in ,

KINACHONISHANGAZA SURA YA NYONI INAZEEKA MIGUU YAKE INARUDI UTOTO

Rolling Stone ndiyo mahali sahihi ambayo unaweza kupataja kama chimbuko la Erasto Nyoni. Hapa ndipo yalikuwa machimbo sahihi yaliyotumika kuchimba hili dini.

Dini ambalo limekuwa faida kwa muda mrefu katika taifa letu. Kuna wakati huwa tunalibeza sana, na kuna wakati mwingine dharau huvaa ndimi zetu na kufungua vinywa vyetu kwa kutamka maneno ya kumdharau yeye.

Vinywa vyetu havijawahi kuvikubali vitu vizuri kwa uharaka zaidi, vinywa vyetu havijawahi kuvikubali vitu vinavyocheza nje ya Simba na Yanga, ndiyo maana tulikuwa tunamdharau sana Nyoni kipindi anaitwa timu ya taifa akitokea nje ya vilabu hivi viwili.

Nafsi zetu zilikuwa zinauma sana!, chuki za waziwazi zilikuwa zinaoneakana kwenye nyuso zetu kwa sababu tu wachezaji wetu pendwa hawakuitwa ila Erasto Nyoni ameitwa.

Wachezaji ambao mioyo yetu inayoongozwa na matamanio iliamini kuwa wanafaa kuitwa kuliko Erasto Nyoni, na wakati mwingine hata timu yetu ilipokuwa inafungwa tulitafutia kichaka cha Erasto Nyoni kujifichia.

Tuliongea mengi sana ya kukatisha tamaa , tulifanya kukebehi sana, na wakati mwingine tulisema “utaanzaje kushinda wakati una Erasto Nyoni katika kikosi chako?”. Tena tulienda mbali kwa kusema ni mchezaji mzee!.

Kwa kifupi tuliona ni mchezaji ambaye hakufaa kabisa kuwepo katika timu yetu ya taifa. Inawezekana umuhimu wake haukuonekana sana kwa kipindi cha nyuma kwa sababu alikuwa nje ya timu za kariakoo (Simba na Yanga).

Hakuwahi kuishi, kusali na kuabudu akiwa katika ardhi ya Kariakoo. Ardhi ambayo inaaminika kila mchezaji mzuri lazima afike pale. Kama hujawahi kufika pale basi hujakamilika kuwa mchezaji mzuri!.

Kwa kifupi kwetu sisi Kariakoo tumeiweka katika picha mfano wa Hijja, ambapo kila mchezaji lazima aende Ku ” Hujji” ili kukamilisha ibada ya mpira wa Tanzania.

Hiki ndicho alichokifanya Erasto Nyoni, alienda Ku “Hijji” kama hitaji kuu la dhehebu letu la mpira. Alienda kutimiza moja la hitaji kubwa, alienda kukamilisha ule msemo wa kuwa ili uonekane bora lazima ucheze Kariakoo.

Na hapa ndipo imani kubwa kwa mashabiki juu ya Erasto Nyoni ilipoanzia. Msimu Jana alikuwa katika bunga ya msimbazi. Aliwinda vizuri kwa kila silaha na nafasi ambayo alipangiwa. Alianza kupangwa kama beki wa kulia, mawindo yalikuwa makubwa tu kwa upande wake.

Ilifikia hatua mpaka akawa ametoa pasi 6 za mwisho. Kocha akaona amweke katika upande wa kushoto kama beki wa kushoto, alifanya kila liwezekanalo ili tu alete nyama kutoka mawindoni. Na mwisho wa siku alifanikiwa kwenye hilo!.

Kuonesha uhodari wake , msimu jana alicheza Method Mwanjali wakiwa mabeki wa kati. Na nafasi zote hizo Erasto Nyoni alicheza kwa uhodari wa hali ya juu. Na msimu tunamuona alicheza nafasi ya beki wa kati na Pascal Wawa.

Na kipindi ambacho timu ilikosa kiungo wa kati wa kuzuia Erasto Nyoni alitumika kama silaha ya ziada. Silaha ambayo haikuwa buku. Silaha ambayo ilikuwa na shabaha hata bila kubebwa na mlenga shabaha!.

Aliweza kutimiza majukumu ya kila nafasi kwa uhodari bila kupungua kiwango chake. Hapa ndipo umuhimu wa mchezaji kama huyu huonekana. Ndiyo ni vigumu sana kumuona kocha akiacha kumwiita Erasto Nyoni katika timu ya Taifa kwa sababu ni silaha ambayo hutumika wakati ambao timu ya taifa huwa imeishiwa silaha.

Na hii lilionekana jana katika mchezo wa Tanzania na Cape Verde. Mechi ya kwanza timu yetu ya taifa ilikuwa imezidiwa kwa kiasi kikubwa sana katika eneo la kati, eneo ambalo kiungo ambaye tulikuwa tunamtegemea alikuwa majeruhi (Jonas Mkude).

Hatukuwa na silaha ya ziada, Emmanuel Amunike aliamua kwenda dukani kununua silaha ya ziada, silaha ambayo ni kongwe. Silaha ambayo ina umri mrefu na uzoefu mkubwa silaha. Lakini ni silaha ambayo ina makali pamoja na kuwa na umri mrefu.

Makali ambayo yalionekana jana. Erasto Nyoni alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuilinda safu ya ulinzi ya timu ya taifa na akaleta utulivu katika eneo la kati. Utulivu ambao haukuwepo katika mechi iliyopita ya iliyochezwa Cape Verde.

Kwa kifupi yeye ndiye alikuwa chachu ya ushindi, aliongeza kitu ambacho hakikuwepo tulipoenda Cape Verde. Kitu ambacho tulikiihitaji sana kuwa nacho siku hiyo, lakini kilikuwepo katika miguu ya Erasto Nyoni pekee. Miguu ambayo kila uchwao hurudi utoto ilihali umri wake unasonga kwenda mbele!.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Zigo la lawama tunalishusha kwa Amunike na kusahau ubovu wa njia zetu!

Tanzania Sports

Niliwahi kumuona “PEP GUARDIOLA” Kwenye mwili wa “MASOUD DJUMA”.