in

Kim Poulsen atupie jicho kipaji cha Kelvin John

Baada ya mchezo kati ya Tanzania na Benin yapo mambo mazuri katika timu yetu ambayo yanapaswa kukubaliwa kuwa ni heshima na kuwapongeza wachezaji wetu. Taifa Stars inawinda tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022. Kikosi cha Taifa Stars kina vijana venye viwango tofauti na umri tofauti.

Kwa mara nyingine TanzaniaSports inachunguza mwenendo wa uchezaji wa timu hiyo na kuibua mada mbalimbali ambazo zinatoa mchango wa mawazo wa namna ya kuimarisha kikosi chetu cha taifa. Endelea kusoma.

IKO WAPI NAFASI YA KELVIN JOHN?

Heshima moja kubwa aliyonayo Kim Poulsen ni kujenga msingi katika timu yake. msingi huo ni ule wa kutoka timu za vijana hadi wakubwa. Ndani ya kikosi cha Taifa Stars kuna wachezaji waliowahi kufundishwa na kocha huyo wakiwa timu za vijana.

Kwa mfano Novatus Dismas, Meshack Abraham, Israel Mwenda, Dickson Job, Ramadhani Kabwili na Nickson Kibabage. Msingi huo unakisaidia kikosi cha Taifa Stars kuwa na wachezaji wanaotengeneza kombinenga muhimu na yenye mafanikio. 

Hata hivyo ukiangalia mwenendo wa timu yenyewe utaona bayana mshambuliaji chipukizi wa KRC Genk ya Ubelgiji anastahili kuitwa katika kikosi hiki. 

Endapo sababu itatolewa kuwa ni mbio za kuwania kufuzu hivyo wanahitajika wachezaji wazoefu, ni muhimu kujiuliza lini tutamtengenezea uzoefu kijana wetu huyo? 

Kelvin ni rika la akina Erling Halland, kwa sababu ametanguliwa miaka mitatu tu. Vilevile kama suala la umri linatengeneza hoja, basi tunaweza kurejea mfano wa wiki hii ambapo kocha wa Hispania, Luis Enrique alimpanga kinda Gavi mwenye umri wa miaka 17 na alicheza kwa dakika 83. 

Enrique katika maelezo yake ya kumpanga Gavi licha ya umri mdogo kucheza na Sergio Busquet na Koke, alisema walimtuma kufanya kazi moja tu; kumfuatilia na kumdhibiti Marco Verrati kila anapokuwepo na mpira au bila mpira. 

Kazi hiyo Gavi aliifanya kwa ufanisi hali ambayo imeibua gumzo ‘kitoto’ chenye umri wa miaka 17 kisicho na uzoefu kimeonesha namna kinavyoweza kucheza kwa umahiri. Katika safu ya ushambuliaji Taifa Stars bado nafasi ya Kevlin John ingalipo. 

Kocha Kim Poulsen anatakiwa kutengeneza wasifu wa mshambuliaji wetu huyu na kupandisha hadhi katika kikosi cha KRC Genk. Poulsen akumbushwe kuwa suala sio mchezaji huyo kulisaidia taifa tu, bali pia kumsaidia mchezaji huyo kupandisha hadhi yake katika kandanda. 

Kwa nchi zilizoendelea, Kelvin John anakuwa mchezaji anayepewa nafasi ya kutengeneza kombinenga na mwendelezo muhimu angali kijana kwa kucheza na wazoefu kama Mbwana Samatta, Reliant Lusajo,Kibu Dennis na wengineo?

MSHAMBULIAJI MBADALA NI YUPI?

Safu ya ushambuliaji ilikosa mabao ya wazi katika mchezo dhidi ya Benin. Hii ina maana Kim Poulsen anatakiwa kuinoa safu hiyo iweze kupachika mabao ya kutosha. 

Ikiwa John Bocco,Simon Msuva,Reliant Lusajo na Kibu Dennis wakichemsha kwenye mchezo ni nani anaweza kuchukua nafasi zao kama si Kelvin John? Kama benchi la ufundi linadhani Kelvin John anatakiwa kusubiri basi ni wazi wanajaribu kuporomosha ari ya mchezaji huyo. 

Hivi karibunu Kelvin alikuwa gumzo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa vijana, ambapo alipachika mabao yaliyopa ushindi timu yake. 

Sisemi yeye anaweza kubeba mzigo mzito kuliko washambuliaji waliopo, badala yake ni namna tunayweza kumtumia katika umri huo akiwa hana woga,ari,kumjengea kujiamini,kutuma ujumbe kwa mataifa mengine kuwa ni nyota wetu kabla hajashawishiwa kuchukua uraia wa nchi zingine. 

Kubwa zaidi Kelvin John ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kuoachika mabao, hatuwezi kusema asubiriwe hadi atomize miaka 22 na zaidi, wakati wapo wachezaji katika umri wa miaka 17,18,19,20 wanatamba katika vilabu mbalimbali. 

Pia hatuwezi kujidanganya kuwa Taifa Stars inao washambuliaji wakali na wenye maarifa ya kigeni kama Kelvin John. Kinda huyo kucheza KRC Genk ni kupatiwa maarifa zaidi ya wachezaji waliopo katika Ligi Kuu tanzania Bara, na pia amejifunza akiwa shule ya soka Leicester City. Kelvin ana kile ambacho kwa kimombo husemwa ‘exposure’. Misingi anayopitia ni tofauti na washambuliaji wetu wengi wa sasa. 

AJIFUNZE KWA KAKA ZAKE

Wakati Taifa Stars ikiwa imerundika mzigo mzito kwa Samatta, je ni mchezaji gani mwingine ambaye atapokea majukumu hayo? Simon Msuva? John Bocco? Kibu Dennis? Reliant Lusajo? Ni mshambuliaji yupi mwenye maarifa mapya ambaye atalisaidia taifa hili? 

Tukubali kumtumia Kelvin John kuanzia sasa kama ambavyo tunawakuza wale waliopitia timu ya taifa za vijana niliowataja hapo juu. 

Kocha Kim Poulsen licha ya uwezo wake mzuri, akumbushwe kuwa taifa letu linazo hazina ambazo zinatakiwa kuendelezwa. Licha ya anaowaendeleza sasa kwa sababu alikuwanao timu za vijana, aambiwe kuwa wapo vijana wengine ambao hawakuwa naye lakini wanahitaji kuendelezwa na kukomazwa. 

Akumbushwe hata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi nafasi ya Kevlin John ilikuwepo. Na michezo mingine ya kirafiki nafasi ya Kelvin John ingalipo. 

Ni wakati kumpa nafasi Kelvin John ili kumpandisha daraja la soka badala ya kusubiri ajipandishe mwenyewe huko Genk. Kumwita timu ya taifa ni faida kwake binafsi,klabu yake na Taifa Stars kwa ujumla. Ni maslahi mapana ya nchi yetu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Newcastle United ni habari ya mjini sasa

Yanga Vs Simba

Ni shangwe za mtoko, mapato na maendeleo ya soka