in , , ,

HONGERENI MBAO, NI WAKATI WA KUILETA PAMBA NDANI YA MBAO.

Mwaka mpya unaanza, tukiwa tumeuaga mwaka mwaka uliopita.

Ni jambo jema na la kumshukuru Mungu kutuwezesha kuiona nuru mpya, na
kutupa pumzi mpya.

Hatukufanya mema kuzidi wengi ambao hawakuuona mwaka huu lakini ni
mapenzi yake mwenyezi Mungu.

Ni mapenzi yake Mungu pekee yanayomwezesha mwanadamu apokee mwaka mpya
kwa furaha au kwa huzuni.

Huwezi kukwepana na mapenzi ya mwenyezi Mungu, lazima ukubaliane nayo
na uyapokee kwa mikono miwili.

Ndiyo maana kwa mapenzi yake aliamua Yanga waweze kuaga mwaka wa 2018
vibaya na kuukaribisha mwaka wa 2017 vibaya.

Yeye ndiyo aliamua kuweka tabasamu kwenye uso wa mashabiki wa Mbao na
kuliondoa tabasamu kwenye uso wa mashabiki wa Yanga.

Ni jambo la kawaida ila linaumiza kama wewe ni shabiki wa Yanga na
linakera zaidi ukigundua unaaga mwaka vibaya.

Huwezi kwepa maumivu na majonzi kwenye maisha, tumeumbiwa vyote
(majonzi na furaha).

Vyote ni vya mwanadamu, ndiyo maana wakati Yanga akiwa na majonzi na
maumivu, Mbao ana furaha kubwa sana moyoni mwake.

Imekuwa ni kawaida kwa Mbao kumfunga Yanga kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Yanga hajawahi kupata ushindi kwenye uwanja wa CCM kirumba dhidi ya Mbao.

Mara nyingi amekuwa mnyonge katika uwanja huu dhidi ya Mbao.

Ni jambao linalotia moyo kuona moja ya timu ndogo inatoa ushindani
mkubwa dhidi ya timu kubwa.

Mbao wamekuwa moja ya timu ambayo imekuwa ikicheza vizuri na kutoa
ushindani mkubwa katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya timu hizi
kubwa.

Ni uwanja ambao Mtibwa aliwahi kufungwa goli 5-0.

Ni uwanja ambao Azam amekuwa akihangaika sana anapocheza na Mbao.

Hata Simba hukutana na upinzani mkubwa sana anapokutana na Mbao kwenye
uwanja huu wa CCM Kirumba.

Mbao amekuwa na tabia ya kukamia pindi anapokutana na timu kubwa, na
kutoweka mkazo anapokutana na timu ambazo analingana.

Imekuwa sifa kwake kuona timu kubwa zikihangaika katika uwanja wa CCM Kirumba.

Hii ndiyo furaha yao, kuwaona Azam FC wanatapa tapa kwao kunafurahisha
zaidi kuliko kuona Majimaji akiacha alama kwenye uwanja huu.

Huwezi kuleta ushindani kwenye ligi kuu kama timu imeamua kuwekeza
nguvu kubwa ya ushindani kwenye baadhi ya mechi na kuwekeza nguvu
ndogo kwenye mechi ambazo ni za timu ndogo.

Mbao hawatoi uzito sawa kwenye mechi za ligi kuu.

Huwezi kudiriki kusema ligi kuu ina ushindani mkubwa wakati kuna
baadhi ya timu ambazo macho yao huelekezwa kwenye baadhi ya mechi.

Ni wakati sahihi kwa Mbao kusema wametosha kufurahia kuwafunga ƳYanga
na timu kubwa pale CCM Kirumba.

Tunahitaji ligi yenye ushindani, ligi ambayo ina timu nyingi ambazo
zinapata mwendelezo mzuri wa ushindi.

Siyo ligi ambayo timu inashinda mechi dhidi ya Yanga tena nyumbani afu
inakuja kufungwa mechi tatu mfululizo.

Ni ngumu kufikia tunapopatamani kama hatuwezi kutengeneza njia ya
kufikia tunapopatamani.

Tuachane na siasa za Simba na Yanga, tukomeshe hii hali ya timu fulani
kujiona kuifunga timu fulani kubwa kwao ni kombe tosha.

Tufikirie zaidi ya hapo, tuwafikirie Mbao katika ubingwa.

Tufikirie katika kujaribu ladha tofauti, tukemee kuona ladha ile ile
ya bingwa, yani leo Simba kesho Yanga.

Tuachaneni na utamaduni huu, tuanze kufikiria kuwaza jinsi ya kutoa
ushindani ule ule kama tunaoutoa kwenye mechi dhidi ya timu kubwa.

Ushindani ambao utawezesha mechi zote za ligi kuu ambazo timu kama
Mbao basi inatoa ushindani ule ule ili kufikia mbali.

Hatuwezi kufika mbali kama maono yetu yanatazama karibu, huwezi
kuitazama kwa uzito mechi ya Simba pekee na mechi zingine ukazitazama
kwa wepesi afu ukatamani ukawa na ndoto ya kufika mbali.

Tuache kujifariji na furaha ya muda, tuwekeze kutafuta furaha ya kudumu.

Tuwekeze ili kupata timu ambayo inaushindani mkubwa kama ilivyokuwa Pamba.

Watu wa Mwanza wamekosa tena timu bora na imara tangia Pamba apotee
kwenye ramani ya mpira wa miguu Tanzania.

Wana Mwanza wanatakiwa waachane na siasa za kuzitesa timu kubwa,
wafikirie namna ya kuiandaa Pamba mpya ndani ya Mbao

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JINSI AMBAVYO LIVERPOOL WATANUFAIKA NA: Virgil van Dijk

Tanzania Sports

WACHEZAJI WANAOFAA KUZIBA NAFASI YA PHILIPPE COUTINHO PALE LIVERPOOL