in , , ,

KIM ATAJA 26 STARS WA KUIVAA MOROCCO

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen leo (Mei 16 mwaka huu) ametaja kikosi cha wachezaji 26 watakaoingia kambini kujiwinda kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco.

Katika kikosi hicho, Kim ameita wachezaji wapya sita ingawa baadhi yao wamewahi kuchezea timu hiyo, huku akiacha wengine watatu aliokuwa nao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Morocco ambapo Taifa Stars ilishinda mabao 3-1.

Wapya aliowaita katika kikosi hicho kitakachoingia kambini Mei 20 mwaka huu, saa 1 jioni kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam ni Ally Mustafa, Vicent Barnabas, Juma Luzio, Haruna Chanongo, Mudhathiri Yahya na Zahoro Pazi. Wachezaji aliowaacha ni Shabani Nditi, Nassoro Masoud Cholo na Issa Rashid.

Kikosi kamili cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ambacho kabla ya kwenda Morocco kitapita jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kirafiki Juni 2 mwaka huu dhidi ya Sudan ni kama ifuatavyo;

Makipa ni nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).

Kocha Kim amesema kikosi kitakachoingia kambini kitakuwa na wachezaji 24 ambapo Samata na Ulimwengu watajiunga na timu jijini Marrakech, lakini wachezaji atakaondoka nao Dar es Salaam kwenda Addis Ababa ni 22 ambapo ataacha kipa mmoja na mchezaji mmoja wa ndani.

Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.

Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.

TANZANIA YAJIONDOA MICHUANO YA COSAFA
Tanzania (Taifa Stars) imejitoa kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayofanyika nchini Zambia kuanzia Julai 2-26 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah amesema Stars ambayo iliingizwa katika michuano hiyo kama timu mwalikwa imejitoa kutokana na mwingiliano wa ratiba kati ya michuano hiyo na mechi za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Amesema awali Tanzania ilithibitisha kushiriki michuano kwa matarajio kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF la kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) likagoma kwa vile kipindi ambacho kilipendekezwa lenyewe litakuwa na uchaguzi wa viongozi wao.

Taifa Stars itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi za CHAN ambapo mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu wakati ya marudiano itafanyika jijini Kampala kati ya Julai 26-28 mwaka huu.

Akizungumzia michuano ya COSAFA, Kocha Kim amesema angependa kushiriki michuano hiyo kwani ingekuwa kipimo kizuri kwa kikosi chake, lakini kwa sasa malengo makubwa ya Stars kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo fainali zake zitafanyika mwaka 2015.

TIKETI SIMBA, YANGA KUANZA KUUZWA KESHO
Tiketi kwa ajili ya pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Yanga litakalochezwa keshokutwa (Jumamosi) kwenye Uwanja wa Taifa zitaanza kuuzwa kesho (Ijumaa) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Vituo vitakavyouza tiketi hizo kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni ni Uwanja wa Taifa, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, OilCom Ubungo, kituo cha mafuta Buguruni, BMM Barbershop Sinza Madukani, Dar Live Mbagala na Sokoni Kariakoo.

Tiketi hizo zitakuwa zikiuzwa katika magari maalumu yaliyoegeshwa katika vituo hivyo. Viingilio katika mechi hiyo ya kufunga msimu ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani, sh. 7,000 viti vya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B n ash. 30,000 kwa VIP A.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Rafa Benitez afunika tena

Beckham: Miaka 20 safi ya soka