in , , ,

Jurgen Klopp – Kipimo cha kwanza..

Tottenham vs Liverpool

 

Tottenham Hotspur wakiwa nyumbani, White Hart Lane kesho Jumamosi watawakaribisha Liverpool kwenye mchezo wa raundi ya tisa ya Ligi Kuu ya England. Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa Jurgen Klopp akiwa meneja wa Liverpool aliyojiunga nayo wiki iliyopita kufuatia kutimuliwa kwa Brendan Rodgers aliyekuwa meneja kabla yake.

Itakumbukwa Tottenham bado hawajapoteza mchezo wowote kwenye dimba lao la nyumbani kwenye michuano hii msimu huu na wiki tatu zilizopita waliwaadabisha vinara wa EPL Manchester City kwa kipigo cha mabao manne kwa moja kwenye dimba lao hilo la White Hart Lane.

Liverpool mbaka sasa wameshinda mchezo mmoja tu dhidi ya Stoke City kati ya michezo minne waliyocheza ugenini msimu huu huku wakipoteza mwingine mmoja dhidi ya Manchester United na kutoa sare miwili dhidi ya Arsenal na dhidi ya Everton kwenye mchezo wao wa mwisho wa EPL.

Jurgen Klopp anahitaji kufanya kazi ya zaida kimbinu na kiuhamasishaji ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wake huu wa kwanza. Zipo changamoto kadhaa zinazomkabili meneja huyo Mjerumani kuelekea mchezo wa kesho.

Changamoto kubwa zaidi ni kikosi chake kuandamwa na majeruhi. Nahodha Jordan Henderson, Christian Benteke, Roberto Firmino, Joe Gomez na Danny Ings hawataweza kutumika kutokana na majeraha.

Changamoto nyingine inayomkabili Klopp ni kwamba anakwenda kucheza na timu ambayo kwa mujibu wa takwimu za msimu huu ni timu bora kuliko timu anayoifundisha yeye.

Advertisement
Advertisement

Ukitazama nafasi katika msimamo wa ligi, Liverpool wapo kwenye nafasi ya 10 wakati Spurs wapo kwenye nafasi ya 8 lakini wamepishana kwa alama moja pekee ambao Tottenham wana alama 13 Liverpool wakiwa na 12.

Ukitazama pia idadi ya mabao ya kufunga, Spurs bado wako mbele. Mbaka sasa wamefunga mabao 11 wakati Liverpool wamefunga mabao 8 pekee. Pia Spurs wameruhusu mabao 7 ambayo ni machache zaidi ya mabao 10 waliyoruhusu Liverpool ambao pia wameruhusu bao kwenye kila mchezo kati ya michezo nane iliyopita kwenye mashindano tofauti.

Kwa upande mwingine takwimu hizi hazina nafasi ya kumyumbisha meneja Jurgen Klopp kuelekea mchezo wa hapo kesho  kwa kuwa zilizalishwa kwenye michezo nane ya mwanzo ambayo ilichezwa kabla yeye hajawa meneja wa klabu hii.

Hata hivyo zinaonyesha namna gani mpinzani wake Mauricio Pochettino alivyoweza kukiongoza kikosi cha Tottenham kufanya vizuri kwenye michezo kadhaa ya nyuma kiasi cha kufanikiwa kutunukiwa tuzo ya meneja bora wa EPL wa mwezi Septemba. Klopp ana kila sababu ya kumuheshimu mpinzani wake huyu.

Tukizigeukia rekodi za mameneja watatu waliopita Liverpool kabla ya Jurgen Klopp zinaonyesha kuwa hakuna aliyeweza kushinda mchezo wake wa kwanza wa EPL. Roy Hodgson alipoingoza Liverpool kwenye mchezo wake wa kwanza wa EPL Agosti 2010 aliambulia sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Arsenal.

Kenny Dalglish aliporejea Liverpool Januari 2011 alipoteza mchezo wa kwanza wa EPL dhidi ya Blackpool kwa mabao mawili kwa moja. Brendan Rodgers yeye alipokea kipigo kikali cha mabao matatu kwa sifuri kutoka kwa West Bromwich kwenye mchezo wake wa kwanza wa EPL akiwa meneja wa Liverpool.

Tunasubiri kuona matokeo ya Klopp kwenye kipimo chake cha kwanza hapo kesho. Itakumbukwa meneja huyu hakuwahi kuiongoza timu yoyote uwanjani tangu alipopoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Ujerumani ‘DFB-Pokal’ dhidi ya Wolfsburg kwa mabao matatu kwa moja Mei 30 mwaka huu.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

LEADERSHIP IS CRUCIAL FOR OUR SPORTS SUCCESS

Tanzania Sports

USHABIKI HUKU UNATAABIKA KUJENGA HIMAYA ZA WENYE MALI