in , ,

HIZI VURUGU ZINAFUATA MAELEKEZO YA KOCHA AU TUNAFURAHISHA MASHABIKI?

Hiki ndicho kipindi ambacho magazeti mengi ya michezo yanauza kuliko
kipindi chote.

Ndicho kipindi ambacho timu nyingi hasa hasa kubwa hutunishiana
kuonekana katika kurasa za mbele za magazeti.

Hakuna kipindi ambacho wamiliki wa vyombo vya habari hasa hasa
magazeti hunufaika kama kipindi hiki.

Wenyewe huombea timu kubwa isajili waiandike kwa mbwembwe. Na ndicho
kipindi ambacho baadhi ya maneno utayasikia yakitumika sana katika
kurasa za mbele za magazeti yetu.

Timu fulani yasajili beki kisiki, timu fulani yaleta mshambuliaji
machachari, timu fulani yaleta kiboko wa fulani kutoka timu fulani.
Hivi vyote ni imradi tu wawavutie mashabiki wa timu zetu hasa hasa
hizi kubwa kununua gazeti husika.

Hii yote ni kwa sababu mashabiki hawa wanapenda kusikia hivo.
Wanapenda timu yao isifiwe zaidi ya timu nyingine. Hakuna shabiki
asiyependa hata siku moja timu yake iandikwe vibaya, kila shabiki ana
sifa ya mwanamke yani lazima umsifie ili umpate.

Ndivyo walivyo mashabiki wote duniani. Ukitaka kupendwa na shabiki wa
timu fulani wewe sifia hata kibovu na hiyo ndiyo silaha ambayo
magazeti hutumia ili kuuza bidhaa zao. Kwao kumfananisha mshambuliaji
fulani kama Messi au Cristiano Ronaldo siyo tatizo kwao maana kalamu
ni yao, wataandika, watasifia, utavutika na utanunua.

Ndicho hiki hufanywa na viongozi wa timu nyingi hapa Tanzania
linapokuja suala la usajili.

Viongozi wengi hufanya usajili kwa ajili ya kumfurahisha shabiki wake tu.

Msukumo kutoka kwa mashabiki ndicho kitu ambacho hufanya viongozi
wengi wawe na maisha ya mashaka mashaka katika maisha ya uongozi wa
ndani ya vilabu hivi.

Hivo mara nyingi huogopa msukumo mkubwa unaokuja mbele yao kutoka kwa
mashabiki wa timu yao. Ili kujiongezea siku za kuishi kwa furaha ndani
ya timu, viongozi wengi hudumbukia katika shimo la kufanya usajili wa
kuwafurahisha mashabiki wao.

Kwao furaha ya kocha siyo kitu katika kipindi hiki cha usajili, jicho
lao humtazama shabiki anataka nini na siyo kocha anataka nini.

Ripoti ya kocha baada ya msimu kuisha kwao siyo ya muhimu na huwa
hawaiitaji sana sema kocha huandika tu kwa sababu anatakiwa aandike
ripoti hiyo.

Suala la yeye kutimizia kilichopo kwenye ripoti ni gumu kwani wakati
wa usajili viongozi wengi huwaangalia kutengeneza furaha kwenye nyuso
za mashabiki na siyo kufurahia kutengeneza furaha ya kocha.

Siyo kitu cha kushangaza kwa kocha kupendekeza usajili wa beki wa kati
katika usajili wake na akasajiliwa golikipa kwa sababu ya kuikomoa
timu fulani iliyokuwa inamwihitaji huyo golikipa.

Lengo kuu hapa hiyo klabu iumie, mashabiki wakasirike na mashabiki wa
upande wa pili wafurahie na wawazomee mashabiki wa upande wa pili ili
mradi siku ziende na tuzidi kunogesha neno “mtani wa jadi”.

Nahisi hapa ndipo makosa yanapoanzia kwa sisi kuitana mtani wa jadi
kwa sababu tunafanya utani mpaka kwenye mambo ya msingi.

Utani wetu hauna mipaka, sisi hadi sehemu za siri tunachezeana kwa
kisingizio cha kuitana watani wa jadi.

Kwa hiyo usije ukashangaa hata siku moja ripoti ya kocha ikipuuzwa kwa
sababu ya kudumishwa neno mtani wa jadi.

Tumekuwa watu wepesi wa kuingiza upuuzi kwenye taaluma za watu.
Hatuheshimu taaluma za watu ndiyo maana tunajivisha kila kitu sisi
tufanye.

Na mwisho wa siku tunampa mzigo mkubwa kocha kwani anakuwa amesajili
mchezaji ambaye alikuwa hamwitaji kwenye kikosi chake.

Na ndipo hapo chanzo cha timu kufanya vibaya, kwa sababu timu inakuwa
imesajili wachezaji ambao walikuwa hawahitajiki kulingana na mahitaji
ya timu husika.

Utaanzaje kumlaumu kocha kwa kufanya vibaya ilihali hukuzingatia
ripoti yake kuwa anataka wachezaji wa aina gani ndani ya kikosi chake?

Yeye ndiye mwenye jicho la kiufundi, jicho ambalo linamuonesha ni
nani anamfaa na yupi hamfai, unapofanya usajili bila maelekezo ya
jicho lake unakuwa unajikaba mwenyewe kabla timu yako haijakabwa
uwanjani.

Ndiyo maana hizi vurugu ninazozisikia kila siku napata shaka nazo kama
zinatokana na maelekezo ya kocha au zinafanywa kuwafurahisha
mashabiki.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SHIKENI KALAMU YENYE MACHO, MASIKIO NA AKILI YA KISHERIA.

MS

SAMATTA MTAA UNAKUHITAJI ILI UKUBEBE.