in , ,

KIFO CHA TIMU ZA AFRIKA KILIANZIA HAPA

Mwaka 1982 ndiyo ulikuwa mwaka wa mwisho kwa timu kutoka bara la Afrika kushindwa kupeleka timu angalau moja katika hatua ya mtoano ya kombe la dunia.

Tangu mashindano ya kombe la dunia la mwaka 1986 bara la Afrika limekuwa likipeleka angalau timu moja katika hatua ya mtoano ya kombe la dunia.

Ilikuwa jambo la faraja kwetu, haikujalisha uchache wetu wa kuwa na wawakilishi watatu lakini tulikuwa na uwezo wa kuonesha vipaji vyetu ambavyo tulijaliwa kuwa navyo.

Vipaji ambavyo viliwashawishi FIFA kutuongezea idadi ya timu shiriki katika kombe la dunia. Ikawa faraja kwetu sisi, tabasamu la furaha likawa limepamba nyuso zetu na hii ni kwa sababu moja, tulikuwa na uwezo wa kuwa na washiriki watano kutoka katika idadi ya washiriki watatu wa awali.

Imani ya kufanya vizuri ikawa imeongezeka kwa sababu ya idadi ambayo tuliipata. Kombe la dunia la mwaka 1990 likatupa mwanga kuwa kuna siku tunaweza tukafika mbali.

Kupitia miguu yenye ukomavu wa miaka 42 ya Roger Milla kwa wakati ule tuliweza kufika hatua ya robo fainali.

Mwanga wa mafanikio kwa mbali ukaanza kuonekana. Watu wengi wakawa na imani kuwa siku ya timu kutoka Afrika kufanya vizuri imeshawadia.

Ndiyo maana hata mkongwe ambaye ni mfalme wa soka ulimwenguni Pele aliwahi kutabiri kuwa timu kutoka Afrika itashinda kombe la dunia.

Maneno yake yalikuwa na baraka kubwa sana kwani kauli yake hii aliyoitoa mwaka 2000 ilikuwa ni kauli yenye  nguvu na baraka kubwa kwa bara la Afrika kwa sababu kombe la dunia la mwaka 2002 tuliisimamisha dunia kwa kuweza kufika hatua ya robo fainali ya kombe la dunia.

Goli la dhahabu likawa kisu kwetu, kisu ambacho kilikatisha uhai wa vipaji vya kina  Aliou Cisse ambaye mwaka huu amekuja kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya Senegal.

Unakumbuka kipi  kipindi jina la Khalilou Fadiga linapotajwa?, kipi kinachomhusu El-Hadji Diouf kinakuja katika kumbukumbu yako kipindi jina lake linapopita sikio mwako?.

Hapana shaka vilikuwa vipaji bora ambavyo vilikuwa vinacheza kwa kujituma kwa ajili ya taifa lao. Muda wote wa mchezo walikuwa makini kwa sababu walikuwa wanajua furaha ya taifa na bara zima la Afrika ilikuwa katika mikono yao.

Thamani ya kucheza katika bara la ulaya tena katika timu kubwa ilionekana. Walitumia uzoefu wao wa kupata nafasi ya kucheza ulaya na kuuweka katika timu za taifa.

Haikuwa ngumu kwao kucheza ndani ya mbinu yoyote ambayo mwalimu wao alihitaji kuitumia. Ndiyo maana walifanikiwa kufanya vizuri.

Utofauti huu unaonekana kwa timu ambazo zimeenda kutembea Russia mwaka huu. Timu ambazo zilikuwa na nyota ambao wanacheza katika bara la ulaya lakini hawakuonesha faida ya wao kucheza katika vilabu vya bara la ulaya.

Umakini ulikuwa hafifu ndani yao. Ndiyo maana walianza vibaya tena kwa kufungwa magoli yanayofanana. Magoli ya mipira ya krosi au iliyokufa tena katika dakika za mwisho.

Senegal ilianza kutoka katika michuano hii kwenye mechi dhidi ya Japan. Mechi ambayo walikuwa na asilimia kubwa ya kushinda kuliko Japan lakini ukosefu wa umakini uliharibu furaha ya Waafrika wengi.

Senegal walikuwa wanacheza kama wameridhika na walikuwa wameshajihakikishia matokeo chanya kwao kabla hata filimbi ya ya mwisho ya mwamuzi.

Hawakuwa na uchungu wa kupigana kwa umakini na kwa nguvu. Hili ndilo gonjwa kubwa lililo sababisha kifo chetu kule Russia, gonjwa ambalo  kwa bahati mbaya timu zote za Afrika zilikuwa zinaumwa na dawa zilikuwa mikononi mwa wapinzani wetu.

Ilikuwa ngumu kwa pamoja kwenda kuzichukua dawa ili kumeza kwa sababu tulimwihitaji mtu mmoja atupiganie.

Huwezi kufika mbali kama una jemadili mmoja kwenye jeshi lako la farao, ndiyo maana timu yao ilishindwa kufika mbali kwa sababu ilijengwa kupitia Mohamed Salah.

Kitu hiki hakikuwepo kwenye mafanikio ya Ghana kwenye kombe la dunia la mwaka 2010 kule South Afrika. Umoja wao ndiyo ulikuwa nguzo ya mafanikio yao.

Walitengeneza timu ambayo inacheza kwa pamoja licha ya kujaza nyota wengi na kuacha kutegemea mtu mmoja ndani ya uwanja. 

Misri hakuwa peke yake kwenye hili janga hata Nigeria ilifikia kipindi matumaini yao yalibaki kwenye miguu ya Ahmed Musa kama ilivyokuwa kwa Senegal ilivyokuwa inatamani Saido Mane kuwa na miguu ya Cristiano Ronaldo lakini utofauti wa ukomavu wa maamuzi ukamfanya Saido Mane abaki katika daraja la ukawaida lisilo na nguvu za kuhimili mafuriko.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

GAZETINI ANAONEKANA NEYMAR, UWANJANI ANAONEKANA COUNTINHO

Tanzania Sports

UFARANSA NA ARGENTINA: VITA YA MREMBO WA SASA NA MREMBO WA ZAMANI