in

Jinsi makocha wa kigeni wanavyotawala Ligi Kuu

Didier Gomes Da Rosa

Ligi Kuu imeanza kwa msisimko wa na ushindani wa aina yake. ushindani upo kwa timu,wachezaji,makocha na viongozi. Timu zote zimeonekana kujiandaa vyema kupambana Ligi Kuu,kutwaa mataji,kubaki ngazi za juu na kutoshuka daraja. Timu wageni Geita Gold na Mbeya Kwanza zimeonesha thamani yao licha ya kutokuwa na matokeo makubwa.

Kocha mwandamizi Meja Mingange amesema kuwa kupitia mechi za awali za Ligi Kuu kumeonekana mabadiliko kwa timu mbalimbali. kocha huyo amesema ushindani uliopo Ligi Kuu kwa sasa umetokana na uwekezaji uliofanywa na Azam Media kwa kumwaga fedha ambazo zinachochea timu kujipanga vizuri na kuonesha ushindani. 

Amesisitiza kuwa mashabiki watashuhudia ushindani zaidi kutokana na hali hiyo huku timu zote zikitaka kupata mamilioni ya fedha ya wadhamini kwa kumaliza nafasi nne za juu. Kwa ushindani hupo ni muhimu kwa maendeleo ya kandanda. 

Hata hivyo Ligi hiyo yenye kushirikisha timu 16 msimu huu 2021/2022 ikiwa pungufu kuliko msimu uliopita 2020/2021 ambako kulikuwa na timu 18 imekuwa na uhaba wa makocha wazawa.

Kwenye Ligi hii kuna makocha wazawa watano tu. Hii ina maana timu zingine zote zina makocha wa kigeni. Timu zenye makocha wazawa ni Namungo (Hemed Morroco), Polisi Tanzania (Malale Hamsini), Ruvu Shooting(Boniface Mkwasa), Tanzania Prisons (Salum Mayanga), Dodoma Jiji (Mbwana Makatta), KMC (John Simkoko).

Vigogo viwili vya soka Yanga na Simba zinafundishwa na makocha wa kigeni. Didier Gomes raia wa Ufaransa na Nasredine Nabi raia wa Tunisia. Kwahiyo timu 11 zinafundishwa na makocha wa kigeni ambao bila shaka wanaongeza chachu katika ligi yetu. Je nini faida ya kuwa na makocha wa kigeni katika timu?

Mosi, maarifa mapya. Makocha wa kigeni wanakuwa wamekulia katika misingi tofauti ya soka. mfano, Gomes aliyekulia Ufaransa au Nabi aliyekulia Tunisia ni Mifano ya makocha ambao wanaleta maarifa mapya katika ligi. 

Mafunzo hayo kwa wachezaji ndiyo chachu ya mafanikio yao na kutayarisha makocha wapya ikiwa wachezaji wataamua kuwa makocha miaka ijayo. Wachezaji wanaofundishwa na makocha wa kigeni hupata maarifa mapya zaidi yay ale waliyoyazoea.

Pili, utamaduni tofauti. Katika hali ya kawaida suala la utamaduni wa maisha lazima makocha wa kigeni wataleta wa kwao na watajifunza kutoka kwa wenyeji. Nabi na Gomes ni mifano sahihi. 

Unaweza kusema George Lwandamina (Azam FC) raia wa Zambia hana utamaudni tofauti katika maisha ya soka, sawa na Mathias Lule (Mbeya Cty) raia wa Uganda, Patrick Odhiambo (Biashara United),Francis Baraza(Kagera Sugar) raia wa Kenya. Nchi kadhaa za Kiafrika zinafanana katika suala la utamaduni hususani zilipo karibu. 

Tatu, hadhi. Makocha wa kigeni wanapandisha hadhi ya Ligi ikiwemo kuwavutia wachezaji wa kwao. Mtibwa Sugar wamemchukua Joseph Omog raia wa Cameroon. Omog ana uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania na barani Afrika kwa ujumla. 

Amekulia katika nchi ambayo imetaa nyota wengi wa soka barani Ulaya na ameshuhudia nchi yake ikifika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990. Hii ina maana hadhi ya Ligi inakuwa imeongezeka kumvuia kocha anayetoka nchi kubwa kisoka barani Afrika.

Nne, kumiminika na kuuzwa kwa vipaji. Sifa za makocha wa kigeni ni kuvutia vipaji vingine vya soka. kwa mfano wanaweza kupendekeza kwa uongozi asajiliwe mchezaji wa aina fulani kutoka kwao. 

Hali hiyo inachangia kuwavutia wachezaji wengine wanapofahamu kuwa raia mwenzao anafundisha timu ya Ligi Kuu Tanzania. Wakenya,Wacameroon,Watunisia na wengineo watakuwa na hamu ya kucheza Ligi hii kwa vile wanavutwa na raia mwenzao. 

Pia makocha hao wanaweza kutumiwa na mataifa walikotoka kutoa taarifa ya kipaji kizuri ambacho kingefaa kusajiliwa kwenye timu zao. Hebu fikiria siku klabu za Esperance,Club Africain au Etoile Du Sahel ikitaka kujua sifa za wachezaji wazuri wa Yanga. 

Bila shaka mtu wa kuzungumza naye atakuwa Nasridine Nabi ambaye atachangia kutoa wasifu na umahiri wa mchezaji au kupendekeza wamsajili mchezaji fulani. Hii inachangia vipaji kuuzwa na wengine kuja kuchukua nafasi katika klabu za ligi kuu. 

Tano, timu 11 kuajiri makocha wa kigeni ina maana uwezo wao wa kuwalipa upo. Hii ina maana pia wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa kaika klabu zetu wanalipwa vizuri kwa maizngira ya kwetu. Kwa mantiki hiyo makocha wa kigeni wanaponoa timu zetu  wanavutia wengine na wachezaji wageni wakiwa wanafahamu kuwa timu zina uwezo wa kulipa kwani bajeti zao zinaruhusu kuajiri hao.  

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Taifa Stars

Taifa Stars kiwango bora bila ushindi ni kilio 

Tanzania Sports

Newcastle United ni habari ya mjini sasa