in , , ,

Kocha wa pili EPL aachia ngazi


*Ni Ian Holloway wa Crystal Palace
*Fabregas atamani kurudia Arsenal

 
Ian Holloway wa Crystal Palace amekuwa kocha wa pili kuachia ngazi miongoni mwa makocha 20 wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Holloway (50) aliyefanya kazi kubwa kuipandisha daraja klabu hiyo ya jijini London, amejikuta katika wakati mgumu, kwani katika mechi nane amekusanya pointi tatu tu.

Kocha huyo mwenye maneno mengi na mvuto kwa waandishi kabla na baada ya mechi msimu huu na mingine kabla aliyokuwa EPL kabla ya kushuka daraja, amekubaliana na klabu kwamba ni jambo jema zaidi kwake kung’atuka.

Ameondoka wakati Palace wakijiandaa kuumana na Arsenal, na tayari kocha Arsene Wenger ameeleza masikitiko yake kwa kuondoka kwa Holloway, akisema ni mtu wa soka, ana mambo mazuri ya aina yake, alipigana kuipandisha timu na anaamini atarejea baada ya muda mfupi.

Inasemwa kwamba kocha wa zamani wa Stoke, Tony Pulis huenda akachukua mikoba ya Holloway. Kocha wa kwanza kupoteza kazi EPL msimu huu alikuwa Paolo Di Canio wa Sunderland, ambaye katika mechi tano alikuwa na pointi moja tu, na hadi sasa timu hiyo haijaongeza pointi.

Holloway anaondoka akiwa amefundisha timu hiyo ya Selhurst Park kwa pungufu ya mwaka mmoja, lakini alipata kuwa EPL akiwa na timu nyingine.

Holloway alijaribu kwa nguvu kuzuia klabu nyingine, ikiwamo Arsenal kumkaribia mchezaji wake nyota, Wilfred Zaha (20), lakini hatimaye Manchester United walimchukua Januari mwaka huu, wakamwacha kwa mkopo Palace hadi msimu wa kiangazi walipomchukua.

Holloway alipata kuwapiga vijembe Arsenal juu ya kumtaka Zaha, ambapo mbele ya waandishi wa habari alidai kinda wake huyo alikuwa ameumia, hivyo angekuwa nje ya dimba kwa muda mrefu, na kuwataka  The Gunners kumsahau kabisa.

Palace wameshinda mechi moja na kupoteza nyingine zote saba kwenye ligi msimu huu, jambo linalowapa wasiwasi wamiliki kwamba watarudi walikotoka mwisho wa msimu.

Mechi iliyopita Jumatatu walibamizwa 4-1 na Fulham na kuachwa wakiweweseka, ambapo Mwenyekiti wa Klabu, Steve Parish alisema kwamba baada ya kukutana na Holloway, kocha huyo aliona kwamba mwelekeo tofauti unahitajika ili kuiacha timu kwenye ngazi hii ya juu zaidi ya soka la England.

Kocha Msaidizi, Keith Millen ametajwa kukabidhiwa timu kwa dharura kwa ajili ya mechi yao ngumu dhidi ya Arsenal Jumamosi hii.
 
FABREGAS: NITARUDI ARSENAL

Ian Holloway
Ian Holloway

Katika tukio jingine, nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal, Francesc ‘Cesc’ Fabregas amesema anatamani siku moja arudi Arsenal.

Mhispania huyo anayechezea Barcelona, amesema Arsenal wapo katika moyo wake na tamaa yake ni siku moja kurudi ama kama mchezaji au katika nafasi yoyote watakayompatia.

Anasema aliondoka vyema bila kugombana na mtu na kwamba anaamini hata Arsenal wenyewe walimuelewa aliporudi Barca, kwani alikuzwa kwenye timu ya vijana – La Masia inayomilikiwa na Barca.

Akizungumzia hilo, Kocha Wenger alisema milango ipo wazi na kufurahia kwamba alilokuwa amelisema awali juu ya uwezekano wa Fabregas kurudi sasa limetoka kinywani mwake mwenyewe.

Wenger alipata kusema huenda Fabregas (26) akarudi Emirates alikocheza mechi 303 kabla ya kujiunga Barca 2011 kwa dau la pauni milioni 35.

Fabregas amedokeza pia kwamba angependa kuwa kocha hapo baadaye na akasema Arsenal wana nafasi kubwa sasa ya kupambana kupata ubingwa wa England, akisema Mesut Ozil aliyenunuliwa kutoka Real Madrid ni hazina kubwa inayoweza kutumiwa kufanikisha azma hiyo.

Ozil amecheza vyema mechi zote tangu ajiunge na Arsenal, ambapo pekee waliyopoteza ni ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund, ambapo walifungwa 2-1 na Wenger amesema kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa mgonjwa kabla ya mechi, lakini akajituma kucheza.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Gor Mahia mabingwa Kenya

Arsenal see off brave Palace..