in , , , , , , ,

Kwanini soka tu? Michezo mingine kunani Tanzania?

 *Vyama vya michezo mingine vipewe msaada na umuhimu kama wa soka

 

Inasikitisha sana kwamba Watanzania tumeipa kisogo michezo mingine isiyo soka kwa sababu za kibiashara. Hakuna ubishi soka inalipa kutokana na kupendwa na watu wengi lakini kihabari, unapoandika au kutangaza soka na kupata manufaa kiuchumi,nini kinakuzuia kutumia nafasi iliyobaki au muda uliobaki kuandika au kutangaza kuhusu michezo mingine?
Lawama hii haipaswi kuwa dhidi ya vyombo vya habari vya Tanzania bali dhidi ya wadau wenyewe wa michezo mingine isiyo soka. Hapa leo nitakupa mfano wa michezo miwili tu; netiboli (mpira wa pete) na basketiboli (mpira wa kikapu).
Wakati wa karinyekarinye za mchakato wa uchaguzi wa TFF, watu wa soka wa nchi ya Tanzania walitengeneza habari kubwa kubwa kila siku kuhusu uchukuaji na urudishaji fomu, kuwekwa mapingamizi, uamuzi wa mapingamizi, rufani za mapingamizi na habari nyingine kemkem. Sasa hivi mtu akikuuliza suala la uchaguzi wa Chama cha Netiboli nchini (CHANETA) limefikia wapi, huna jibu kwa sababu CHANETA wenyewe hawana juhudi zozote za kulikupandisha juu suala hilo kihabari.
Mashabiki wa mpira wa wavu wakiwa katika uwanja wa YMCA Dar
Mashabiki wa mpira wa wavu wakiwa katika uwanja wa YMCA Dar
Kama mapingamizi kwenye mchakato wa uchaguzi wa TFF yalivyokuwa habari kubwa, ndivyo kusuasua kwa wadau wa mchezo wa netiboli kuchukua fomu za kugombea uenyekiti, umakamu Mwenyekiti na Uweka Hazina kulivyopaswa kuwa habari kubwa ya mchakato wa uchaguzi wa CHANETA. Hii ya CHANETA haikuwa hivyo kabisa.
Ni habari kubwa mno timu yetu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kuifunga Morocco 3-1 hapa nyumbani lakini kwa mshangao si habari kabisa kwa timu yetu ya taifa ya netiboli iliyoshiriki mwezi Desemba 2012 mashindano ya mataifa sita yanayojulikana kama “Netball Nations Cup” huko Singapore ikipambana na wenyeji Singapore, Malaysia, Sri Lanka, Jamhuri ya Ireland na Namibia kubeba kombe hilo huko ugenini mbele ya miamba hiyo ya mchezo huo!
Kama tulivyowahi kuandika hapa, Tanzania imepanda kwenye msimamo wa mwezi Desemba 2013 wa viwango vya mchezo wanetiboli duniani toka nafasi ya 19 mpaka ya 17 ikiwa ya nne barani Afrika, ikiziruka nchi maarufu kadhaa kwa mchezo huo kama ifuatavyo na nafasi zao kwenye mabano:-  Ireland (29), Singapore (19), Malaysia (24), Switzerland (33), Namibia (26), Zambia (23), Sri Lanka (22) and USA (18). Hii wala haikuwahi kuwa habari popote zaidi ya kwenye mtandao huu wa www.tanzaniasports.com/new
Na wala kwenye msimamo wa Januari 27, 2013 tulipokamata nafasi hiyo hiyo na tukiwa nafasi ile ile ya nne barani Afrika tukizidiwa tu na Malawi (5), Afrika Kusini (6) na Botswana (17) wala hiyo haikuwa habari nchini Tanzania! Kinyume chake, tunachimba sana habari za soka kwa sababu huko kuna biashara ya uhakika kupitia wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wetu walio wengi sana.
Serikali inabidi ivisaidie vyama kuwa na mashindano kama iivyokuwa Bonite Cup
Serikali inabidi ivisaidie vyama kuwa na mashindano kama iivyokuwa Bonite Cup
Tukiutazama mchezo wa basketiboli. Mchezo huu ndiyo unaoongoza kwa kutengeneza mwanamichezo tajiri kuliko wote wa kitanzania. Huyu ni Hasheem Thabeet wa timu ya Oklahoma City Thunder ya moja ya ligi kubwa za basketiboli duniani ya NBA ya Marekani. Kupitia changamoto ya mafanikio ya mchezaji huyo, wadau wa mchezo huo wa Tanzania wangeuinua vya kutosha mchezo huo miongoni mwa vijana wa kizazi hiki. Kinyume chake, kuna mashindano ya taifa ya mchezo huo yamefanyika Tanga hivi karibuni bila msisimko wowote, kiushabiki na kihabari!

 

Kufuatia kudorora kwa sasa kwa michezo mingine nchini ukiondoa soka, ipo haja kwa wadau wa michezo hiyo mingine kuweka suala la kuiinua miongoni mwa watoto wetu na vijana wetu kuwa moja ya mikakati yao ya kuendeleza michezo hiyo. Wenyewe wawe wanahangaika kulazimisha habari zao kuingia kwenye vyombo vya habari. Wasiige soka inayojitangaza yenyewe kwa ukubwa wa upenzi inaopata toka kwa watu.

 

Nashauri kila mdau wa mchezo wowote ule, uliopo  na usiokuwepo nchini lakini wa kimataifa kama Raga (Rugby) iliyo maarufu jirani kabisa hapa Kenya, kuweka mikakati ya nguvu ya kuinua umaarufu wa michezo hiyo nchini kiasi cha kuwajua na kuwashabikia wachezaji wake kama enzi za kina Flaviana Makorongo  na Jane Butinini wa mchezo wa netiboli au Dulla na Mwinuka wa basketiboli.

Bila kufanya hivyo, kuna siku watoto wetu watapita jirani na uwanja wa netiboli au basketiboli na kuuliza ” eti yale yaliyosimamishwa ni manini na yana kazi gani?” wakiuliza kuhusu milingoti ya magoli ya michezo hiyo kama sasa hivi watoto wengi wa kitanzania waliozaliwa miaka ya 2000 kuja miaka hii wasivyojua chochote kuhusu ala za muziki wa dansi.                        

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

CHANETA Kuchaguana Dodoma 20 April 2013

Messi aokoa jahazi Barcelona