in , ,

KUFUZU EURO 2016:

 

*Uholanzi waduwazwa

 

*Ubelgiji, Italia, Wales safi

 

Matumaini ya Uholanzi kuvuka moja kwa moja kwa ajili ya fainali za michuano ya Euro 2016 yamepata pigo kubwa baada ya kufungwa 1-0 na Iceland jijini Amsterdam.

Uholanzi waliobadili kocha majuzi tu, kwa kumwondoa Guus Hiddink na kumpa nafasi hiyo Danny Blind walikuwa na wakati mgumu dhidi ya timu ambayo haijapata kuingia fainali hizo katika historia yake.

Bao la Iceland liltiwa kimiani na kiungo wa Swansea, Gylfi Sigurdsson mapema katika kipindi cha pili kwa njia ya penati, ambapo kwenye kipindi cha kwanza Mdachi Bruno Martins Indi alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Kolbeinn Sigthorsson.

Kwa hali ilivyo sasa, Uholanzi wanashika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, wakiwa nyuma ya Jamhuri ya Czech kwa pointi sita na nyuma ya vinara Iceland kwa pointi mbili.

Katika mechi hiyo, mshambuliaji mkongwe aliyepata kucheza Arsenal na Manchester United kabla ya kutimkia Fenerbahce, Robin van Persie alikuwa kwenye benchi la Uholanzi tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo, wakati Daley Blind wa Man U alicheza dakika zote 90.

Asilimia moja ya wananchi wote wa Iceland walisafiri hadi Amsterdam kujionea pambano hilo na kuondoka kwa furaha kubwa baada ya ushindi muhimu. Iceland ni kisiwa cha Nordic chenye watu 323,002.

Kocha wao, Heimir Hallgrimsson alisema kwamba wapo juu kwa sasa, katika kilele cha mafanikio ya soka. Katika mchezo wa kwanza jijini Reykjavik, Iceland waliwatandika Uholanzi 2-0 kwa mshangao wa wengi, na ikiwa watashinda mechi ya Jumapili hii dhidi ya Kazakhstan watafuzu moja kwa moja.

Kwa upande mwingine, kichapo kwa Uholanzi, kikiwa ni cha tatu kwenye mechi hizi za kufuzu, kinamaanisha kwamba watatakiwa kujitahidi kwenye mechi tatu zilizobaki, huku wakiwaombea mabaya washindani wao wengine kwenye kundi hilo.

Wakibahatika kushika nafasi ya tatu watacheza mechi ya mchujo kupata timu moja ya kuungana na wawili wa juu. Uturuki walikwenda sare ya 1-1 na Lithuania wakati Czech waliwafunga Kazakhstan 2-1.

Katika mechi nyingine, Italia wamewafunga Malta 1-0 kwa bao la Graziano Pelle, idadi ya mabao ikiwa hiyo pia kwenye mechi ya mkondo wa kwanza. Wapinzani wa Italia katika nafasi ya kwanza kwenye Kundi H, Croatia walikwenda suluhu na Azerbaijan.

Norway wamebaki nafasi ya tatu baada ya kuwapiga Bulgaria 1-0,  kwa bao la Vegard Forren.

Katika mechi nyingine, Gareth Bale aliwajaza furaha Wales kwa kufunga bao pekee dhidi ya Cyprus na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa Euro 2016. Wales hawajafungwa na wanaongoza kundi lao

Wales hawajafungwa tangu kuanza mechi hizi za mchujo, wakiongoza kwa tofauti ya pointi tatu katika Kundi B na wanajua kwamba ushindi dhidi ya Israeli Jumapili hii utawahakikishia kuingia kwenye fainali za mwakani, na watahitimisha miaka 58 ya kusubiri kufika kwenye fainali ya mashindano makubwa.

Ubelgiji nao wamejiweka pazuri baada ya kuwafunga Boznia-Herzegovina 3-1. Alikuwa mchezaji mpya wa Manchester City, Kevin De Bruyne, mchezaji wa Man United, Marouane Fellaini na yule wa Chelsea, Eden Hazard waliotikisa nyavu, wakati Edin Dzeko alitangulia kuwafungia wageni. Ubelgiji wanashika nafasi ya pili nyuma ya Wales, wakifuatiwa na Israeli waliomalizia hasira zao kwa Andorra kwa kuwatandika 4-0.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Welbeck kitandani

Tanzania Sports

MIKEL OBI ANAIKATAA HESHIMA