in

Kwanini chipukizi wa nje hawaitwi Taifa Stars?

KELVIN JOHN

Wakati Shirikisho la soka Hispania likipambana juu ya kupata nafasi ya kumtumia mchezaji kinda Ansu Fati katika kikosi cha taifa hilo nilikuwa nafuatilia kwa umakini juu ya uamuzi wa serikali ya nchi hiyo. Niliamini Hispania imejaa vipaji vingi si ya kuhangaikia kipaji cha Ansu Fati kwakuwa imezalisha nyota wengi chipukizi na wakongwe. 

Mjadala ulikuwa mkubwa na kila mtaalamu wa mpira wa miguu nchini humo alitaka kuona Ansu Fati anaichezea Hispania. Lilikuwa kama tukio la kitaifa kuhakikisha Ansu Fati anakuwa mchezaji wa Hispania. Awali Fati alitajwa kwenye kikosi cha vijana cha taifa hilo lakini akatakiwa kwenda timu ya wakubwa, inayonolewa na Luis Enrique kwa sasa. 

Kwao kwenda timu ya vijana haikuwa kipaumbele chao bali walitaka achezea timu ya wakubwa. Katika mazingira kama hayo tunafahamu wapo wanaozungumza hadharani na wengine wanazungumza sirini. Wale waliozungumza sirini hatuwajui, na walitaka nini walipokuwa wakiitaka serikali ihakikishe inamkabidhi uraia Ansu. 

Kinda huyo mwenye miaka 17 alitakiwa kuwa raia wa Hispania na kuchezea timu ya taifa ya nchi hiyo. Inafahamika Hispania ina mashabiki wa soka wabaguzi mno, lakini kwenye suala la kipaji wanaonekana kubadilika. 

Wengi wanakumbuka matunda aliyoleta kocha wao mwenye mafanikio Luis Aragones ambaye alimteua kiungo mkabaji Marco Senna kwenye kikosi cha kwanza. Senna alikuwa mhimili wa kikosi cha Aragones na alifanya kazi zote za kihuni na maarifa katikati ya dimba na kuwarahisishia viungo washambuliaji kuzinyanyasa timu pinzani. 

Senna alifanya kazi zote nzuri na chafu alizopewa na kocha wake Aragones ili kuhakikisha anawalinda mabeki wake na kuwawezesha viungo washambuliaji kufanya kazi zao. Hispania ikaibuka bingwa wa Ulaya mwaka 2008. Miaka miwili baadaye yaani mwaka 2010 wakatwaa Kombe la Dunia pale Soccer City Soweto nchini Afrika kusini.

Marco Senna kama Ansu Fati wote ni weusi. Kwahiyo nilipoona Ansu Fati akigombea kati ya Hispania na Guinea hakika lilikuwa jambo la kuchekesha kidogo kinda wa miaka 17 amegeuka lulu ugenini. 

Hata hivyo mwisho wa siku Hispania ilifanikiwa kumpata Ansu Fati kuwa mchezaji wao na bila kupepesa macho kinda huyo alikuwa anajumuishwa kikosi cha wakubwa tu. Kwao Fati alistahili kupangwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa kuliko kile cha vijana. 

Mikakati ya Hispania ilikuwa bayana kuhakikisha wanampata kabla ya kutimiza miaka 18 ambako kwa mujibu wa sheria atakuwa na uamuzi wa kuchagua nchi ya kuchezea timu ya taifa. Kwa sasa Hispania wameula kumnasa kinda huyo.

Serengeti boys
Serengeti boys

Mkasa huu unatukumbusha namna ya kuwatumia vijana wetu kuwajengea mazingira ya kuichezea Tanzania katika soka. naamini Tanzania inao vijana wengi wanaocheza soka la barani Ulaya hata kwenye klabu ndogo, lakini wanapeperusha bendera ya Tanzania. hawa hawajachukua uraia wan chi nyingine. Wapo wengine ambao wamechukua uraia wan chi walizopo wazazi wao hivyo kushindwa kuitumikia Tanzania kwenye soka kwa vile hairuhusu uraia pacha, wala kutoa umaalumu fulani kwa raia wake waliopo nje ya nchi. Hilo nalo la ajabu, na linawezekana serikali ikatengeneza utaratibu wa ‘umaalumu’ wa raia hao kwenye sekta ya michezo. 

Kocha wa Taifa Stars Ettiene Ndayiragije anaopoita wachezaji kujiandaa na mechi hata za kirafiki hatuwaoni makinda wakijumuishwa. Leo hii unaweza kujiulzia yuko wapi Tiba John? Yuko wapi Eliud Ambokile? Kelvin John anayetabiriwa kuwa mrithi wa Mbwana Samatta yuko wapi? Oscar Nkomola yuko wapi? Je, ni kweli vijana hawa hawawezi kuitwa hata kufanya mazoezi na wakubwa ili waandaliwe kuchukua nafasi zao?

Kama nchi za wenzetu zilizofanikiwa kisoka wanawaita wachezaji wao wakiwa na umri wa miaka 17 kuwapa uzoefu inakuwaje vigumu kwetu kuwaita kwenye kikosi cha Taifa Stars ili kuwapa aria na uzoefu? Je hilo haliwezi kuchangia baadhi yao kubadili uraia na kucheza nchi zingine huku tukiwa tunashuhudia bila kuchukua hatua zozote?

Hapo ndipo nawakumbuka Wahispania katika mbio zao za kuhakikisha Ansu Fati anachezea timu yao ya taifa. Hawakujali umri wake wa miaka 17 bali walizingatia faida ambayo taifa ingelipata kwa kumchukua mchezaji huyo. Kipaji chake kinakuja kuleta faida ya taifa, na kwamba hata kama wanategemea huduma ya wachezaji wakongwe. 

Je, kwanini hatumwiti Kelvin John kujumuika na kikosi cha wakubwa, hata akiishia benchi kushuhudia mechi inamsaidia kumudu kuhimili presha, kupata maarifa ya mchezo kuliko kumwacha jukwaani? Ugumu wa kumtumia kijana huyo hata kwenye mechi za kirafiki uko wapi? 

Wenzetu waliofanikiwa wanaamini kuwa mchezaji chipukizi akichukuliwa hata kuwekwa benchi na kushuhudia wakubwa wakiwajibika inaendeleza kipaji chake kuliko kumwacha kabisa. wakati tunasifia vipaji vya chipukizi kutoka Ulaya, ni kwa vipi sisi kama nchi hatuchukui hatua kuhakikisha kuwa wachezaji wetu makinda wanapewa fursa ya kujifunza kwa wakubwa? 

Malengo yetu ni kutaka tuwe na wachezaji wa kulipwa lakini wale walioko kwenye vilabu mbalimbali sehemu tofauti duniani tunashindwaje kuwatumia ili kutangaza nchi yetu? Kuitwa mchezaji wan je ni sifa kwake na klabu yake, hivyo kuiongezea klabu yenyewe thamani kwa wadau wake. 

Sasa kama hatuwatumii chipukizi walioko nje, ni lini tutaweza kuibua mastaa wetu au hadi tusubiri waibuliwe na vilabu vya nje ndio tujigambe? Tujisahihishe.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Taifa Stars

KUFUZU AFCON

Madhara ya mipira ya kichwa

Soka: Punguzeni vichwa