in , , ,

JIJI LINA MSINGI WA MAWE, MUNGU KAWAPA MBAO KWA AJILI YA PAA LENU

Historia inaonesha Mwanza ni moja ya sehemu ambayo imekuwa ikitoa
vipaji vingi vya mpira kuanzia miaka ya nyuma mpaka hivi sasa. Nyakati
tofauti zimekuwa zikija na wachezaji bora tofauti kutoka jiji la
Mwanza.

Hutokosa tabasamu unapomkumbuka Nteze John Lungu kwa sababu katika
nyakati zake za mpira alihusika kwa kiasi kikubwa kujenga tabasamu la
wapenzi wa mpira ambalo limekuwa nembo na ni vigumu kufutika katika
kumbukumbu zao.

Mhuri wa uimara na ubora wake umewekwa katika mioyo yetu na hii ni
kuonesha kuwa katika kizazi chake yeye pamoja na wengine wengi
walikuwa ni nguzo imara ya furaha ya wana Mwanza na Watanzania.

Yawezekana umri ukawa tatizo na ukawa mtu ambaye hukufanikiwa kuwaona
hawa wazee wetu, lakini hapana shaka Mungu alikupa neema ya kukiona
kipaji cha Mrisho Ngassa.

Kipaji ambacho kilikuwa kinaabudiwa na kila Mtanzania, kipaji ambacho
kila Mtanzania alitamani akikiona kwenye moja ya ligi kubwa duniani
lakini ndivyo hivo Mungu alikiweka sehemu ambayo mwili na akili
havikutaka kutembea mbele.

Ni mara chache sana kwa mshambuliaji wa pembeni kuwa na magoli mengi
na wakati mwingine kuwazidi mpaka washambuliaji wa kati, hiki kitu
alikuwa nacho Mrisho Khalfan Ngassa.

Neema yote hii imetoka kwenye miamba, miamba ambayo inapendezesha jiji
la Mwanza kila upande wa pande zote za dunia. Na neema hii hii
inaonesha msingi wa soka la Mwanza umejengwa na miamba izungukayo jiji
hili.

Miamba iliyozunguka jiji la Mwanza ni ishara kubwa kuwa ndani ya
Mwanza huzaliwa miamba katika fani mbalimbali, na ndiyo maana Joh
Makini aliogopa kujiita mwamba wa Tanzania kwa sababu ya uwepo wa Fid
Q.

Hii yote inaonesha Mungu alitoa upendeleo mkubwa katika jiji la
Mwanza, upendeleo ambao uliifanya Pamba iwe timu ambayo inatoa
ushindani mkubwa.

Wana Pamba ndiyo waliohusika kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa Pamba na
kuilea Pamba, kibaya zaidi ndiyo waliohusika kuiua Pamba na imekuwa
ngumu kwao kuifufua.

Na hii ni kutokana na siasa za Usimba na Uyanga ambao kwa kiasi
kikubwa linatafuna mpira wa jiji la Mwanza.

Ilikuwa ni rahisi kwa Toto Afrika kufanya vizuri kwa sababu ya wao
kuwa timu ambayo tayari imeshajenga jina jijini Mwanza , ila kwa
sababu wameamua kuwa mtoto wa Kulwa imekuwa ngumu kwao kujiwazia
wenyewe zaidi ya kumuwazia Kulwa.

Alliance Sports Academy ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na
kuipeperusha bendera ya mkoa wa Mwanza lakini cha ajabu hawataki
kufanya hivo.

Mkoa uko njia panda, Pamba ipo lakini haipo, Toto Afrika inatumika
kwenye siasa za Usimba na Uyanga na ndiyo Kansa inayoimaliza Toto
Afrika .

Miguu imekuwa mizito kwenye hatua za maendeleo ya mpira wa Mwanza.
Nafsi zimenyong’onyea na zimekosa mfariji wa kweli kwenye huu msiba.
Kila anayekuja mbele ya wakazi wa Mwanza kama mfariji amekuwa
haaminiwi na wakazi wa Mwanza kwa hofu ya yeye pia kujiingiza katika
siasa za Usimba na Uyanga.

Na ndiyo maana ni ngumu kwa baadhi ya wakazi wa Mwanza kuamini kuwa
Mbao FC inaweza ikawa mfariji sahihi katika msiba wao.

Kashfa ya upangaji wa matokeo kwa baadhi ya timu zilizokuwa kundi moja
na mbao katika ligi daraja la kwanza ndiyo ilimpa nafasi Mbao Fc
kupanda ƙligi kuu msimu.

Kitu hiki kilikuwa kama mshangao kwao na kwa Watanzania wengi hali
iliyosababisha kuamini kuwa Mbao haitoweza kuwa na maisha marefu
katika ligi kuu, lakini tafasri imekuwa tofauti. Leo hii Mbao Fc
imefanikiwa kubaki ligi kuu tena kwa kumfunga bingwa wa msimu huu.

Kumfunga bingwa siyo habari kubwa kwangu, habari kubwa ni mafanikio ya
Mbao FC katika mashindano ambayo walishiriki msimu huu likiwemo kombe
la shirikisho la soka Tanzania yani TFF.

Ukitazama njia ambazo walipitia Mbao zinakupa taswira kuwa ndani yao
kuna kitu kikubwa lakini hajapatikana mtu wa kukifanya hicho kitu
kikubwa kung’aa.

Timu ambayo ina bajeti ndogo tena bajeti yenyewe fedha zake
zinapatikana siku chache kabla ya mechi kwa kuchangishana lakini
ikafanikiwa kufika fainali ya kombe la shirikisho la soka Tanzania (
TFF) tena mbele ya timu ngumu kama Kagera Sugar na aliyekuwa bingwa
mtetezi wa kombe hili yani Yanga .

Ni timu ambayo imeamini katika vijana na vipaji vipya kwa kuvipa
nafasi ya kucheza na kuonesha vipaji vyao.

Hii yote inaonesha wanauwezo wa kupitia njia tofauti na wenzao na
wakafanikiwa kufika mbali kama wakiungwa mkono kwa dhati na wana
Mwanza.

Ni kipindi sahihi kwa viongozi wa Mbao FC kujiepusha na siasa za
Usimba na Uyanga ili wajenge ufalme wao wenyewe wenye kujitegemea kwa
kila kitu.

Muda huu Mbao Fc ipo katika masikio na midomoni mwa Watanzania wengi
ni wakati mzuri kwa viongozi wa Mbao FC kutafuta wafanyabiashara kuja
kuwekeza kwao.

Maandalizi ya msimu ujao yanatakiwa yaanze mapema ili kuepukana na
adha waliyokutana nayo msimu huu kwa wao kupigania kutoshuka daraja
mwishoni mwa ligi.

Ushikamano na umoja wa wana Mwanza ndicho kitu ambacho kinahitajika kwa sasa.

Kwa pamoja wanatakiwa kusimama na kushikana mikono ili kuibeba Mbao Fc
juu ya mafanikio.

Fainali ya kombe la Shirikisho iko mbele yao kwa sasa, fainali ambayo
itawapa nafasi Mbao Fc kuwa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya
kimataifa .

Uwakilishi huu utatoa nafasi kwa mkoa wa Mwanza kupata fursa ya
kuangalia michuano hii ya kimataifa kwa sababu uwanja wa CCM kirumba
imeidhinishwa na CAF kutumika katika michezo ya kimataifa.

Msingi wa soka la Mwanza ni imara na unavutia , lakini tatizo paa
lilikuwa limeezekwa vibaya, muda huu wana Mwanza wamepata mbao imara
za kuezekea Paa lao.

Ni kazi kwao kujivunia ubora na uzuri wa nyumba yao, maana imechakaa
sana tangia Pamba aondoke.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

HONGERA SERENGETI BOYS, VITA BADO MBICHI..

Tanzania Sports

PAZIA EPL LAFUNGWA: