in , ,

JANUARI NI MBALI MNO KWA FC BARCELONA

 

Rafael Alcantara wa Barcelona alipata majeraha Jumatano ya wiki iliyopita kwenye mchezo  wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Roma. Majeraha ya kiungo huyo maarufu kwa jina la ‘Rafinha’ yatamuweka nje ya uwanja mbaka mwishoni mwa msimu.

Hili ni pigo kwa FC Barcelona. Rafinha katika siku za karibuni amekuwa mchezaji muhimu mno kikosini. Kwenye mechi za awali za msimu huu alikuwa akiziba pengo la Neymar kwenye nafasi ya ushambuliaji wakati mshambuliaji huyo alipokuwa akisumbuliwa na maradhi.

Hata hivyo kwa kawaida Rafinha anacheza nafasi ya kiungo ndani ya kikosi cha Barcelona. Msimu uliopita alicheza jumla ya michezo 24. Pengine hakuwa muhimu sana kutokana na uwepo wa Xavi Hernandez ambaye alikuwa akipokezana nafasi kikosini na Ivan Rakitic.

Xavi Hernandez alishatimkia Al-Sadd SC ya Qatar kabla ya kuanza kwa msimu huu. Hapa ndipo umuhimu wa Rafinha unapoongezeka hasa ikizingatiwa kuwa mchezaji huyo amekuwa akionyesha kiwango cha juu mno kwenye siku za karibuni.

Kuumia kwa Rafinha kunawaacha Barcelona wakiwa hawana mbadala wa kuaminika wa kupokezana nafasi na viungo Ivan Rakitic na Andres Iniesta ambao ndio chaguo la kwanza la Luis Enrique. Mbaya zaidi kiwango cha Rakitic kinaonekana kushuka. Hivyo anahitajika kiungo wa kuaminika wa kumpa changamoto ya nafasi kikosini.

Kiungo Arda Turan aliyetokea Atletico Madrid tayari alishasaini mkataba na FC Barcelona. Turan ana uzoefu na kiwango cha juu kuliko hata Rafinha. Hata hivyo Barcelona hawana ruhusa ya kumsajili Turan kwenye kikosi chao kwa sasa kwa kuwa wana adhabu ya kufungiwa kusajili ambayo itaisha mwishoni mwa mwaka huu.

Toni Freixa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi wa klabu hii wa mwezi Julai amewashauri Barcelona waombe kibali cha kumsajili Arda Turan. Freixa amedai kuwa kwa sasa dirisha la usajili limeshafungwa na litakapofunguliwa adhabu ambayo Barcelona walipewa na FIFA itakuwa imekwisha.

Hivyo Barcelona wanahesabiwa kuwa wamemaliza adhabu yao ya kufungiwa kusajili kwa mujibu wa Freixa kutokana na sababu hizo alizotaja. Yaani kwa kuwa hiki si kipindi cha dirisha la usajili na kitakapofika timu hiyo itakuwa imeshamaliza adhabu yake.

Akadai kuwa kwa sasa Barcelona wanaweza kuruhusiwa kusajili mchezaji mbadala kwenye kikosi kwa kuwa hilo linaruhusiwa mchezaji anapopata majeraha ya muda mrefu hata kama si kipindi cha dirisha la usajili.

Kocha mkuu wa FC Barcelona Luis Enrique haoni haja ya kujaribu kuomba kibali cha kumsajili Turan kikosini. Amesema kuwa FIFA hawawezi kuwaruhusu kwa kuwa waliwauliza kuhusu uwezekano huo kabla ya msimu kuanza lakini wakawaambia kuwa wasingeruhusiwa kufanya hivyo.

Uamuzi aliouchukua Luis Enrique ni kumjumuisha kikosini kiungo Gerard Gumbau kutoka timu ya vijana ya Barcelona ili azibe pengo la Rafinha. Kiungo huyo ana kipaji kinachotosha kabisa kuwa mchezaji nyota wa timu hiyo baadae. Lakini kwa sasa hatoshi kuziba pengo la Rafinha.

Barcelona wanalazimika kusubiri mbaka Januari ili wamsajili Arda Turan pamoja na Aleix Vidal kikosini. Hata hivyo ratiba ya Barcelona kabla ya Januari ina michezo migumu mno hivyo Januari ni mbali. Mwishoni mwa mwezi Novemba Barcelona itakutana na Real Madrid ugenini kisha itacheza na Roma baada ya siku mbili.

Baada ya hapo kuna michezo mingine migumu dhidi ya Valencia kisha Bayer Leverkusen. Huduma ya Arda Turan kama mbadala wa Rafinha ingehitajika sana kwenye mechi hizi. Lakini hataweza kupatikana mbaka Januari.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Van Gaal aota ubingwa

MZUNGUKO WA TATU LIGI KUU BARA