in , ,

KESSY ANAWAPA SIMBA FUNZO WANALOSTAHILI

 

Kitita cha milioni sitini za kitanzania ndicho kitu pekee kitakachowawezesha Simba SC kubaki na mlinzi wao mahiri wa kulia baada ya msimu huu kumalizika miezi michache ijayo.

Mkataba wa miezi 18 ambao mlinzi huyo wa kulia, Hassan Kessy alisaini Disemba mwaka juzi utamalizika Juni mwaka huu. Amegoma kusaini mkataba mwingine ikiwa hatapatiwa milioni 60 anazohitaji.

Hivi kiwango cha Hassan Kessy kimekuja kuonekana wakati huu ambapo mkataba wake umebakisha miezi mitatu pekee kumalizika?! Hapana, Kessy amekuwa akionyesha kiwango cha juu tangu alipotua Msimbazi.

Aprili mwaka jana uongozi wa Simba ulionyesha wazi kuwa ulitambua kiwango alicho nacho Kessy. Ni pale mlinzi huyo wa kulia alipogoma kusafiri na timu kwa ajili ya mchezo wa VPL dhidi ya Kagera Sugar.

Alikuwa akiushinikiza uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi umlipe fedha za usajili alizokuwa akidai pamoja na nyumba ya kuishi aliyokuwa ameahidiwa. Uongozi wa klabu ukafanya jitihada zote na kumlipa Kessy madai yake.

Simba SC walitambua umuhimu wa Kessy tangu wakati huo. Inanishangaza kuona wakati wote huo hakukuwa na jitihada za kumrefushia mkataba kijana huyo.

Jitihada hizo zilianza kujitokeza Novemba mwaka jana wakati mkataba wa mchezaji huyo ulipokuwa umebakisha miezi saba pekee kufikia mwishoni. Dylan Kerr alinukuliwa akiuomba uongozi wa Simba uhakikishe Kessy anabaki Msimbazi.

Tangu wakati huo kulishakuwa na tetesi kuwa klabu za Yanga na Azam zinavutiwa na mchezaji huyo. Inaaminiwa kuwa kuna donge nono ambalo Kessy ameahidiwa na moja kati ya klabu hizo ama azote mbili.

Na ndio maana mchezaji huyo anahitaji kiasi hicho cha fedha ili asaini mkataba mpya. Kama klabu inacho kiasi hicho cha fedha si tatizo. Ila vinginevyo ni tatizo kwao.

Naziona dalili za wazi kuwa Simba hawataweza kumbakisha mchezaji huyo muhimu Msimbazi baada ya msimu huu. Hata mwalimu Jackson Mayanja anaonekana kukata tamaa.

Mayanja amenukuliwa akisema kuwa kama Kessy hataki kurefusha mkataba wake basi aachiwe aende zake. Hii haiwezi kuwa na maana kuwa Mayanja hakitambui kiwango cha juu alicho nacho Kessy.

Kocha huyo anautambua wazi umahiri alio nao Kessy ndani ya uwanja. Amemtumia Kessy karibu kwenye kila mchezo tangu alipotwishwa mikoba ya timu hiyo. Na Kessy ameonyesha kiwango cha kuridhisha kwenye michezo hiyo.

Ila tu kuna methali fulani inayomuelekeza Mayanja kusema kuwa kama Kessy hataki kurefusha mkataba aachiwe aende zake. Methali hiyo ni ‘La Kuvunda Halina Ubani’.

Swala la Kessy sasa linaonekana kuvunda. Na kama ni kweli limevunda basi ni wazi kuwa halina ubani. Hata la Singano lilivunda na likakosa ubani na Simba hawakuwa na namna zaidi ya kumuachia mchezaji huyo.

Kuna kitu muhimu ambacho Simba SC na klabu nyingine za nyumbani zinashindwa kujifunza kutoka kwenye klabu za nje. Zinashindwa kujifunza namna ya kutawala mikataba ya wachezaji.

Klabu za nje huwa zinafanya jitihada za kurefusha mapema mikataba ya wachezaji wao muhimu. Huwa hazisubiri mikataba hiyo ibakishe kipindi kifupi kwani mchezaji anaweza kushawishika na ofa za timu hasimu.

Kama Simba walishindwa kujifunza kwa makosa waliyofanya kwenye suala la Singano basi wanastahili hili funzo lingine kutoka kwa Hassan Ramadhani Kessy.

Wasipojifunza kwenye hili la Kessy wasubiri. Pengine watapata nafasi nyingine ya kujifunza kupitia kwa Ibrahim Ajib ama nyota mwingine muhimu siku za usoni.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Leicester wazuiwa lakini …

Tanzania Sports

Kilio Arsenal, Spurs, Man City