in , ,

Kwa heri Arsene Wenger, tutakukumbuka

*Simulizi ya mahaba inamalizika kwa simanzi kubwa
*Pazia sasa linashushwa la miiaka 22 ya mafanikio

HIVI karibuni niliandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook salaam za
kwa heri, kwa lengo la kumtakia kila la kheri kocha Arsene Wenger
anayeondoka Arsenal baada ya miaka 22.

Mara baada ya kupost, rafiki yangu na nguli wa habari za michezo, Edo Kumwembe alinipa ‘live’ juu ya tabia yangu ya kumtetea Wenger, au AW,
hata pale anapoharibu.

Tulibishana sana na inabaki kuwa ukweli kwamba mie ni mmoja kati ya
watu wachache ambao bado wanaamini AW anastahili kuendelea kuwa kocha
wa Arsenal.

Nakumbuka Kumwembe alinieleza juu ya ukweli kwamba Wenger amekuwa
akifanya vibaya, akiwakosesha raha washabiki lakini nikamtetea tu,
lakini nilimwambia na bado nitasimamia kusema kwamba aliyofanya kwa
klabu ni makubwa sana na ameifikisha pazuri sana, ikiwa klabu kubwa.

Alipoingia Highbury enzi zile 1996 klabu ilikuwa tofauti kabisa na
sasa, kaiendeleza, wakapata makombe na kwenda msimu mmoja mzima bila
kufungwa enzi za ‘The Invicibles’.

Ni kwa sababu yake Uwanja wa Emirates, moja ya viwanja vikubwa na vya
kisasa zaidi nchini hapa, ulijengwa na sasa wamiliki wanafaidi sana
kiuchumi.

Aliacha kusajili majina makubwa ili fedha zielekezwe kwenye ujenzi
huo, na hili aliulizwa mapema na wenye mali ikiwa wasajili au wajenge
uwanja, akasema wajenge uwanja, na ndiyo maana amekuwa akirejewa kama
‘profesa’, wengine wakisema ni mbahili. Ukweli ni kwamba ana shahada
ya uchumi.

Jumapili hii ni siku yake ya mwisho Arsenal kwa maana ya mechi uwanja
wa nyumbani wa Emirates, na ni siku ya washabiki kumuaga.
Simulizi kubwa la mahaba au mapenzi linafika mwisho sasa, pazia la
uwapo wake Arsenal likielekea kushushwa taratibu lakini kama ilivyo
kwa hadithi nyingi za mahaba, huwa haziishi vizur sana.

Baadhi ya kumbukumbu za Arsene Wenger, mechi za hivi sasa hazipo hapa.

Arsenal na Arsene nao si tofauti, anamaliza msimu mwingine tena bila
ubingwa na wala pasipo kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa
sababu wanamaliza nje ya nne bora walikokuwa kwa miongo miwili
mfululizo.

Naam, walikuwa na matarajio ya kupita na kufika kwa njia waliyotumia
Manchester United wa Jose Mourinho mwaka jana – Ligi ya Europa, lakini
wameishia njiani kwa kutibuliwa na Atletico Madrid.

Washika Bunduki wa London walianza vibaya nusu fainali kwa sababu
waliruhusu bao kwenye mechi ya mkondo wa kwanza nyumbani Emirates,
wakienda sare ya 1-1, wakijua kwamba Atletico kwenye dimba la nyumbani
kwao ni wagumu hasa na ni nadra kuruhusu bao.

Na kweli, ‘send-off’ ya Wenger sasa inaenda kwa majonzi kwa sababu
hana kikombe, alitolewa kwenye mashindano ya Kombe la Ligi na Kombe la
FA na kwa Ligi Kuu ya England (EPL) sana sana anaweza kumaliza katika
nafasi ya sita.

Hiyo inamaanisha kwamba msimu ujao wana kibarua kigumu tena cha
Europa, na safari za mbali na mazingira magumu ya kazi kwa maana hali
ya hewa viwanjani kama maeneo ya Urusi, wakiwa na safari ndefu.

Pamoja na mwisho mgumu huu, Wenger amefanya mengi klabuni hapo na hata
makocha wazoefu kama Sie Alex Ferguson anakiri kwamba amefanya
makubwa. Jose Mourinho naye anasema huyu si adui wala hasimu bali
rafiki na mtu mahiri ndiyo maana alikuwa akisigishana naye.

Wakati Fergie akisema kwamba anafurahi kwamba rafiki yake, aliyekuwa
hasimu kabla anastaafu wakati huu, Mourinho anasema atafurahi ikiwa
Wenger naye ana raha na hali yake, lakini akisema angependa bado
asiondoke kwenye soka moja kwa moja.

Wenger mwenyewe anasemaje? Anasema kwamba lazima kujihisi huzuni kubwa
na huwezi kuondoka kwenye klabu ulioyokaa kwa miaka 22 kirahisi au kwa
raha, akisema Arsenal ni klabu aliyoipenda sana.

Klabu inakuwa katika hali tofauti ikiwa wanafuzu kwa UCL au la;
kifedha inalipa sana kufuzu lakini sasa huu ni mwaka wa pili pasipo
kufuzu. Wadhamini na watangazaji maeneo mbalimbali ya dunia hutazama
pia mafanikio ya klabu kabla ya kuingia mikataba na kutoa fedha.

Wenger pia anakuwa na mwisho wa simanzi kwa sababu amewaacha mahasimu
wao wa London Kaskazini – Tottenham Hotspur kuwa juu yao, wakifuzu kwa
UCL na wakiwa na kiwango bora hasa chini ya Mauricio Pochettino na
wakifikiriwa kwamba ndani ya muda si mrefu wanaweza kuwa washindani
wakubwa wa ubingwa wa England.

Watu wa Arsenal sasa wanasubiri kuona mrithi wa Wenger atakuwa nani;
ni Mikel Arteta, Thierry Henry au Patrick Vieira waliokuwa wachezaji
chini ya Wenger au watachukua kocha mzoefu?

Swali hilo haliwezi kupata majibu sasa na Wenger mwenyewe ansaema
hawezi kujua wala hahusiki na kutafuta mrithi wake lakini akiulizwa na
wahusika atatoa maoni yake.

Binafsi nahisi kwamba klabu itashuka pasipo kuwa na Wenger (68) kwa
sababu nimekuwa siku zote nikiamini kwamba ndiye mtu sahihi wa
kuiongoza klabu kwa falsafa zake na msimamo thabiti.

Mazungumzo yangu na Edo Kumwembe.

Nani ataipandisha tena klabu? Tunapomuaga Wenger tutarajie mabadiliko
kwenye sera hivyo kwamba kiasi kikubwa cha fedha kitawekezwa? Kuna
wanaosema kocha mpya atapewa pauni milioni 50 tu kwa ajili ya usajili
kiangazi hiki lakini wengine wanasema kwamba ni pauni milioni 200.

Kama nakumbuka vyema, ni kwamba tangu kiangazi cha 2014 hadi sasa
Wenger ametumia pauni milioni 163 tu, wakati akina Pep Guardiola wa
Manchester City wanatumia hadi milioni 300 kwa msimu mmoja hivi.

Ni kweli kwamba karibuni amevunja rekodi ya klabu lakini bado
hawafikii wale wengine wa aina ya Mourinho na Guardiola. Arsenal
wamewasajili Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang katika
madirisha mawili yaliyopita ya usajili. Hata hivyo, zipo taarifa
kwamba Aubameyang hakuwa chaguo lake bali wakuu wengine walioingia
Emirates karibuni.

Wanahitajika wachezaji wapya bado, ikiwa ni pamoja na beki wa kati
mmoja au wawili na golikipa, ambapo Jan Oblak wa Atletico Madrid
anafikiriwa angekata kiu ya wana Arsenal maana kwa sasa Petr Cech umri
unakwenda na David Ospina ndio hivyo na matokeo ya mechi zao.

Kwa sera ya Arsenal na kipa huyu kuwa na sharti la kutolewa si chini
ya pauni milioni 100, basi anayeweza kufikiriwa ni yule wa Bayern
Leverkusen, Bernd Leno. Wenger anaondoka pia akiwa hajatimiza ndoto
yake ya kumsajili beki wa kati wa West Bromwich Albion, Jonny Evans
aliyekuwa Manchester United zamani.

Wenger alizaliwa Oktoba 22, 1949 na anashikilia rekodi ya kuwa kocha
aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika klabu moja kwa sasa.
Ndiye pia anashikilia rekodi ya kutwaa mataji mengi zaidi katika
Arsenal. Anasifiwa kwa kuleta mapinduzi ya soka England kwa
kubadilisha namna ya mazoezi lakini pia milo.

Born: October 22, 1949 (age 68), Strasbourg, France
Nationality: French
Height: 6′ 3″ (1.91m)
Parents: Alphonse Wenger, Louise Wenger
Children: Léa Wenger

Huyu ni mzaliwa wa Strasbourg aliyekuzwa Duttlenheim na kuingizwa
kwenye soka na baba yake aliyekuwa kocha wa timu kijijini kwao.
Alichezea timu mbalimbali za ridhaa kabla ya kuingia kwenye ukocha,
akapata diploma 1981.

Baada ya kutopata mafanikio akiwa na Nanc alikoondoka 1987, alijiunga
na Monaco na akawapa ubingwa mwaka uliofuata. Mwaka 1991 Wenger
aliwapa tena taji katika Coupe de France, akaondoka huko 1994.
Alifundisha kwa muda mfupi kwenye klabu ya Japan ya Nagoya Grampus
Eight, akawapa mataji ya Kombe la Mfalme – Emperor’s Cup na Japanese
Super Cup.

Ni baada ya hapo aliingia England, wengi wakimshangaa kwa sababu
hakujulikana, ikizingatiwa kwamba wakati huo soka haikuwa ikioneshwa
sana, na Japan hawakuwa maarufu kwenye mchezo huo. Kuna swali maarufu
lililokuwa likiulizwa; ‘Wenger who?’.

Ferguson mwenyewe alikuwa akishangaa, akisema jamaa huyu aliyetoka
Japan atafanya nini, lakini baadaye akasema kumbe ni mtaalamu.
Wakati sasa unawadia, na kwa hakika upo hapa kwa ajili ya kumalizia
simulizi hii ya mahaba inamalizika kwa simanzi.

Mail to: [email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

WACHEZAJI MZIGO YANGA

Tanzania Sports

Yanga ina kikosi chepesi katika michuano migumu