in , , ,

KUFUZU KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA

Mabingwa Zambia wapita kwa mbinde

*Uganda wawabana pumzi hadi penati 20

Mabingwa wa Afrika wamefuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kwa bahati, baada ya kuzidiwa nguvu katika dakika 90 za mchezo.
Uganda ndio waliowafanya Zambia wakeshe wakiomba, baada ya kuwatungua kwa bao moja jijini Kampala.
Hiyo ilikuwa kulipiza kisasi kwa Zambia waliowachapa bao hilo hilo mjini  Ndola, Zambia mwezi uliopita.
Timu ya kufuzu kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika Afrika Kusini hakuweza kupatikana, hata baada ya Zambia na Uganda kupigiana penati tano tano, kwani walikuwa nguvu sawa.
ilibidi mikwaju zaidi ya penati iongezwe hadi mshindi apatikane, ndipo ikabidi mabingwa waende hadi penati ya 10 ili kupata ushindi, na sasa wana kazi kubwa ya kutetea kombe.
Wa Zambia ulikuwa ushindi wa penati 9-8, ambapo Patrick Ochan wa Uganda alikosa penati muhimu, katikati ya kelele za washabiki wa Uganda waliotaka kuona timu yao ikiingia kwenye fainali hizo.
Mechi hiyo ilijenga ushindani wa aina yake uliokaribia na uhasama, ambapo Uganda kwa mara nyingine wamekosa nafasi ya kufuzu kwa asilimia ndogo kabisa.
Kwa mpira ulivyoanza Jumamosi hii jijini Kampala, wakiwa na uungwaji mkono wa maelfu ya washabiki wao, Uganda walionekana kuwa na nafasi nzuri ya ushindi.
Na kweli, katika dakika ya 27 tu mambo yalijipa, kwani Geoffrey Massa aliandika bao la kuongoza, huku Uganda wakiwachezesha Zambia kwata na kuwafanya wahemee juu juu.
Uganda waliendelea kucheza kwa kujituma ili kutafuta bao la pili ambalo lingewahakikishia kufuzu moja kwa moja, lakini kikosi hicho kinachonolewa na Mskochi, Bobby Williamason kilishindwa kuwazidi nguvu mabingwa.
Golikipa wa Zambia, Kennedy Mweene atakumbukwa na Waganda, kwani alizuia nafasi zao za wazi za kuandika mabao, kushinda na kufuzu, kutokana na jinsi alivyocheza kwa ushujaa.
Nyota ilionekana kulalia kwa wenyeji bado, kwani wageni walipoanza kupiga penati, walikosa ya kwanza kupitia kwa nahodha wao, Chris Katongo.
itakumbukwa kwamba, Katongo ndiye alikuwa chachu ya ushindi uliowafanya Zambia kutawazwa mabingwa wa Afrika, hivyo alipewa nafasi ya kwanza akiaminika angefunga, ili awatie nguvu wenzake, lakini haikuwa hivyo.
Hata hivyo, Uganda walishindwa kutumia fursa hiyo kwa uendelevu, nao wakafikia mahali wakashindwa, hadi ilipofika fursa ya Ochan aliyeshindwa kufanya kweli.
Zambia walishinda mechi ya fainali ya kombe hilo mwaka huu kwa mikwaju ya penati dhidi ya Ivory Coast, katika fainali zilizofanyika Libreville, Gabon.
walihamasika kucheza vyema, maana fainali hizo zilifanyika karibu na ufukwe ambao wachezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia walifia kwa ajali ya ndege mwaka 1993.
Uganda ilikosa ushiriki wa fainali zilizopita kwa ncha ya sindano, walipokwama kushinda mechi ya mwisho ya kufuzu iliyofanyika Kampala.
mara ya mwisho kushiriki fainali hizo ni 1978, ambapo walifika hadi fainali, wakaishia kuwa washindi wa pili.
Timu ya taifa ya Mali iliichapa Botswana mabao 4-1 na kujikatia tiketi ya kushiriki fainali hizo, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja uliokarabatiwa wa Lobatse.
 Magoli ya Mali yalifungwa na Cheikh Tidiane Diabate, Modibo Maiga, Mahamadou Samassa na Abdou Traore na kuwafanya Mali wawe na ushindi wa jumla wa mabao 7-1.
Mali walishika nafasi ya tatu kwenye fainali zilizopita.
Ghana walikuwa wa kwanza kufuzu kwa fainali hizo, baada ya mchezaji wao mahiri, Afriyie Acquah kufunga bao pekee kwenye mchezo wake dhidi ya Malawi uliofanyika mjini Lilongwe.
Acquah aliitwa kwenye kikosi hicho dakika za mwisho kuchukua nafasi ya majeruhi. Katika mchezo wa kwanza, Ghana walishinda mabao 2-0 nyumbani.
Timu hiyo ya Afrika Magharibi ilikuwa ikipewa nafasi kubwa kutwaa kombe mwaka huu, lakini waliishia nusu fainali, walipotolewa na Zambia.
Waliishia kushika nafasi ya nne, baada ya kupokea kichapo kutoka kwa Mali katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.
fainali za Mataifa ya Afrika zinafanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Januari 19 hadi Februari 10 mwakani, na ni moja ya michezo yenye mvuto barani Afrika na kwingineko.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TFF, serikali wazikamua klabu

Cameroon nje Kombe la Mataifa Afrika