yani kwao wao kila mtu atakayekuja kwao lazima apewe ushirikiano mkubwa sana.

Ndicho kilichotokea kwa Brendan Rodgers ambaye alianza kuwapeleka sehemu ambayo ilionekana kabisa inaweza kuwa sehemu sahihi ambayo walikuwa wanaitamani siku nyingi.

Taratibu aliwaonesha mwanga kuwa anaweza kuwafikisha sehemu ambayo kuna maji kwa ajili ya kukata kiu yao ya miaka 29.

Steven Gerald ndiye aliyeharibu kila kitu , mechi dhidi ya Chelsea ndiyo iliyoharibu matamanio ya Liverpool.

Walishindwa kuyafikia tena matamanio yao. Hawakukata tamaa na waliendelea kuishi kwa kuamini kuwa kesho yao itakuwa bora zaidi kuliko ya jana yao.

Huu ndiyo moyo wa ushindi ambao walikuwa wanatembea nao kila uchwao. Makocha tofauti walikuja baada ya Brendan Rodgers kumaliza safari yake.

Lakini kocha ambaye alikuwa anatazamiwa kuwa na njia sahihi ya kuwapatia maji ni Jurgen Klopp. Mjerumani ambaye alikuja Liverpool kama mshindi.

Alikuja Liverpool akiwa tayari ameshadhibitisha kuwa mshindi kutokana na mafanikio ambayo aliyapata na timu ya Borrusia Dortmund.

Miaka mitatu pekee ndiyo ambayo Jurgen Klopp alitumia kuwaahidi Liverpool kuwa anaweza akajenga timu ya ushindi.

Timu ambayo inaweza kushinda ligi kuu ya England tena baada ya miaka 29. Walimwamini kwa sababu tu historia ilikuwa inamuonesha kama mshindi.

Miaka mitatu ishapita, msimu huu alikuwa anatazamiwa kuibeba Liverpool na kuipa ubingwa. Liverpool msimu huu imeonekana ni timu ambayo inaweza kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya England.

Wamekata kileleni kwa muda mrefu lakini kwa bahati mbaya Jana wameshuka baada ya kupata suluhu na Everton.

Matumaini yameshaanza kupotea taratibu tena. Hii ni kwa sababu wanaweza kuwa na presha kubwa ya kumfukuza Manchester City kwa sasa, kazi ambayo ni ngumu sana.

Wanaweza wakashinda msimu huu, kitu pekee ambacho wanatakiwa kukifanya ni wao kuacha kuishi katika matumaini.

Waache kuishi kuwa ipo siku watabeba kombe la ligi kuu ya England hii inawasababishia wao kutokuwa na hasira za kushinda.

Kwa sababu tu hawaamua kupanga siku sahihi ya kushinda ila wanabaki na matumaini ya kesho kushinda, hivo hata Leo wakikosa hawataumia watabaki kuamini kesho watashinda.

Hiki kitu kinawabomoa sana. Wangeweka malengo ya mwaka Fulani wao kuchukua na kuamua kukimbia kwa nguvu zote.

Ili wafanikiwe kabisa kuchukua kwa mwaka huo, kuliko kukata kila siku wanaishi na matumaini ambayo yanawamaliza wao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ronaldo ameondoka na mvuto wa El Clรกsico

Tanzania Sports

PSG walikitupa kitabu walichopewa na Barcelona