in

Kama vipi tuwape uraia kina Morrison, Bangala

Kibu Denis

KIBU Dennis ni mshambuliaji mpya aliyesajiliwa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania, Simba. Nyota huyo alikuwa anakipiga katika klabu ya Mbeya City ya Jijini Mbeya. Ni miongoni mwa vipaji vinavyoinufisha Tanzania kwa sasa. Kwa wale waliotazama mchezo wa kirafiki kati ya Tanzania na Malawi mwaka huu wanakumbuka namna mshambuliaji huyo alivyokuwa mwiba kwa ngome ya The Flames. 

Uhodari wa kukaa na mpira,kasi,mashuti,muono wa mchezo ni sifa amabzo zilimwonesha katika pambano hilo. Ni dhahiri kocha mkuu wa Taifa Stars anahitaji huduma ya mshambuliaji huyo kadiri anavyoweza ndio maana amekuwa akimwita katika kikosi chake. 

Hata hivyo jina la Kibu Dennis lilikuwa mjadala mkubwa baada ya kutajwa sio raia wa Tanzania hali ambayo iliwashangaza wapenzi wa soka. Kilipotangazwa kikosi cha kuwavaa Benin katika uwanja wa Benjamin Mkapa, 

Kibu Dennis hakuweza kucheza mchezo wa mashindano ya CAF wala FIFA. Kwa mantiki hiyo Idara ya Uhamiaji ilikuwa inashughulikia suala la uraia wake. Siku chache baadaye akatangazwa rasmi kuwa raia wa Tanzania. 

Kibu Dennis ameishi maisha yake asilimia tisini akiwa Tanzania hivyo asingweza kujitaja kuwa yeye ni raia wa DR Congo.  Sasa niingie kwenye hoja yangu ya leo. 

Inafahamika Kibu Dennis hata angejitambulisha kuwa raia wa DRC asingepata nafasi ya kucheza timu ya nchi hiyo kwa sababu wengi wa wachezaji wao wanacheza nje ya nchi. 

Baadhi ya wachezaji hawakuzaliwa DRC badala yake wamerudi kuichezea nchi hiyo kwa sababu ya wazazi wao. Wapo wachezaji katika mataifa kama Tunisia, Morocco,Nigeria ambayo ynawaita wachezaji timu za taifa lakini hawakuzaliwa ndani ya nchi hizo, na hufanya hivyo sababu ya wazazi wao tu. 

Wazazi wa wachezaji hao wanakuwa wamekutana nje ya nchi,wakazaa na kuendelea kutumia hati za kusafiria za nchi hiyo. Hakim Ziyech nyota wa Chelesa, ana uraia wa Morocco lakini yeye alizaliwa Uholanzi kwa wazazi wenye asili ya Morocco. 

Wapo wachezaji katika mataifa hayo pia hata kuimba wimbo wa taifa hawajui lakini wanazitumikia nchi hizo vizuri na vipaji vyao vinawanufaisha. 

Yapo mataifa jirani hapa Kenya,Uganda na hasa Burundi na Rwanda ambayo yamekuwa yakiwatumia wachezaji waliozaliwa mataifa mengine ya jirani. Wao wanachojali ni kunufaika na kipaji cha mchezaji husika, na zaidi ni kwa sababu mchezaji huyo anakuwa hana uhakika wa kuitwa katika nchi yake ya asili. 

Taifa la Brazil linasifika kwa vipaji vingi vya soka, nalo lilishuhudia nyota wake wakichukua uraia wa Urusi na Hispania. Diego Costa alikuwa mshambuliaji anayetajika barani Ulaya na mwenye uraia wa Brazil. Lakini kwenye mashindano ya Kombe la Dunia alilazimika kuiwakilisha Hispania ambayo ilipigana vikumbo kuhakikisha anachezea nchi hiyo badala ya Brazil alikozaliwa. Wabrazil nao wakaendelea na maisha yao, hawakuhitaji huduma ya Diego Costa.

Aymeric Laporte ni raia wa Ufaransa ambaye kwa sasa ni beki kisiki wa Manchester City. Lakini nyota huyo hakuichezea nchi yake ya kuzaliwa ya Ufaransa, badala yake alicheza ngazi ya timu ya taifa ya Hispania. 

Hakuona nafasi ya kuichezea Ufaransa, hivyo ombi la kuchukua uraia wa Hispania lilipofika naye hakuzembea. Hapa sizungumzii suala uraia pacha, bali uamuzi wa mchezaji na viongozi wa timu kumpa uraia mchezaji ambaye atawanufaisha kwa kipaji chao.

Turudi hapa Bongo, kuna wachezaji wa kigeni wanaocheza katika vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara; Larry Bwalya, Chris Mugalu, Yannick Bangala, Bernard Morrison, Asamoah na wengineo. 

Wengi wa wachezaji waliopo nchini hawana uhakika wa kuitwa timu zao za taifa. Ni wachezaji wachache hupata nafasi hiyo kama walivyokuwa Cletous Chama na Luis Miquissone. kwa mnaana hiyo mamlaka zinazohusika na mchezo wa soka zinaweza kuchukua uamuzi kushawishi kuwapatia uraia wachezaji wa aina hiyo. 

Hakuna kocha mwenye kushawishika kumwita Bernard Morrison katika kikosi chake nchini Ghana kwa sbaabu anazidiwa uwezo na wachezaji wao wanaocheza Ulaya. Kwahiyo uwezekano wa Morrison kuichezea timu ya taifa ya Ghana haupo. Hilo ni pamoja na Chris Mugalu,Yannick Bangala na wengineo ambao wanaweza kuitumikia Taifa Stars. 

Wachezaji niliowataja si wa kipekee, lakini wana vipaji ambavyo vinaweza kutoa mchango mkubwa katika kikosi chetu. Mathalani, tunao wachezaji wenye vipaji vizuri katika timu yetu ya taifa na vilevile tunaweza kutathmini uwezo wa mchezaji kama Morrison namna anavyowazidi wachezaji wetu. Je ni mchezaji gani mzawa pale anamzidi uwezo Morrison,Bangala,Mugalu na wengine? 

Ninadhani tunaweza kutumia njia ya kuwavutia kwa kuwapa uraia kwa malengo ya wao kutumikia Taifa Stars. Kwa sababu hilo siyo suala  geni, linafanyika katika mataifa mbalimbali, na sasa tumempa Kibu Dennis ambaye atatunufaisha kwa kipaji chake. 

Kama wapo wachezaji ambao hawana uhakika wa kuitwa katika nchi zao, na wana vipaji vizuri basi wachukuliwe tu. Hakuna sababu za kupinga kwamba hawana mapenzi na nchi, kwani wangapi wamepewa nafasi hizo na wameshindwa kuzitendea haki au watanzania wenyewe wanakutwa na matukio ya ukosefu wa uadilifu kila kona? 

Nasema tukiacha siasa zetu zisizotusogeza mbele bila shaka tunaweza kuwa kama Hispania au England ya leo iliyojaa wachezaji wengi weusi lakini wakiwa raia halali wa nchi hiyo.

Mataifa mengi ya Ulaya kwa sasa yanachukua wachezaji kutumikia timu zao za taifa ili kunufaika na vipaji vyao. Kuanzia Sweden,Uswisi,Denmark,Italia,Urusi na kwingineko wapo wachezaji weusi ambao hawakuzaliwa huko lakini wamepewa uraia kwa ma;lengo maalumu wazinufaishe nchi hizo kutokana na vipaji vyao. Nafikiri kina Morrison wanaingia kundi hili, hakuna kocha mwenye mpango kumwita kule Ghana, sasa kwanini tusichangamkie kipaji hicho? Nafungua mjadala.

Baruapepe; [email protected]

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
West Ham

Nani huyu anataka kuinunua West Ham United?

Xavi Hernandez

Xavi kurudisha tabasamu Barcelona?