in , , ,

Kombe la Dunia wingu zito


*Fifa lazima wachukue hatua kulinda heshima

FAINALI za Kombe la Dunia zipo kwenye hatua tatu za kilele, lakini ikiwa misingi iliyopelekea timu kufika huko ilikuwa na tatizo, ni wazi hadhi ya kombe hilo kubwa zaidi kwa soka itashuka.

Dhahiri ni kwamba kuna wingu, tena si dogo, linaelea juu ya utata wa masuala ya mechi za fainali za mwaka huu nchini Urusi, na kati ya hayo ni vituko vilivyoonekana kwenye mechi baina ya England na Colombia, hatua ya 16 bora ambapo kusema kweli mwamuzi mchezo ulielekea kumshinda, japo dakika za mwisho za kipindi cha pili na muda wa ziada alishituka na kuwa mzuri.

Wachezaji wa England waliingia kwenye mchezo huo na kucheza wakionekana kuwachukulia Colombia kuwa washari na Colombia walijikuta wakiwakwatua, iwe kwa sana au kidogo lakini muda mwingi mwamuzi alionekana kuharibu mchezo kwa filimbi zisizokuwa na tija na kadi zisizokuwa za lazima kwa Colombia.

Hata bao la England la penati hawawezi kujisifu kwa sababu lilitokana na penati iliyotolewa kitata, baada ya mchezaji wa Colombia kumshika na kuanguka na mshambuliaji wa England, Harry Kane wakati kona ikipigwa. haikujulikana na wala haitakaa ijulikane kama mpira huo wa penati ungefika langoni na kwamba Kane angefunga. Matukio ya kukamatwa hivyo wachezaji na kuangushwa wakati kona zikipigwa ni mengi, lakini hakuna hata moja lililovutia penati isipokuwa hilo la Kane tu.

Wachezaji wa Colombia walimvaa na kumlalamikia mwamuzi lakini kilichotokea ni kupata kadi zaidi za njano. Kuna wingu bay asana la kudanganya waamuzi au waamuzi kuvutika mapema mno na faulo ndogo ndogo na kwa kweli hali hii lazima idhibitiwe na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), vinginevyo utamu wa gemu utapotea kabisa. Zamani penati hazikuwa zikipatikana kilaini jinsi hii; ni aibu kuvuka hatua moja kwenda nyingine kwa ukandamizi dhidi ya timu nyingine na Colombia wamelia na kusikitika kwa haya.

Moja ya magumzo makubwa yanayoendelea sasa ni juu ya Neymar wa Brazil na clips nyingi tu zimetengenezwa na kutupwa mtandaoni kuonesha jinsi anavyojidai kuumia sana, akiguswa tu anaanguka na kujidai kulia hasa kana kwamba mguu umevunjika au kukatika, lakini akishagangwa na adhabu kutolewa, ndiye anayeipiga na wala haoneshi tena kuchechemea wala maumivu. Wachezaji wa zamani, wachambuzi na hata makocha wa sasa wamekemea hilo, wakisema linaharibu mchezo mzuri wa soka. Waamuzi nao wanatakiwa wajiongeze, wajue kipi kweli na kipi sicho, na si kila akienda chini mpira usitishwe. Wakati mwingine huu ni mchezo wa watu walioshiba hivyo ifike wakati watu wawe wanaume kweli kweli.

Neymar alikuwa kituko kwenye mechi dhidi ya Mexico, akiisha kuanguka au kuangushwa anajizungusha mara nyingi sana; ikiwa ameumia kweli yawezekanaje azidi kujizungusha? Si atazidi kujiumiza? Haiingii akilini, lakini waamuzi wanamwendekeza tu kama yule Mark Geiger alivyowaendekeza England.

Geiger hakuwa na sababu ya kumwadhibu Carlos Sánchez kwa jambo lile na timu jinsi ile, bado Kane akapiga na kufunga penati ile uzuri kabisa. Hata hivyo, kuna vitendo vingine vingi vinafanyika mbele ya nyuso za waamuzi na hakuna hatua inayochukuliwa. Kuna wachezaji wa Colombia waliomzunguka mwamuzi na kuwa kana kwamba wanamgombeza lakini akawa anawasogeza naye kusogea tu. Cristiano Ronaldo alimropokea mwamuzi mbele ya macho yake kwenye mechi dhidi ya Uruguay, mwamuzi akamwangalia tu.

Lakini pia kuna uamuzi mwingine wa ajabu, mfano mpira kwenda kwenye mkono wa mchezaji au mkono kwenda kwenye mpira; waamuzi wamekuwa na tafsiri tofauti kabisa. Kwenye mechi baina ya Nigeria na Argentina, Marcos Rojo aliinua kabisa mkono wake kuupiga mpira ndani ya eneo la penati lakini wakanyimwa penati licha ya mwamuzi kutumia teknolojia ya VAR.

Ajabu nyingine, Gerard Pique wa Hispania alikuwa akiruka kuokoa mpira, tena ukiwa nyuma ya kichwa chake na akiwa hauoni huku amenyoosha mikono yote juu muda wote na mpira ukampiga kwa bahati mbaya; mwamuzi akatoa penati.

Ukweli ni kwamba lazima wachezaji wabadilike, maana wanatazamwa na watu wa rika tofauti na watoto na chipukizi wakiwachukulia kama watu wa kupigiwa mfano kwa siku zijazo wakati watu wazima na wazee wakitaka kuona mchezo wenye heshima na kufuata kanuni hivyo waamuzi wawe makini zaidi na watumie vyema VAR huku Fifa wakichukua somo kwa haya, vinginevyo watadharaulika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

RONALDO HAWEZI KUWA NA DAMU YA ZIDANE

Tanzania Sports

YANGA IMESHINDWA KUTIBU KILEMA CHA AKILI