in , , ,

HISTORIA ITAMKUZA SALAH JUU YA KINA ABOUTRIKA

Misri imewahi kuwa na kizazi cha dhahabu, kizazi ambacho kilikuwa na
kila aina ya nyota ndani ya kikosi chao.

Kikosi ambacho ndani ya miongo mitatu kilifanikiwa kushinda kombe la
Mataifa huru ya Afrika (Afcon) Mara nne. ( 1998, 2006,2008,2010).

Kikosi hiki kilikuwa chini ya kocha Hassan Sheheta, kocha ambaye
aliipa mafanikio makubwa nchi yake ya Misri.

Alitengeneza kikosi imara ambacho kinasemekana ndicho kilikuwa kizazi
cha dhahabu.

Kizazi ambacho kiliwafanya Wamisri waone kushinda kombe la mataifa
huru ya Afrika (Afcon) kwao ni kitu cha kawaida.

Wengi walikinai ƙkombe hili , wakabaki na kiu moja tu nayo kwenda
kombe la dunia.

Mara ya mwisho kwa Misri kushiriki kombe la dunia ilikuwa mwaka 1990.
Hivo kila mtu katika miji ya Cairo, Alexandria na miji mingine ya
Misri alikuwa na shauku kubwa ya kuishuhudia timu yao ikiwa inacheza
kombe la dunia.

Imani ya Wamisiri ilikuwa kubwa sana juu ya kikosi cha Shehata kwa
sababu waliamini kikosi kile kilikuwa kinauwezo wa kuwapeleka kombe la
dunia.

Utamwambia nini Mmisri juu ya Mohamed Aboutrika akuelewe?

Kiungo ambaye kwao wao wanaamini ndiye kiungo bora kuwahi kutokea
katika kizazi cha soka barani Afrika.

Kiungo ambaye alikuwa na uwezo wa kuibeba timu mabegani mwake na kukimbia nayo.

Vipi kuhusu kipaji cha Mohamed Zidan? Kipaji ambacho kilikuwa
kinafurahisha kwa kiasi kikubwa kukitazama machoni kwa sababu ya uwezo
wake mkubwa wa kucheza mpira.

Kizazi hiki kilipita, kiliweka alama kubwa kwenye historia ya mpira wa
miguu duniani. Alama ambayo ni vigumu kufutika.

Alama ambayo itabaki kwenye kumbukumbu ya Wamisri wengi, lakini kikosi
hiki hakikudhi matarajio ya Wamisri.

Matamanio yao makubwa yalikuwa ni wao kushiriki kombe la dunia.

Walitamani kushindana na timu bora zaidi ya timu za Afrika ambapo wao
waliona imetosha kwao kuwa wababe wa Afcon , hivo walitamani kwenda
sehemu kubwa zaidi ya hiyo.

Sehemu ambayo kila jicho la dunia litashawishi ubongo kuwapigia makofi
na kukiri kwa vinywa kuwa Misri imebarikiwa kuwa na vipaji.

Lakini cha kusikitisha zaidi kikosi kile bora cha dhahabu cha kina
Shehata kilishindwa kufikia matamanio ya Wamisri.

Kilipita kizazi kile huku kikiwaacha Wamisri katika huzuni kubwa sana
ambayo ilikosa mtu wa kuja kuwafariji kwenye huzuni hiyo.

Miaka 28 imepita, miaka ya mateso na huzuni kubwa. Miaka ambayo
Wamisri walitumia muda mwingi kuwaangalia wenzao kwenye luninga
wakipambana katika kombe la dunia.

Lakini baada ya miaka 28 ametokea mfariji wao, mfariji ambaye
ametimiza matamanio yao ya siku nyingi. Matamanio ya kushuhudia kombe
la dunia huku timu yao ikiwa ndani ya mashindano.

Kikosi kilichokuja kuwafariji ni tofaufi na kikosi ambacho walikuwa
wanakitegemea siku zote.

Wamekuja kufarijiwa na watu ambao kwa asilimia kubwa hawapo kwenye
mnyonyoro wa kikosi kile cha dhahabu.

Leo hii kina Mohamed Elneny ndiyo mashujaa wapya na wakubwa katika
ardhi ya Misri.

Leo hii historia ya soka la Misri itamtazama kwa ukubwa Mohamed Salah
juu ya kina Aboutreka.

Magoli mawili ya Mohamedd Salah yamewapeleka sehemu ambayo kila Mmisri
alikuwa anatamani kufika .

Mohamed Salah amekamilisha furaha yao ambayo ilikuwa haijakamilika.
Kila mtu alisubiri kwa hamu ikamilike.

Lakini alikosekana mtu sahihi wa kuikamilisha ile furaha, lakini Salah
ndiye ambaye amekuja kukikamilisha.

Vilio vya furaha vilitawala katika nchi ya Misri, kila sehemu watu
wengi walitembea kuonesha furaha yao kwa matokeo hayo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ALEX IWOBI , NIGERIA ITAKUKUMBUKA KWENYE VITABU VYAKE

Tanzania Sports

VITU MUHIMU KWENYE MECHI ZA KUFUZU KOMBE LA DUNIA NCHINI RUSSIA 2018