in ,

Jonas Mkude: Pambana na Hali Yako!

Meneja wa zamani wa Liverpool ya Uingereza ukipenda waite Majogoo wa Anfield aliyefundisha kilabu hicho cha Merseyside kwa kipindi cha zaidi ya miaka 14 aliwahi kunukuliwa akisema timu inayoshinda mechi zake huwa kikosi hakibadilishwi, au kwa lugha ya kimombo “the winning team/side never changed”.

Kocha huyu sio mwingine bali ni Bill Shankly, mzaliwa wa mji wa Glenbuck uliopo Scotland, alitoa kauli hiyo alipoulizwa kuhusu mmoja wa wachezaji wake wa kipindi hicho ambaye hakupewa nafasi pamoja na kuwa alionekana ana uwezo wa hali ya juu.

Kauli ya Bill Shankly ya kwamba kikosi kinachokupatia matokeo mazuri [ushindi] huwa hakibadilishwi kwa kiasi fulani inashabihiana na kinachoendelea Msimbazi hasa kutokana na ukweli kwamba Kocha wao kaonekana kutokubadili sana kikosi chake hasa sehemu ya kiungo ambayo ndio uti mgongo wa timu tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara.

Anachokifanya kocha wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon naamini kingefanywa na Kocha wa timu yoyote hasa ukizingatia matokeo mazuri ambayo timu yake wamekuwa wakiyapata katika mechi nne walizocheza tangu kuanza kwa ligi kuu hivi karibuni.
Pamoja na matokeo mazuri ambayo yamekuwa yakipatikana klabuni hapo hadi wakati huu, hali hiyo ya kutokubadili kikosi hasa sehemu ya kiungo kwa timu ya Simba kumepelekea badhi ya wadau na wanazi wa timu hiyo kuanza kuhoji ni kwanini baadhi ya wachezaji hawapewi nafasi.

Kimsingi jina la kiungo Jonas Mkude ndio limekuwa halikauki vinywani mwa baadhi ya mashabiki wa Simba na katika mitandao ya kijamii wakihoji kulikoni, mbona kijana wao kipenzi hapangwi ilihali misimu michache iliyopita alikuwa sio tu ni nahodha bali pia kiungo tegemeo kwenye kikosi cha Msimbazi?

Kibaya zaidi hata baadhi ya vyombo vya habari vimeipokea agenda hiyo na kuanza kuhoji jambo hilo bila kuangalia matokeo ya Simba tangu kuanza kwa ligi kuu ya Tanzania Bara maarufu kama Vodacom Premier League [VPL] mwezi Agosti mwaka huu.

Kiungo Jonas Mkude ni matunda ya mradi wa timu ya vijana ya Simba, alifanikiwa kupandishwa timu ya wakubwa pamoja na kina Hamisi Ndemla, Singano Messi, Edward Christopher na wengineo mnamo mwaka 2012 baada ya kufanya vizuri katika timu ya vijana.
Tangu kupandishwa kwa Mkude katika kikosi cha kwanza amekuwa ni mchezaji aliyekuwa na uhakika wa kuwamo kikosini katika mechi za Simba za ligi na mashindano mbali mbali ya ndani ikiwamo kombe la Mapinduzi. Hali hii ilipelekea Mkude kupata nafasi hata katika kikosi cha timu ya Taifa, maarufu kama Taifa Stars.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa ligi msimu huu 2017/2018, nafasi ya Jonas Mkude katika kikosi cha Simba imezidi kuwa finyu, hajaweza kuanza katika mechi yoyote zilizochezwa hadi sasa na badala yake Kocha amekuwa akimtumia James Kotei kama kiungo wa kuzuia.

Ni ukweli usiopingika kwamba uelewano wa hali juu uliopo kati ya viungo James Kotei na Mzamiru Yasin umekuwa ndio sababu ya msingi ya kumfanya Kocha Omog kumweka benchi Jonas Mkude hasa ukizingatia matokeo mazuri ambayo timu ya Simba imekuwa ikiyapata.
James Agyekum Kotei maarufu kwa jina la James Kotei ambaye alilelewa katika vituo vya kukuza vipaji vya Corner Babies pamoja na Golden Boot Academy nchini Ghana katika ya miaka ya 2002 hadi 2009 amekuwa nguzo imara katika kuimarisha ulinzi na kuunganisha safu kiungo.

Tangu msimu mpya wa ligi uanze, chini ya Kotei na Mzamiru, kikosi cha Simba sio tu kimekuwa kikitawala sehemu ya kiungo dhidi ya wapinzani wao, bali pia kimeruhusu mabao mawili tu katika michezo minne ya Ligi jambo ambalo ni ishara tosha ya uimara wa safu ya ulinzi na kiungo, maeneo ambayo ndio msingi wa timu yoyote.

Katika mazingira ambayo timu inafanya vizuri, ni vigumu kwa Kocha yoyote kuingiza ingizo jipya hasa katika kipindi ambacho shinikizo la timu kupata ushindi ni kubwa mno kutokana na gharama kubwa iliyotumika katika ya usajili wa wachezaji.
Kinachotokea kwa nahodha wa zamani wa Simba ni kipindi cha mpito, ni upepo mbaya ambao huvuma kwa kila mchezaji kwa kipindi chake, jambo la msingi ni jinsi gani mchezaji husika amejiandaa kuukabili huo upepo na kurejea na nguvu na ari mpya pindi upepo utakapoisha.

Huu ni wakati wa Mkude na wachezaji wengine wanaopitia kipindi kigumu kama yeye kupambana na hali zao, wajitume, waonyeshe nidhamu ya hali ya juu, wasikate tamaa na wawe watimilifu kimwili na kiakili ili ikitokea siku wakipewa nafasi waweze kuitumia kikamilifu.
Alamsiki

Na Amon Petro
Email: [email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KUNA UWEZEKANO MKUBWA TIMU ZA EPL ZIKACHUKUA UTAWALA WA TIMU ZA LA LIGA MSIMU HUU

Tanzania Sports

CONTE ALIJIANGAMIZA MWENYEWE?