in , , ,

KAMATI YA UCHAGUZI KUJADILI SIMBA, YANGA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchaguzi ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira
wa miguu baada ya tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya
watani wa jadi (Simba na Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.

Sekretarieti ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira
wa miguu wakiomba matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na
Yanga) yafanyike katika siku tofauti.

Wakati Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu
tayari ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha kuwa
timu ambazo zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu zitacheza siku
hiyo.

Sekretarieti imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa
vile yeye na kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa
Uchaguzi. Huko nyuma TFF imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu
ya Taifa (Taifa Stars), jambo ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo
kuwa na ajenda moja tu.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha kikao
cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.

*COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800*

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya
Coca Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya
mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza
Septemba Mosi mwaka huu.

Coca Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya
ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa
kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16
itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.

Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi
ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika
Septemba 6 mwaka huu.

Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma,
Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.

Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja
wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke
na mkoa mmoja wa Unguja.

Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma
wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.

Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za
Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza
timu mbili.

* *

*Wakati huo huo,* semina ya makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki
michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi
Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9
alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.

*RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI GRACEMO BAMBAZA*

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo
cha aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma,
Gracemo Bambaza kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean
Road, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza
kwa kipindi chote akiwa mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango
wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.

Bambaza aliyezaliwa mwaka 1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika
vituo vya redio vya Wapo cha Dar es Salaam na Pride cha Mtwara
amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa
ajili ya mazishi.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira
na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina

* *

*TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI*

Tiketi kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam
itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi.

Vituo vitakavyouza tiketi hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo,
Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko
Sinza Madukani.

Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote
yanayouza tiketi yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na
bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya
VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A
watalipa sh. 30,000.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

UCHAGUZI TFF KUFANYIKA OKTOBA 18, 2013

KAMATI YAPITIA USAJILI, NGASA KUCHEZEA YANGA