in , ,

JANA MLIMTEGEMEA MANJI, LEO MTENGENEZENI MANJI WENU

Mpira ni pesa, hii kauli ina maana kubwa sana ingawa sisi
tunaichukulia kawaida kwa sababu tumezoea kuchukulia vitu kawaida
katika ukawaida usio wa kawaida.

Mpira unatengeneza pesa nyingi sana kama ukiamua kuwekeza pesa , akili
na muda kwenye mpira. Vitu hivi vitatu vina umuhimu mkubwa katika
uwekezaji wa mpira biashara kwenye mpira ili upate faida.

Naaaam, faida ya kwenye mpira hupatikana kwa kuweka pesa, muda na
akili ! . Hakuna kitu chenye mafanikio makubwa ambacho kinahitaji muda
mfupi. Kila kitu chenye mkondo mkubwa wa mafanikio huitaji uwekezaji
wa muda.

Ndiyo maana hata biashara ya kuuza wachezaji inahitaji muda, biashara
hii haipo hapa Tanzania hasa hasa kwenye vilabu vyetu vikubwa. Wao
walianzisha klabu kwa ajili ya kununua wachezaji tu, ni aghalabu
kusikia Simba au Yanga imeuza wachezaji nje au ndani ya nchi kwa faida
kubwa, hata ukisikia hiyo huwa ni bahati mbaya kwa sababu hakuna
mipango ya kuonekana kwenye hii biashara.

Hawana hata mascout ambao wangetumika kwa ajili ya kusaka vipaji
vikubwa nchini ili waviendeleze kwa manufaa ya timu (ndani ya uwanja)
na manufaa ya klabu ( kuwauza), wanategemea kugombania na Simba au
Azam Fc pale Manungu. Hii ni vita ya watu wasio na akili ndiyo maana
hawana hata mipango ya kuibua wachezaji vijana.

Mipango yao ya kuibua wachezaji wenye umri mdogo kuanzia miaka sita
(6) huishia kwenye karatasi na hakuna uhalisia wowote waliouonesha
kupitia mipango yao.

Kuibua vipaji kutoka kwenye umri mdogo kuna faida kubwa sana kwa
sababu vipaji hivi hukua katika mazingira ya msingi sahihi ya mpira,
msingi ambao utawezesha kuwa na ukuta imara katika vipaji vya
wachezaji na timu kwa ujumla.

Mchezaji aliyekulia mazingira kama haya ni rahisi kumuuza nje na kupata pesa ndefu ambazo zitasaidia timu,
Ni ngumu kukuta timu yenye mazingira ya kuuza wachezaji kuwa na vilio vya
njaa. Na hiki kitu kinahitaji uwekezaji wa muda.

Uwekezaji wa muda huenda sambamba na uwekezaji wa akili. Unavyofikiria
ndivyo unavyojitengeneza wewe mwenyewe.

Ulivyo sasa hivi ni matokeo ya ufikiriaji wako, unapoona muda huu
Yanga inakosa pesa za miezi minne za kumlipa Mwalimu George Lwandamina
ni matokeo ya ufikiriaji wa viongozi waliopita na wasasa.

Nembo yao ni kubwa mno kibiashara lakini wameshindwa kufikiria namna
ya kuitumia nembo yao kibiashara ili iwe inaingiza pesa kubwa.

Kuna vitu vinaweza kuonekana ni vidogo lakini vina matokeo makubwa
sana. Mfano, wapenzi wa Yanga ni watu wanaoipenda Yanga kutoka moyoni.
Huwa wanaiunga mkono kwa hali na mali, lakini watu hawa
hawajatengenezewa mazingira yatakayowafanya wao wanufaike na timu
inufaike.

Wapenzi hawa wana familia ,ndani ya nyumba kuna vitu vingi sana
vinahitajika ili vipendezeshe nyumba. Mlangoni pazia ni kitu cha
msingi sana kwenye nyumba yoyote.

Yanga imeshindwa kuingia mkataba na wabunifu wa mapazia ambao
watatengeneza mapazia yenye nembo ya Yanga. Hata kama mapazia haya
yasipokuwa ya rangi ya njano na kijani , hata yakiwa na rangi nyeupe
lakini yawe na nembo ya Yanga. Nembo shabiki wa Yanga atajivunia
kununua, hawa watu tutawafanya wasiende kununua mapazia ambao hata
hatujui yametengezwa na nani.

Zulia la mlangoni ni muhimu sana , ukiingia ndani utakutana na kapeti,
kapeti ambalo litakuwa limebeba samani zenye nembo ya Yanga. Kiasi
kwamba kuanzia kwenye zulia, kapeti, viti, kabati mpaka vikombe na
sahani viwe na nembo ya Yanga.

Bidhaa hizi zinawafaa watu wenye hali ya juu na chini. Mazingira haya
ukiwatengenezea utawapa nafasi ya kuzidi kukunufaisha wewe kupitia
nembo yako kubwa. Na siku wakienda uwanjani watengenezee skafu, jezi
na uwauzie, hili tushaimba sana.

Nafurahia muda huu wanaelekea kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa timu
hii itasaidia timu iwe ze kujitegemea na kuachana na hulka ya
kumtegemea mtu.

Yanga kujiendesha kibiashara , kwa kujitegemea ni kitu chenye afya
kuliko kuiendesha timu kwa kumtegemea mtu. Yusuph Manji kaondoka,
timu imetetereka. Wachezaji hawalipwi mshahara, kocha kaondoka kwa
sababu hajalipwa miezi minne.

Wafikirie na jinsi ya kuongeza wadhamini ambao watakuja kupunguza
gharama za uendeshaji. Mfano wakiingia makubaliano na Gym ili
wachezaji wake wawe wanafanya mazoezi ya Gym hii itakuwa na faida kwao
Yanga na mmiliki wa Gym kwa kutangaziwa bidhaa yake. Kuna namna nyingi
za kufikiria kibiashara kama akili yako ukiamua kuiwekea mwanga ndani
yake na ukifanikisha hapo utakuwa umemtengeneza Manji wa kudumu kwenye
klabu (mfumo imara wa mapato ya klabu) na kuachana na tabia ya
kumtegemea mtu binafsi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Tulitamani Singida Iwe Azam Fc, Azam Fc inatamani iwe Singida United

Tanzania Sports

Simba inacheza kibingwa