in

Jihadharini na Barcelona ya Lionel Messi

Lionel Messi

LA LIGA

DIEGO Simeone anaongoza Ligi Kuu Hispania akiwa na viporo vitatu vya mechi mkononi. Atletico Madrid wana pointi 37 kwa mechi 15, huku Real Madrid wakiwa nafasi ya pili, kisha Barcelona wamepanda hadi nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Granada.  

Ushindi wa Barcelona dhidi ya Granada ni mechi ambayo ilinivutia kwa kiasi kikubwa wikiendi hii. Baracelona ambao wanategemea kupata rais mpya mwaka huu walikipiga na Granada huku wakionesha hali tofauti ya kimcehzo, mbinu na ari ya kufukuzia taji la La Liga huku wakiwa chini ya uongozi wa Lionel Messi. 

Hakika Lionel Messi ndiye kila kitu katika timu ya Barcelona kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10. Ujio wa mchezaji chipukizi Pedri ingawa hajafikia robo ya uwezo wa Ansu Fati ambaye ni majeruhi, lakini kinda huyo amekuwa chachu na amempa tabasamu Messi namna avayocheza na kuipa Barcelona mchango muhimu kuelekea mbio za ubingwa msimu huu. 

Frank De Jong ni silaha ambayo inatumiwa vizuri na Barcelona wakati huu kupunguza majukumu ya Messi. Ukweli ni kwamba Barcelona ni timu inayotakiwa kufuatiliwa zaidi msimu huu licha ya kuanza kwa kusuasua. Barcelona hii si timu ya kubezwa ama kusema ni mbovu haiwezi kuleta ushindani na kufukuzia taji la La Liga chini ya kocha mpya Ronald Koeman.

Kilichotokea kwenye uwanja wa Los Carnenes ndicho kinanipa tafakuri kuwa Lionel Messi hayuko peke yake bali anasaidiwa na Antonio Griezmann ambaye ni chachu ya ushindi katika mchezo wa Granada. Ousmane Dembele ni nyota mwingine ambaye atakuwa msaada mkubwa kwa Barcelona. 

Beki wa kati Samuel Umtiti ni miongoni mwa nyota waliocheza mchezo dhidi ya Granada. Kwamba wachezaji wazoefu na makinda wataibuka na kitu kizuri mwishoni mwa msimu huu. Dalili za kuleta matokea mazuri zimeonekana kwenye mchezo wao na Granada.

Wengi wanaamini Barcelona imepepesuka kwa kiasi kikubwa hasa wakiukumbuka ugomvi wa nahodha wao Lionel Messi na klabu yake. Lakini Messi anawaongoza makinda kustawisha jezi za timu hiyo na bila shaka wengi wao wanajisikia fahari kucheza pamoja na nyota huyo aliyetikisa soka kwa miaka 15.

Kwanini nasema Barcelona sio timu mbaya kiasi hicho? Mwaka  2008 aliyekuwa rais wa Barcelona, Juan Laporta amewahi kusema, “Nawatahadharisha, Barcelona sio mbaya kiasi hicho,”. Maneno ya Laporta yalikuja kipindi ambacho Barcelona ilikuwa chini ya kocha Pep Guardiola.

Kipindi hicho ilidaiwa kuwa Barcelona haiwezi kufanya lolote katika mashindano ya La Liga,Kombe la Mfalme na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini kilichitokea baadaye dunia ilishuhudia kandanda la aina yake na matokeo bomba kabisa kutoka kwa Barcelona. Historia inajieleza wazi.

Kwenye mchezo wao wa wikiendi hii dhidi ya Granada tumewaona Barcelona wanaoimarika na kupanda hadi nafasi ya tatu hali ambayo italeta ushindani mkubwa. 

Ingawa Pep Guardiola hayupo Barcelona lakini Ronald Koeman sio kocha wa kubeza na anaweza kuonesha maajabu msimui huu. Sababu itakuwa rahisi, wengi wanatarajia kuwa atafeli. Hakuna anayempa nafasi Koeman kama atafanya lolote na wengi wanatarajia kuwa huenda akatimuliwa kabla au baada ya kumalizika msimu huu. 

Marc Andre ter Stegen alirudi golini kwenye mchezo wa Granada. Huyu ni silaha mojawapo ya ushindi wa Barcelona kutokana na umahiri wake. Kazi aliyofanya kwenye mchezo dhidi ya Granada kuzuia michomo ya mshambuliaji Antonio Puertas ulikuwa umahiri wa aina yake. Puertas alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Barcelona, lakini golikipa wao Stegen alikuwa imara na kufuta matumaini ya nyota huyo kupachika angalau bao moja la kufutia machozi. 

Lionel Messi amebainisha kwa vitendo kuwa anasaka tuzo ya mfungaji bora maarufu kama Pichichi na hadi sasa anaongoza orodha ya wafumania nyavu wa La Liga. Kwenye mchezo dhidi ya Granada alifunga mabao mawili hivyo kufikisha jumla 11 ya La Liga msimu huu. 

Kitu kimoja ambacho kiliwagharimu Barcelona tangu mwanzo wa msimu ni majeruhi ya wachezaji mbalimbali. Mfano kuelekea mchezo wa Granada pia ilishuhudiwa Ronald Araujo akiumia wakati wa kupasha misuli, hali ambayo ilimlazimu kocha wa Barca kumwingiza Samuel Umtiti. 

Hata hivyo kipindi cha kwanza chote Samuel Umtiti alikuwa anaugulia misuli, na alionekana wazi atarudishwa kwenye vitanda hospitalini. Hata hivyo alijitahidi kumaliza mechi yote lakini atakuwa mchezaji anayetakiwa kupatiwa matibabu haraka. Hilo ndilo tatizo linalowakumbuka Barcelona tangu kuanza kwa msimu huu.  

Antonio Griezmann anaonekana kuimarika sasa na kiwango chake kizuri na kuondoa ukame wa mabao baada ya kufunga bao lake la kwanza tangu Desemba 2 mwaka 2020. Alipachika bao hilo kutokana na kazi nzuri ya Ousmane Dembele.

Kiungo Sergio Busquets alicheza mchezo wake wa 600 akiwa amevaa jezi za Barcelona. Akiwa amejiunga mwaka 2005 na sasa ametimiza miaka 32 Busquets anaonekana bado kuwa nguzo ya Barcelona msimu huu huku Koeman akitambua na kuendelea kumtumia kama chachu ya ushindi. 

Mojawapo wa matukio ya kifundi yaliyosisimua kwenye mchezo huo ni kocha wa Granada, Diego Martinez kumwingiza Jesus Vallejo ili kuwadhibiti Barcelona ambao walionekana kulishambulia lango lake kama nyuki. Hata hivyo mbinu hiyo haikudumu kwa muda mrefu kwani Vallejo alilimwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Barcelona, Martin Braithwaite.

Kipindi hiki ni wazi Barcelona wanainua mabega yao na kuanza kuonesha zaidi makucha kuelekea kumalizika msimu huu. Ni wazi hatuwezi kusema Barcelona haina uwezo wa kutwaa taji la La Liga wakati wapinzani wake wameruhusu ifike nafasi ya tatu ikiwa inachuana na watanguliz wake Real Madrid na Atletico Madrid kuwania ubingwa. 

Ndiyo maana ninasema Barcelona sio timu mbaya kiasi hicho. Lazima timu pinzani zijihadhari na mashabiki wake waamini kuwa Koeman anaweza kufanya kitu cha ajabu msimu huu na wote wakabaki wanashangaa tu. Inawezekana wanaoibeza Barcelona wakaumbuka kam alivyowahi kusema Juan Laporta, “jihadharini, Barclona si wabaya kiasi hicho.”

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SIMBA VS PLATNUM

Thamani ya miguu ya mastaa wa kigeni wa Simba

Simba

TFF haitaki Simba kufundishwa na kocha MZAWA?