in , , , , ,

LIGI YA MABINGWA ULAYA

Barca waua, Arsenal sare

UTAMU wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) umeanza ambapo Barcelona
wamewatandika bila huruma Celtic, wakiwafyatua mabao saba kwa sifuri
huku Arsenal wakiwa ugenini kwa Paris Saint-Germain (PSG) wameenda
sare ya 1-1.

Lionel Messi alifunga mabao matatu, ikiwa ni hat-trick yake ya sita
kwenye michuano ya UCL katika historia, na Celtic ndicho kipigo chao
kikubwa zaidi kupata, safari hii wakifundishwa na kocha wa zamani wa
Liverpool, Brendan Rodgers.

Celtic walikosa kabisa bahati, kwani licha ya kuzawadiwa penati,
Moussa Dembele alishindwa kufunga, ikiokolewa muda mfupi kabla ya
Messi kupachika bao la pili kwa Barca. Katika kipindi cha pili, mpira
wa adhabu ndogo wa Neymar ulizama moja kwa moja wavuni, Andres Iniesta
akatia la nne, Messi la tano na Luis Suarez akamalizia kazi.

Arsenal kwa upande wao, walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Alexis
Sanchez baada ya PSG kupata bao katika dakika ya kwanza tu ya mchezo,
mfungaji akiwa ni Edinson Cavani. Arsenal walimchezesha kipa namba
mbili, David Ospina, na alifanya vyema kwa kuokoa mabao mengi ya wazi.

Nusura Alex Iwobi awapatie Arsenal bao la ushindi kwenye dakika za
majeruhi lakini haikuwa. Olivier Giroud wa Arsenal na Marco Verratti
wa PSG walipewa kadi nyekundu dakika ya 93 kutokana na mchezo mbaya
uliowahusisha wawili hao.

Ndani ya dakika 27 tu alizocheza akitokea benchi, Giroud alipewa kadi
mbili za njano, ambapo ya pili ilitokana na kumchezea vibaya Verrati
japo Giroud anadai alijiangusha. Arsenal waliteswa na kasi ya Cavani,
Angel di Maria na Serge Aurier ambapo wakati mwingine walimtegemea
zaidi Ospina – na hakuwaangusha.

Arsene Wenger atafurahia pointi hiyo moja, kwani PSG walionekana kuwa
wakali muda mwingi. Walipeana pasi nzuri lakini walionekana
wakitikisika kwenye eneo la ulinzi. Kwenye mechi nyingine ya kundi A,
Basel wa Uswisi nao walikwenda sare ya 1-1 nyumbani kwa Ludogorets
Razgrad wa Bulgaria, hivyo timu zote zimefungana kwa pointi na mabao.

Kwenye mechi nyingine, Bayern Munich waliwakung’uta FC Rostov 5-0,
Benfica wakiwa nyumbani wakaenda sare ya 1-1 na Besiktas, wenyeji
Dynamo Kiev wakalala 1-2 kwa wageni Napoli wakati PSV Eindhoven
walifungwa nyumbani kwa Atletico Madrid.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SUNDERLAND STABILISING TANZANIAN FOOTBALL

Tanzania Sports

Man United hoi Europa